Monday, April 14, 2014

Alishikiliwa kwa masaa matatu, hakunywa maji japo alizamishwa kwa masaa hayo, maajabu hayo!





  “Mungu asiporuhusu kufa huwezi kufa hadi aruhusu yeye” ndivyo anavyoanza kusimulia kisa cha kusisimua na cha ajabu Erika Kajuanga (70) mwanamke aliyenusurika kuliwa na mamba baada ya kushikiliwa kwa masaa matatu chini ya maji.

Erika Kajuanga ni mkazi wa kijiji cha Bujonde wilayani Kyela mkoa wa Mbeya ambaye alifikwa na mkasa wa kukamatwa na mamba mnamo Novemba 27 mwaka 2012 majira ya saa moja asubuhi alipokuwa anafua nguo kando ya mto Kiwira.

“Nikiwa nafua nguo ghafla nilishikwa na mamba ambaye alinizamisha kwenye maji akikimbia toka pale aliponikamatia na kunipeleka ndani zaidi umbali ambao wenzagu tuliokuwa tunafua nao hawakuweza kubaini”anasimulia. 

Akiwa huko chini mamba alimwingiza kwenye pango chini ya maji akiwa tayari amemvunja mikono yote miwili na kumjeruhi goti na kumuacha kwa muda baadaye mamba huyo alirejea na kumtoa pale alipomuacha na kumwinua juu na kisha kumzamisha tena.

Mama huyo alikuwa akiomba Mungu amnusuru na hatari hiyo. Fahamu zilimjia akaingiza mdomoni mwa mamba nguo aliyokuwa ameshikilia mkononi licha ya mikono hiyo kuvunjwa aliweza kuishindilia vizuri kinywani mwa mamba huyo ndipo alipomwachia na kukimbia.

Akiwa chini ya pango kwenye maji mama huyo anashindwa kujua ilikuwaje hakudhuliwa na maji kwani hadi anatoka hakunywa hata kidogo na kwamba aliwezaje kupumua kwenye maji bado kwake ni kitendawili.
Baada ya kuachiwa hakuwa na uwezo wa kuogelea hivyo alijilaza chali akitumia miguu aliweza kufika eneo lenye jiwe kubwa akiwa hapo aliwaona watu waliokuwa wanajitahidi kumtafuta akapiga ukulele wa kuomba msaada ndipo walipofika wanaume wenye mikuki na kumwokoa.

Anasema ilifika hatua alikata tamaa ya kuokoka kwani alijua mamba yule angeweza kumrudia wakati wowote kabla hajapata msaada.

Alikimbizwa katika hospitali ya Kyela na kupatiwa msaada kisha kukimbizwa katika hospitali ya rufaa Mbeya ambapo hakuweza kupata matibabu yoyote kwasababu ya kutokuwa na fedha. Aliambiwa atoe shilingi laki tatu. Hata hivyo Kajuanga anadai kuwa yalitokea mabishano kati ya wahudumu wa hospitali hiyo waliodai kuwa bibi amepona kifo cha mamba na sasa mnamwacha afie hospitali kwa kukosa matibabu.

Kama ilivyo ada ya mja hunena mahali pande mbili zikivutana Mungu huinua upande mmoja kumtetea mja wake, walijitokeza ndugu na kumsaidia kumpeleka katika hospitali ya Peramiho iliyoko Songea mkoani Ruvuma baada ya kuwepo katika hospitali ya rufaa Mbeya kwa siku tatu bila matibabu. 

 Erika Kajuanga anawashukuru watu wa Mungu ambao walijitolea na kumsaidia kwenda katika hospitali ya Peramiho ambako anaendelea na matibabu hadi leo na kwamba hali yake inaendelea vizuri baada ya mikono iliyovunjwa kuungwa vizuri.

Tukio hili liliwashangaza wanakijiji wa Bujonde wakijiuliza bibi huyo aliwezaje kuwa mikononi mwa mamba kwa masaa matatu na baadaye kuachiwa; kweli Mungu mkubwa.

 Unaweza kuona makovu makubwa mikononi mwake hapa ni baada ya kutoka katika hospitali ya Peramiho

  

Tunduma sasa karaha

Posted by Unknown On 12:34 AM No comments
Malori yanayosubiri kuvuka kwenda nchi za kusini mwa Afrika yamekwama sasa kwa takriban wiki mbili kwa kinachoelezwa kuwa ni ubovu wa barabara upande wa Nakonde Zambia. Pamoja na sababu hiyo serikali ya Tanzania haijaandaa maeneo maalum kwa ajili ya maegesho ya magari na hivyo kuwalazimu madereva wengi kuegesha magari yao kando ya barabara kuu itokayo Dar es salaam kwenda Zambia.

Huko ni kukwama kiuchumi kwani shughuli za usafirishaji zinaposimama kwa sababu zisizo za lazima kuwepo na ufuatiliaji anayesababisha achukuliwe hatua.

Hiyo ndiyo hali halisi

Site search

    More Text