Monday, February 8, 2010











Levi Eshkol, David Ben-Gurion na Golder Meir hao wote ni mawaziri wakuu wa zamani wa Israel.

Tangu Disemba 27 hadi 18 Januari 2009 vyombo vya habari duniani vilitawaliwa na taarifa za mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas la Palestina. Katika vita hiyo takriban wapalestina 1300 na Waisraeli 13 walipoteza maisha.

Dunia imegawanyika huku upande mmoja ukiunga mkono kundi la Hamas na wengine wakiiunga Israel. Ili kujua uhalisia wa mapigano hayo tazama historia ya mataifa hayo.

Madai ya Waisraeli yanaanzia katika misingi ya kidini ambapo katika Biblia (kitabu kitakatifu kwa Wakristo na Wayahudi), kitabu cha kwanza cha nabii Musa kiitwacho Mwanzo sura ya 12 inaonesha jinsi Ibrahim anavyoitwa na mwenyezi Mungu ili kumtumikia.

Eneo hilo la Palestina (zamani lilijulikana kama Kaanani)ndiyo chimbuko la dini kuu tatu zenye msingi wa Ibrahim ambazo ni dini ya Wayahudi, Ukristo na baadaye Uislam.

Dini ya wayahudi yenye misingi ya Biblia Agano la Kale likianza na vitabu vitano vya Musa (Mwanzo, Kutoka, Hesabu, Mambo ya Walawi na Kumbukumbu la torati), Ukristo ukianza misingi kwenye Agano la Kale hadi Agano Jipya na Uislam ukishika vitabu vinne Tourat ya nabii Musa (a.s), Zabur ya nabii Dawood (a.s), Injili ya Issa bin Mariam (a.s.) au Yesu na Quran ya Muhamad (s.a.w)

Ibrahim mwenyeji wa Uru wa Ulkadayo (Mesopotamia) leo Iraq wa kabila la Waebrania anahama kutoka Iraq na kwenda Haran Syria na baadaye kutelemkia Kaanani (Uyahudi) ambapo Mwenyezi Mungu anamtokea katika njozi na kumwapia Ibrahimu kuwa ardhi yote hiyo amepewa yeye na uzao wake na kuahidiwa baraka yaani kubarikiwa kwa kila atakaye mbariki na kwamba jamaa zote za dunia zitajibarikia.

Pamoja na ahadi hiyo Mungu anamwambia nabii Ibrahimu kuwa uzao wake utakwenda utumwani Misri kwa miaka mia nne hadi kizazi cha nne ndipo watakapookolewa na kupandishwa Kaanani (Palestine).

Mizizi ya ugomvi huo inaanzia karne ya 19 wakati wa vuguvugu la utaifa la Uzayuni na Uarabu (Arab nationalism) vuguvugu la wayahudi (Jewish National Movement) lilianzishwa kuwa la kisiasa mwaka 1892 dhidi ya Urusi na Ulaya. Mkakati ulianza kwa wayahudi wote popote walipo kurejea katika nchi ya Palestina ambapo walipachukulia kuwa ndiyo nchi yao ya asili.

Katika kutimiza azma yao World Zionist Organization na Jewish National Fund walihimiza uhamiaji na kufadhili ununuzi wa ardhi chini ya utawala wa Ottoman na Uingereza katika Palestina.

Mgongano huo ukianzishwa na Uingereza kwa kile kilichafahamika kama Hussein-McMahon Correspondence na Balfour Declaration of 1917, na kufuatiwa na milipuko ya mapigano ya mara kwa mara kati ya Wayahudi na Waarabu katika eneo la Palestina.

Hakuna asiyekumbuka jinsi kiongozi wa Wanazi Adolf Hiltler alivyowafanyia wayahudi kwa maangamizi makuu ya Nazi Holocaust, ikiwa ni jitihada ya kulifuta taifa hilo..

Azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 1947 liliridhia kugawanywa kwa nchi ya Palestina kwa wayahudi na wapalestina ambapo wayahudi walikubali na wapalestina wakiungwa mkono na Umoja wa Nchi za kiarabu wakikataa na kusababisha kuzuka vita baina yao.

Vita hivyo viliwafanya wapalestina kuhama na kukimbilia nchi jirani za kiarabu wakiwa wakimbizi yaani Al-Naqba.

Israeli ilijitangazia uhuru wake Mei 14 mwaka 1948 kufuatia uhuru huo mataifa ya kiarabu Misri, Lebanon, Syria, Jordan na Iraq yaliivamia Israeli na kuzuka vita ya iliyojulikana kama 1948 Arab-Israel war. Israeli iliibuka kidedea ikiyateka maeneo zaidi ya ramani ya awali na kugawa mji wa Yerusalem.

Mwaka 1964 wapalestina walianzisha chama cha Palestinian Liberation Organization (PLO) ambacho hakikutambuliwa na Israeli.

Katika vita vya Siku Sita 1967 vya Israeli na waarabu ambavyo Israeli ilishinda kwa kishindo ikiacha hasara kubwa kwa maadui zake viliifanya nchi hiyo kujiongezea ukubwa mara tatu ya ule wa awali.

Siri ya ushindi wa vita hivyo ulitokana na mbinu na maandalizi mazuri yaliyokuwa yamefanywa na hasa ni kule kuvamia kabla ya adui hajakushambulia. Kama wangesubiri washambuliwe basi Israeli ingefutwa katika ramani ya dunia kama waarabu walivyokuwa wameazimia.

Vita hiyo ya 1967 Israeli ilipigana na Misri, Syria, Lebanon, Jordan zikisaidiwa kijeshi na Sudani, Iraq, Algeria nchi zilizopeleka askari na silaha, Urusi ikisaidia mataifa hayo kwa wingi wa silaha.

Kabla ya vita mataifa ya Marekani, Uingereza na Ufaransa yalipeleka silaha kwa Israeli na kuifanya isiwe na wasiwasi katika matumizi ya silaha.

Nini chanzo cha vita hiyo? Israeli na majirani zake walikuwa wakiishi katika hali ya uhasama tangu 1948 baada ya azimio la umoja wa mataifa la mwaka1947, lililoamuru kugawanywa kwa nchi hiyo, waarabu walikuwa bado wanayo hasira juu ya uwepo wa taifa hilo mashariki ya kati.

Viongozi mbalimbali wa nchi za kiarabu waliazimia kuifuta Israeli kwenye ramani ya dunia. Israeli iligombana na Syria ilipoanza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya maji kuyatoa mto Jordan na kusambaza katika nchi hiyo. Jeshi la Syria likatumia milima/miinuko ya Golan ilinayopata futi 3000 juu ya Galilaya kushambulia vijiji na mashamba.

Mashumbulio ya Syria yaliongezeka sana mwaka 1965 -66, Israeli ikilalamika Umoja wa Mataifa ambao ulisisitiza kuacha mapigano bila kuchukua hatua yoyote kwa Syria ambapo hata ulipotoa azimio la kulaani mashambulizi hayo yalipingwa kwa kura ya veto na Urusi.

Mashambulizi hayo yalienda sanjali na vitendo vya kigaidi dhidi ya taifa hilo ambapo mwaka 1965 Rais wa Misri Gamal Abdel Nasser alisema “hatutaingia Palestina nchi ikiwa imefunikwa kwa mchanga bali damu”. Baada ya miezi michache Nasser alisema tena kuwa azma ya waarabu ni kuona wapalestina wanakombolewa, kwa kifupi ni kuiondoa dola ya kiyahudi kwa maangamizi.
Aprili 7, 1967 Syria ikitumia ndege aina ya MiG21 ilizokuwa imepewa na Urusi ilishambulia vijiji (kibbutzim) kutokea Miinuko ya Golan, Jeshi la Israeli lilitungua ndege sita za Syria.

Urusi iliipa taarifa isiyo sahihi Syria kuwa Israeli inajiandaa kwa vita licha ya Israel kukanusha lakini Syria ilijipanga ikiweka makubaliano ya ushirikiano na Misri.

Tarehe 15 Mei, 1967 siku ya uhuru wa Israeli, majeshi ya Misri yalivuka kuelekea Sinai karibu na mpaka na Israeli ambapo siku tatu baadaye tarehe 18 jeshi la Syria likajipanga kwa vita katika milima ya Golan.

Baada ya majeshi ya Misri na Syria kujipanga kwa vita, Gamal Abdel Nasser aliamuru jeshi la umoja wa mataifa UN Emergency Force (UNEF), lililokuwa Sinai likiikinga Israeli tangu 1956 kuondoka mara moja bila kushirikisha umoja huo.

Mei 22, Misri ilifunga mlango bahari wa Tiran na kuzuia meli zote za kutoka mashariki kuingia Israeli na kuzuia meli za Iran zilizokuwa zinapeleka mafuta ya petroli na kuifanya nchi hiyo kutokuwa na njia inayopitika (uamuzi wa Misri ulikiuka sheria za kimataifa).

Radio Sauti ya Waarabu ikisema “kwa kuwa sasa jeshi la kimataifa lililokuwa linaikinga Israeli limeondoka hatutavumilia zaidi wala kulalamika umoja wa mataifa ila jambo moja tutakalofanya ni kuipiga vita na kutokomeza siasa za kizayuni”.

Naye waziri wa ulinzi wa Syria Hafez Assad alisema “majeshi yetu yako tayari kuifuta Israeli” nakuu kwa kimombo ‘Our forces are now entirely ready not only to repulse the aggression, but to initiate the act of liberation itself, and to explode the Zionist presence in the Arab homeland. The Syrian army, with its finger on the trigger, is united....I, as a military man, believe that the time has come to enter into a battle of annihilation” alisema hayo Mei 20, 1967.

Rais wa Marekani Johnson alilaani na kusema kitendo cha Misri ni kinyume na sheria ya bahari iliyopitiwa mwaka 1958 ambapo umoja wa mataifa ulitambua haki ya Israeli kutumia mlango bahari wa Tiran (Straits of Tiran) kupitisha meli.

Nasser aliendelea na vitisho akiitaka Israeli kuingia vitani akidai kuwa hawatasikiliza shauri lolote la masikilizano kwani wao wako vitani na Israeli tangu mwaka 1948. Aliongeza kusema kuwa majeshi ya Misri, Jordan, Syria na Lebanon yametulia mipakani mwa Israeli na nyuma yao yapo majeshi ya Iraq, Algeria, Kuwait, Sudan, Saudi Arabia na ulimwengu wote wa kiarabu. Alijigamba zaidi kwa kusema kwa tendo hili dunia yote itastaajabia na kujua kuwa waarabu wapo wamejizatiti kwa vita.

Rais wa Iraq Abdur Rahman Aref alisema “Uwepo wa taifa la Israeli ni kosa ambalo ni lazima lirekebishwe, huu ni wakati wa kufuta aibu ambayo tumekuwa nayo tangu 1948, lengo letu ni kuifuta Israeli kwenye ramani”. Iraq ilipeleka majeshi yake Juni 4 kujiunga na Misri, Jordan na Syria.

Majeshi ya kiarabu yanayokadiliwa askari 465,000, zaidi ya vifaru 2,800, na ndege 800 viliizunguka Israeli.

Kipindi hicho Israeli ilikuwa kwenye hali ya tahadhari kwa wiki tatu muda huo iliutumia kuingiza silaha toka mataifa ya magharibi Marekani, Ufaransa na Uingereza. Silaha zilishushwa katika mji wenye bandari wa Haifa.

Israeli kwa kuwafahamu adui zake walivyo waliwafanyia kamchezo ka hadaa, kwanza ilifungua mpaka wake na Misri ili kuruhusu wapelelezi wa Misri kuingia na kutoka. Pili oparesheni ya kuhamisha silaha zilizowasili katika mji wa Haifa wakazipeleka ghuba ya Aqaba eneo lenye pori na miamba wakati wa mchana na kuzirudisha Haifa usiku na kuzihifadhi kwenye mahandaki.

Jambo jingine lililowasaidia Israeli ni hadaa iliyofanywa, Waarabu walipotangaza vita na kuitisha Israeli, iliwaita makamanda wote waliokuwa likizo kurudi kazini na mawaziri waliokuwa ziarani kurudi mara moja, jambo lililofanywa na Misri pia.

Baada ya wiki hizo tatu za maandalizi ya nguvu Israeli ikatangaza kuwa makamanda waliokuwa likizo waendelee na likizo zao inaonesha waarabu walikuwa wanawatisha tu hakutakuwa na vita.
Kipindi hicho Marekani ilijaribu kuzuia vita kwa kuishauri Misri kusitisha mpango wa vita lakini haikuwezekana kumshauri raisi wa Misri Gamal Abde Nasser hali iliyomfanya Rais wa Marekani Johnson kuonya kuwa “Israeli haitakuwa pekee vitani labda ikitaka kuwa hivyo”

Juni 5, 1967 waziri mkuu wa Israeli Levi Eshkol aliamuru kuishambulia Misri, hapo Israeli ilikuwa peke yake, lakini yenye makamanda waliojizatiti kwa mkakati maalum. Jeshi lote la anga la Israeli ukiacha ndege 12 tu ziliachwa kulinda anga la Israeli, majira ya saa 1.14 asubuhi (saa moja asubuhi) walipiga mabomu viwanja vyote vya ndege za kivita vya Misri wakati marubani wa ndege hizo wakipata kifungua kinywa.

Ndani ya masaa mawili ndege 300 za Misri zilikuwa zimeshapigwa mabomu na kuharibiwa kabisa, masaa machache baadaye ndege za Israeli zilishambulia majeshi ya anga ya Jordan na Syria na kiwanja kimoja cha Iraq.

Jioni ya siku ya kwanza ya vita ndege zote za Misri na Jordan na nusu ya ndege za Syria zilikuwa zimeharibiwa zikiwa viwanjani. (ujanja wa kuzipiga zikiwa kwenye hanger kabla hazijaruka ulitumika).

Misri iliyokuwa na nguvu za kijeshi na jeshi kubwa la ardhini lenye vifaru na magari ya vita ilianza matayarisho ya kuyavusha kwenye mfereji wa Suez (madarajani) likafauru kuvusha askari 20,000 hadi penisula ya Sinai.

Israel ikiwa inaangalia mwenendo wote wa majeshi ya Misri iliacha operesheni hiyo ifanyike ya uvushaji askari na silaha kuelekea Sinai na kisha ikatuma ndege zake kuvunja madaraja ya Suez na kuhakikisha hakuna msaada wa kijeshi wala chakula utakaovuka kusaidia kikosi kilichokwisha vuka.

Kisha vilianza vita vya ardhini ambapo mapigano makubwa ya kihistoria ya vifaru yalitokea baina ya majeshi ya Misri na Israeli katika jangwa la Sinai.

Baada ya Jordan kushambuliwa wapalestina wapatao 325,000 walioishi Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan walilazimika kukimbia na kwenda nchini Jordan kuepuka vita.

Kikosi kidogo cha mashujaa wa Israeli kiliwekwa kuzuia majeshi ya Syria wakati vita vikali vikiendelea baina ya Israeli na Misri na Jordan hadi walipoona wamedhoofisha majeshi hayo ndipo kikosi kizima cha jeshi la anga kiliposhambulia ngome ya Syria kwenye milima Golan, Juni 9, baada ya siku mbili za mashumbulizi ya nguvu (heavy bombardment) walifaulu kupenya safu ya Syria.
Baada ya siku sita za mapigano Israeli ilikuwa na uwezo wa kuingia Cairo, Damascus na Amman bila kikwazo, wakati huo lengo la kuiteka Sinai na Miinuko ya Golan lilikuwa limefikiwa. Viongozi wa Israeli hawakuwa na nia ya kupiga miji mikuu ya nchi hizo, jambo ambalo walikuwa na uwezo nalo.
Zaidi ya hayo Urusi ikiwa imechanganyikiwa na mafanikio ya Israeli ikawa inatishia kuingilia vita. Wakati huo waziri wa Mambo ya nje (Secretary of State kama wanavyomwita) wa Marekani Dean Rusk aliishauri Israeli kukubali wito wa kusimamisha mapigano, Israeli ilikubali Juni 10 ilisimamisha mapigano.

Ushindi wa Israeli uliigharimu. Katika kushambulia milima ya Golan wanajeshi 115 wa Israeli walipoteza maisha ikipoteza ndege 46 kati ya 200 wakati upande wa waarabu Misri askari 15,000, Syria 2500 na Jordan 800.

Mwisho wa vita Israeli ilikuwa imejiongezea ukubwa wa eneo mara tatu kutoka maili za mraba 8000 hadi 26,000, ushindi huo uliifanya Israeli kuutwaa mji wa Yerusalem, mkono bahari wa Sinai, Golan Heights, Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan.

Licha ya vita hiyo Israeli iliwashauri wapalestina kuendelea kuishi chini ya utawala wa Israeli ambapo baadhi ya familia za wapalestina zilizokuwa zimetengana waliweza kuungana na wengine hawakuwa na imani na Israeli.

Mwezi Novemba 1967, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio na 242 lililowataka Israeli na Waarabu kuwa na amani ambapo Israeli ilitakiwa kuondoka katika Ardhi ilizoteka kwa makubaliano ya kuwa na amani na majirani zake.

Mwandishi maarufu wa habari za Waarabu katika Israeli Don Peretz aliyetembelea Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan siku chache baada ya vita alithibitisha kuona jinsi Israeli ilivyojitahidi kurejesha hali ya kawaida ya maisha na kuzuia kuhama kwa waarabu maeneo hayo.

Mgogoro mwingine uliibuka mwaka 1973, vita vilivyojulikana kwa jina la Yom Kippur, waziri mkuu wa Israeli akiwa Golder Meir (Iron Woman) ambavyo Israeli ilipigana bila ya maandalizi yoyote kwani ilishambuliwa kwa kustukizwa.

Golder Meir ambaye alichaguliwa kuchukua nafasi ya Levi Eshkol kufuatia kifo chake cha ghafla Februari 26, 1969 na Meir kuanza kazi hiyo Machi 17 mwaka huo akiwa na sifa kem kem ikiwepo ya kufanikisha serikali ya mseto mwaka 1967 baada ya vita ya siku sita chama cha Mapai kilijiunga na vyama vingine vya Rafi na Ahdut HaAvoda na kuunda Israel Labour Party.

Ni katika kipindi cha Golder Meir kabla ya vita ya Yom Kippur yalitokea mauaji ya wanamichezo wa Israeli huko Ujerumani waliposhiriki michezo ya Olimpiki 1972 (1972 Summer Olympics) mauaji yaliyojulikana kama Mauaji ya Munich (Munich massacre) ambapo jumla ya wanamichezo 11 waliuawa na kikundi cha wapalestina kiliichoitwa Black September Organization.

Kwa ujasiri mkubwa baada ya kuona jumuia ya kimataifa haijachukua hatua stahili, Golder Meir aliamuru shirika lake la kijasusi Mossad kuwasaka na kuwaua wote walioshiriki kupanga mauaji hayo ambayo watekaji nyara walidai kuachiwa huru kwa wafungwa 363 wa kipalestina na wengine walioshikiliwa katika magereza ya Israeli. Operasheni hiyo ilijulikana kama Operesheni Ghadhabu ya Mungu au Operesheni Singe. ( Operation Wrath of God au Operation Bayonet)

Katika operesheni hiyo ambayo ililenga kulipiza kisasi kwa wote waliohusika kupanga mauaji hayo wakiwepo baadhi ya wanachama wa kundi la PLO na Black September Organization ambapo mauaji yalitekelezwa kwa siri na kundi la watu 15 waliogawanywa katika squad tano.

Vita ya Yom Kippur au Ramadhan war au vita vya Oktoba kama vinavyojulikana vilipiganwa toka Octoba 6 hadi 26 mwaka 1973 umoja wa mataifa ulipoilazimisha Israeli kusimamisha vita na hasa baada ya Israeli kukizingira kikosi kikubwa cha tatu cha Misri (Third Army).

Mwanzoni waarabu walionekana kushinda vita na kusababisha hasara kubwa kwa jeshi la Israeli lakini upepo uligeuka ambapo Israeli iliwapiga adui zake na kupenya hadi ukingo wa magharibi wa bahari ya Shamu (walivuka mfereji wa Suez)

Hata hivyo Idara ya Usalama ya Israeli ililaumiwa kwa kutokuwa makini kwani walionywa mara kadhaa kuhusu kusudio la waarabu la kuishambulia Israeli.

Vilianza kwa mashambulizi ya ghafla ya Misri na Syria siku ya sikukuu kubwa ya wayahudi ya kidini ambapo mataifa hayo mawili yaliishambulia Israeli kwa nguvu na kuonekana kama watashinda vita katika masaa 24 hadi 48 ya kwanza baada ya hapo hali iligeuka.

Katika wiki ya pili ya mapigano Syria ilikuwa imesukumwa kutoka milima ya Golan na kwa upande wa Misri vikosi vilisukumwa hadi kusini mwa Sinai na kisha kikosi cha Israeli kikapenya kati ya vikosi viwili vya Misri na kuvuka mfereji wa Suez na kukizingira kikosi cha tatu (Third Army) cha Misri.

Jeshi la Misri lililokuwa limevuka mfereji wa Suez (mpaka wa vita vya 1967, mstari wa kusimamisha mapigano) likajigawa Ukanda wa Gaza na kusini ukingo wa mashariki wa Suez likavunja ngome iliyojengwa iliyoigharimu Israeli USD 500 ambayo ilipewa jina la Bar Lev Line kwa heshima ya Jenerali Chaim Bar-Lev.

Kuzingilwa kwa kikosi huko kuliipa nguvu Israeli wakati wa mazungumzo yaliyokuwa kiini cha mkataba wa Camp David, Israeli ilitaka kukiangamiza kikosi hicho ambapo Misri ilibidi ijisalimishe ili kuokoa maisha ya wanajeshi wapatao 20,000.

Marekani ilitumia mwanya huo kuilazimisha Misri kufuta maombi ya msaada iliyokuwa imeomba toka Urusi na kuahidi kuisaidia na hivyo kupunguza ushawishi wa Urusi eneo hilo ambapo mambo yalihitimishwa kwa mkataba wa Camp David uliopatanisha Israeli na Misri hadi leo.
Baada ya kifo cha Gamar Abde Nasser rais wa Misri alitawala Anwaar Sadat ambaye alikuwa ametangaza mwaka 1972 kuwa ameamua kuingia vitani na Israeli na kwamba ameandaa wanajeshi milioni moja ambao wako tayari kujitoa muhanga ili kukomboa maeneo ya Sinai.

Kwa kauli hiyo mwishoni wa 1972 alinunua ndege za kivita MiG-21, makombora ya kutungulia ndege ya SA-2, SA-3, SA-6 na SA-7 , na vifaru aina ya T-55 na T-62, silaha za kulipulia vifaru RPG-7 na makombola ya vifaru ya AT-3 kutoka Urusi.

Sadat akiipa jina la Operesheni Badr (neno la kiarabu lenye maana ya mwezi mpevu) akilinganisha na Vita vya Badr ambavyo waislam waliwashinda Wakuraish wa Maka akikusudia kurudisha heshima ya Waarabu waliyopoteza katika vita ya 1967.

Habari za kijasusi ziliifikia Israeli kuwa Misri ilipanga kuivamia Israeli lakini isingefanya vile bila kupokea ndege za MiG-23 na makombola ya Scud ambayo yangetumika kuibomoa miji ya Israeli.
Taarifa hiyo iliifanya Israeli isiwe makini na kudhani vita isengetokea katika muda mfupi hivyo.
Mikakati ya vita iliyofanywa na Sadat na mwenzie Assad wa Syria ilikuwa kuivamia Israeli siku ya sikukuu kubwa ya Yom Kippur ambapo ilikuwa ni siku ya mapumziko, hakuna kuwasha mioto wala kuendesha magari na hivyo kufanya kila kitu kuwa kimya kabisa.

Hali hiyo iliwasaidia Israeli kwani walipovamiwa ghafla iliwawia rahisi kutumia barabara kujipanga haraka kwani hakukuwa na msongamano wa magari barabarani, pia iliwakusanya maaskari wa akiba kirahisi kwani wengi walikuwa kwenye masinagogi wakisali.

Mbinu nyingine iliyotumiwa na Misri ni kuwapa likizo maaskari wa akiba ambapo Nasser aliruhusu askari 20000 kwenda mapumzikoni na wengine kwenda Hija.

Usiku wa Septemba 25 mfalme Hussein wa Jordan aliruka kwa ndege kwa siri hadi Tel Aviv kumwonya waziri mkuu wa Israeli Golder Meir juu ya shambulio lililopangwa dhidi yake jambo ambalo walipuuza.

Mwezi huo Israeli ilipata maonyo kumi na moja toka vyanzo vya kuaminika lakini mkuu wa Mossad Zvi Zamir alipuuza. Lakini Golda Meir, Moshe Dayan, na Jenerali wa Israeli David Elazar walikutana saa 2:05 asubuhi ya siku ya Yom Kippur, masaa sita kabla ya shambulio.
Golder Meir alikataa kuanzisha shambulio akihofia kutopata msaada wowote toka nje. Wakati huo nchi za Ulaya zilikuwa zimeacha kuisaidia Israeli silaha. Mara waziri huyo alipotoa uamuzi alipokea ujumbe kutoka kwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Henry Kissinger kuwa Israeli isishambulie isubiri tu.

Vita hiyo ambayo kwa sehemu kubwa Israeli ililemewa na kupata hasara kubwa kwani katika masaa 27 ya kwanza ilikuwa imepoteza ndege 30 na vifaru 300 katika shambulio la Misri la Bar-Lev huku jeshi hilo la Misri likiwa limesonga mbele kwenye jangwa la Sinai kilomita tano.

Israeli ilibidi ibadili mbinu za kivita kwani makombora ya ulinzi wa anga ya SAM yaliwazidi nguvu, wakaamua kutumia jeshi la miguu (Infantry), kikosi hicho kilifaulu kwa sehemu kubwa hadi kupenya hadi kwenye safu yalikowekwa makombola hayo na kuyaharibu na hivyo kudhoofisha mfumo wa kujikinga wa Misri.

Baada ya kudhoofisha mfumo huo wa ulinzi ndipo jeshi la anga la Israeli likazidisha mashambulizi. Siku iliyofuata, Oktoba 15, Israeli ilianzisha Operesheni Abiray-Lev (yaani stout-hearted men au operesheni ya majasiri/mashujaa).

Divisheni iliyoongozwa na Meja Jenerali Ariel Sharon ilishambulia safu za jeshi la Misri eneo la Ismailiya kati ya kikosi cha pili kilichokuwa kaskazini na cha tatu kusini (Second and Third Army) na kufaulu kupenya hadi Suez na kuvuka.

Baada ya siku chache Israeli ilijenga madaraja manne kuvuka mfereji wa Suez mwisho wa vita Israeli ilikuwa ndani ya Misri kilomita 101 kutoka mji mkuu wa Misri Cairo.

Kwa upande wa Syria hali ilikuwa tofauti kidogo, pamoja na kuwa na silaha kama zile za Misri vita vilikuwa vikali ambapo ndege za Israeli zikikwepa kutunguliwa zilikuwa zikipita uwanda wa chini wa Jordan kisha kuibukia Syria na vifaru vingi vilipelekwa huko.

Viongozi wa Israeli waliithamini sana milima ya Golan na hivyo kupeleka nguvu zote hapo kwani jeshi la Syria lingefaulu kuteka milima hiyo ingelikuwa rahisi kupita hadi Tiberias, Safed, Haifa, Netanya, na Tel Aviv.

Askari wote wa akiba walipelekwa milima ya Golan wakipewa vifaru na kuendelea na mapambano, hapo ndipo alipoibuka shujaa wa vita hivyo Luten Zvika Greengold ambaye alifika jioni hiyo kwenye uwanja wa mapambano, alikuwa peke yake akitumia kifaru chake kupambana na majeshi ya Syria akiyapiga hadi msaada ulipofika.

Masaa 20 baadaye Zvika Force jina alilobatizwa alitumia kifaru chake kuingia katikati ya vifaru vya Syria na kuvipiga huko na huko ambapo alibadili vifaru sita, wakati mwingine akijichanganya na kikosi cha vifaru mara nyingine peke yake, alijeruhiwa, aliunguzwa moto lakini aliendelea na mapambano kwa kitendo hicho Zvika alitangazwa kuwa shujaa wa vita hivyo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio namba 338 la kusitisha vita baada ya Marekani na Urusi kukubaliana Oktoba 22 ambalo lilianza kutekelezwa masaa 12 baadaye.

Baada ya kuanza utekelezaji wa azimio hilo Misri ilishambulia mara kadhaa vikosi vya Israeli ikiharibu vifaru 9, kwa kulipiza kisasi Israeli ilielekeza majeshi yake kusini na kukizingira kikosi cha tatu cha Misri baada ya Jenerali David Elazar kuomba idhini toka kwa Moshe Dayan kwani zoezi la kusimamisha mapigano lilianza kutekelezwa wakati Israeli imebakiza mita chache kufikia malengo wakateka barabara kuu ya Cairo kwenda Suez.

Asubuhi ya Oktoba 23, Urusi iliilaumu Israeli kwamba majeshi yake yalionekana yakielekea kusini Henry Kissinger akampigia simu Golder Meir kuwa unawezaje kutambua mstari wa kusimamisha mapigano jangwani ambapo Meir alimjibu kuwa wote watajua tu akiwa na maana watajijua na jeuri yao, muda mfupi baadaye Kissinger alipata taarifa za kuzingirwa kwa kikosi cha tatu (Third Army).

Kissinger aligundua kuwa hiyo ni nafasi ya pekee kwa Marekani kuibana Misri ili kuiondoa kwenye ushawishi wa Urusi, kwa kweli Misri haikua na ujanja wowote zaidi ya kuitegemea Marekani kuizuia Israeli isikiangamize kikosi kilichozingirwa ambacho hakikuwa na chakula wala maji.
Wakati huo Rais wa Urusi Leonard Brezhnev alimtumia barua Rais wa Marekani Richard Nixon akisema kuwa Urusi na Marekani kwa pamoja visimamie usitishaji huo wa mapigano vinginevyo Urusi ingeingilia kuisaidia Misri.
Urusi ilikuwa imeshaandaa vikosi na baadhi yake ikawa imevisafirisha toka Urusi hadi kwenye kituo chake cha kijeshi cha Yugoslavia na kupeleka kikosi cha wanamaji 40,000 kwenye bahari ya Mediterrenea.

Kwa bahati mbaya barua hiyo ilifika Nixon akiwa amelala hivyo Kissinger na maafisa wengine wa Ikulu akiwemo Katibu wa ulinzi James Schlesinger, Mkurugenzi wa CIA William Colby na Mkuu wa WhiteHouse Alexander Haig (Kashfa ya Watergate ikiwa kileleni) waliishughulikia.

Wakubwa hao bila kumshirikisha Rais Nixon wakajibu kwa jina la Nixon kwa Urusi na kuiambia Misri ijitoe katika ushawishi wa Urusi vinginevyo Urusi ikiingilia na wao wataingia vitani, hilo likawa tishio la vita ya tatu ambayo ingekuwa ya Nuclear.
Urusi ilishangaa na hofu iliyowakumba Marekani hata mkuu wa KGB Yuri Andropov akasema hali ni tete hatuwezi kuruhusu vita ya tatu.

Asubuhi yake Misri ilikubali ushauri wa Marekani na kutangaza kufuta ombi la msaada iliyokuwa imeomba awali na Urusi ikakiri kushindwa vita kwa waarabu na huo ukawa ndiyo mwisho wa mgogoro.

Kutekelezwa kwa wito wa kusimamisha mapigano baina ya Misri na Israeli kuliichanganya Syria iliyokuwa imejiandaa upya kuishambulia Israeli tarehe 23 Oktoba baada ya kutafakari ikajua kuwa nguvu yote ya Israeli ingehamia kwake na kupiga Damascus hivyo Assad akatangaza kusimamisha mapigano Oktoba 23, na Iraqi ikawarudisha nyumbani askari wake.

Hata hivyo baada ya vita hiyo Golder Meir alijiuzulu kufuatiwa lawama za kutojiandaa kwa taifa hilo kivita (utayari wa vita) baada ya tume ya Agranat Commission kuelekeza lawama zote kwake na Yitzhak Rabin akamrithi mnamo Juni 3, 1973.

Mwaka 1975, Meir alituzwa Tuzo ya Israeli ( Israel Prize ) kwa mchango wake maalum kwa taifa la Israel. Alifariki Disemba 8, 1978 kwa saratani mjini Jerusalem akiwa na umri wa miaka 80.

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text