Sunday, January 31, 2010

Askofu wa KKKT dayosisi ya Konde Dr. Israel Peter Mwakyolile amekemea na kulaani wafanyabiashara washirikina wanaosababisha mauaji ya watu wasio na hatia na hasa watoto wadogo.

Aliyasema hayo jana Jumapili katika ibada ya kumweka wakfu Msadizi wa Askofu Mchungaji Geofrey Mwakihaba na kuwabariki wataradhia wa uchungaji 12 wakiwemo wanawake wawili iliyofanyika katika kanisa kuu la mjini Tukuyu wilayani Rungwe.

Mwakyolile alieleza kusikitishwa kwake kuhusiana na vifo vya watoto wawili waliouawa wiki iliyopita na kutupwa katika shamba la kanisa hilo hali iliyouacha mji wa Tukuyu ukitandwa na hofu.

“Biashara hizo ninazilaani zisifanikiwe zife kwa kuwa zina vima vya damu” alisisitiza huku akiwataka wakristo wote kuwa nuru inayoangaza tofauti na vitendo hivyo na kuwataka wafanyabiashara hao kutubu mara moja kwa vitendo vinavyomuudhi Mungu.

Katika ibada hiyo iliyohudhuriwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa chini ya mkuu wa mkoa wa Mbeya John Mwakipesile aliyewakilishwa na mkuu wa wilaya ya Rungwe Jackson Msome akiwemo na mkuu wa wilaya ya Ileje Esther Wakali na mamia ya waumini takribani 1400.

Wataradhia wa uchungaji waliobarikiwa kuwa wachungaji ni Stanton Mwakalobo, Asheri Mwambulo, Felix Mbogela na Noa Mwakalundwa. Wengine ni Mathayo Mwantemanye, Neleson Mulungu, Nelusigwe Ikuka, Andagile Mwakijungu, Enock Mwakyoma, Israel Chipezya, Mbumi Tonoka na Anganile Mwangosi.

Pia katika ibada hiyo Askofu Mwakyolile amlimwingiza kazini mkurugenzi wa fedha Daniel Mbembela ambaye alimbariki kusimamia kurugenzi hiyo.

Wiki iliyopita watoto wawili wa kike Edna Daud (5) na Esther Saulo James (5) walibakwa na baadaye kuuawa kwa kunyongwa na kufichwa katika shamba la makao makuu ya kanisa la KKKT Dayosisi ya Konde eneo la Buliyaga.

Mwaka jana 2009 kuanzia mwezi Mei, Juni na Disemba watoto walipotea katika mazingira ya kutatanisha na kukutwa wakiwa wamefariki dunia huku wakiwa wamelishwa madawa ya kulevya katika maeneo mbali mbali Tukuyu mjini.

Site search

    More Text