Saturday, September 20, 2014

Posted by Unknown On 7:25 AM No comments
Barabara kuu ya Dar es Salaam - Lusaka Zambia maarufu kwa jina la Tanzam Highway eneo la Songwe kwa Feston linaharibika baada ya wananchi wa eneo hilo kufungulia maji ya mfereji na kufanya bwawa kando ya barabara bila kuelewa madhara yake.

Mhandisi wa Tanroad mkoa wa Mbeya James Nyakabari hajaona hilo. Pia maeneo mengi kuanzia Tunduma hadi Mlowo yameharibiwa na mifugo, wenda kwa miguu na magari yanayochepuka na hivyo kula mabega ya barabara (Road shoulders) zaidi ya mita 2.

Ukarabati wa mara kwa mara unahitajika ili kuziba nyufa badala ya kungoja kujenga kuta.

Hii ndiyo hali halisi ya bwawa hilo kando ya Tanzam Highway kwenye kizuizi cha ukaguzi ushuru wa mazao


Maji yakitiririka toka kwenye mfereji wa umwagiliaji na kuingia kando ya barabara ya lami


 Ndoo zinazotumika kuchotea maji kwa ajili ya kuoshea magari na pikipiki


NFRA kununua tani 200,000 za mahindi

Posted by Unknown On 7:06 AM No comments
Ununuzi wa mahindi ulioanza wiki iliyopita utapunguza kwa sehemu kubwa ukosefu wa soko uliojitokeza kwa msimu huu 2014/15 ambapo wakulima waliuza kwa wafanyabiashara kwa shilingi 24,000 kwa plastic kilo 20 badala ya shilingi 500 kwa kilo inayotolewa na Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa.

Licha ya ununuzi huo serikali inapaswa kubuni shirika litakalofanya biashara ya ununuzi na usagaji wa nafaka ili hata maamuzi ya kuuza mahindi nje yasiwepo tuuze unga yaani ni mahindi yaliyoongezwa thamani.

Pamoja na hayo changamoto ni nyingi ikiwepo uchache wa vituo vya kununulia mahindi hayo hali inayosababisha mlundikano mkubwa wa magari na kulazimu magari kukaa wiki bila kushusha mzigo.

Wiki iliyopita Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Godfrey Zambi alisema serikali imepanga kununua jumla ya tani 200,000 bila kueleza umma kuwa hizo tani 200,000 ni kati ya tani ngapi zilizozalishwa na kwa kiasi hicho amewasaidiaje wakulima ambao kwa vyovyote wamezalisha zaidi kuliko uwezo wa serikali kununua.
 Hilo ni lundo la mahindi yaliyonunuliwa  kwa wiki moja

 Ustadi wa kazi unatukumbusha enzi za Shirika la Usagishaji la Taifa yaani NMC

 HUo ni upimaji unaoendelea hivi sasa

Mijadala inaendelea kwa madereva waliokaa hapo kwa zaidi ya wiki bila kushusha mahindi

Monday, September 1, 2014

Ugugaji kuku wa kienyeji

Posted by Unknown On 1:50 AM No comments
Ufugaji kuku na hasa wa kienyeji ndiyo njia pekee ya kumkomboa mwananchi vijijini kiuchumi. Serikali inapaswa kuhakikisha madawa ya mifugo na kinga au chanjo inayouzwa madukani iwe halisi na ya ukweli isiwe kama mwaka 2013 chanjo feki ilizagaa madukani matokeo yake wafugaji waliochanja mifugo yao ilikufa. Nani amefanya tahmini ya hasara iliyowafika wakulima hao? Nani anawalipa fidia ilihali mkulima ni kama mtoto yatima ambaye hapaswi kudeka?
 Ufugaji wa kuku ukienda sanjali na ukulima utanufaishana kwani kuku watapata mazao ya kilimo nalo shamba litarutubishwa na mbolea ya kuku.
Mzunguko huo wa mazao na mifugo mwaisho wa siku utakuwa na tija
 Hivi ndivyo tunavyofuga, hapa chini ni wenzetu wa Ethiopia wanafuga kisasa ambacho tuliowengi hatuwezi kutokana na gharama za mtaji zinazohitajika.
 Banda hili linatufaa kwa wale wenye maeneo ya kati yaani lenye ghorofa ili kuwa na nafasi kubwa ya kufugia ambapo unaweza kufuga huria hayo mabanda wakatumia kulala na kutagia.
 Kwa wale wa mijini unaweza weka banda kama hili uwani na ukafuga bila matata

KIlimo mseto

Posted by Unknown On 1:20 AM No comments
Kuna kila sababu ya wakulima kuangalia upya jinsi tunavyokitegemea kilimo na ni mazao gani tuzalishe. Tukiwa tunatafakari tufanyeje tujaribu kuwekeza katika kilimo cha mazao mbalimbali ambayo soko lake ni la uhakika zaidi.
 Tunapotembelea mashamba ya wenzetu katika utekelezaji wa kilimo kwanza kwa vitendo tujifunza kuwa kilimo mseto ndicho kitatusaidia. Tulime migomba, tufuge samaki, tufuge nyuki bila kusahau mkombozi wa maskini yaani ufugaji wa kuku wa kienyeji.
 KIlimo mseto kimesisitizwa katika mbio za mwenge 2014 kama hapo chini palivyo.
 Kilimo ni biashara kama hivi
 Huo ni ufugaji wa samaki

Tuesday, August 5, 2014

Wakulima kazi kwelikweli

Posted by Unknown On 12:36 PM No comments

Pamoja na jitihada zinazofanywa na mkulima mmoja mmoja za kuzalisha mazao ya kilimo chakula na biashara bado mazingira yake ni magumu analima bila kuwa na uhakika wa soko. Bei zenyewe zinapangwa na wanunuzi halafu sisi wa mjini tunalaumu ughali wa chakula kumbe ni wanunuzi wa kati ndiyo wanalangua mazao hayo. Serikali iandae vema mazingira ya kuwa na soko la uhakika kupitia mamlaka zake au hata vyama vya wakulima (vikundi). 
Ushirika uliotarajia kusaidia kutatua matatizo ya soko leo hii ushirika ni marehemu na bila kutafuta chombo mbadala hali itaendelea kuwa mbaya. Serikali itenge fedha za ununuzi wa mazao yote na kuelekeza nguvu kama sera inavyotamka.

Serikali ikishindwa kumtafutia mkulima soko la mazao yake itawalazimu kudai kwa nguvu kwani mkulima hana likizo yaani sawa na yatima kwani yatima hadeki.


Mambo yalivyokuwa katika uwanja wa nanenane wa John Mwakangale juu ni vifaranga wa Malawi chini ni mkulima wa Tunduru akiwa katika banda lake akionesha muhogo babu kubwa.

Hapo juu ni madumu ya asali ya nyuki wakubwa ba wadogo karibuni

Maonesho haya hayakuacha kuonesha kuku kama ndege wa kukupa kipato na anaweza kufugwa na kaya maskini.
Hao kuku ni aina ya Kenya wanaitwa Kenbro Dr Mbwaga wa Uyole ndiye mfugaji wa kuku hao

Nanenane 2014 Kilimo ni Biashara

Posted by Unknown On 12:09 PM No comments
Maonesho ya kilimo, mifugo na ujasiriamali ni fursa pekee inayoonesha hisia za watanzania kuhusu matarajio yao kulinganisha na fursa zilizopo.

Watunga sera wamekuwa wakiwayumbisha wakulima kwa kutoa sera zisizotekelezeka na porojo nyingi. Ilipobuniwa kaulimbiu ya Kilimo kwanza wengi walikuwa na tumaini ya kuushinda umaskini wakidhani serikali ingekuja na mikakati kabambe ya utekelezaji wa kilimo kwanza kwa vitendo kumbe sivyo ilivyotokea.

Maenesho ya nanenane jijini Mbeya yamefana licha ya kukumbana na changamoto kadha wa kadha zinazojitokeza. Tumaini la wakulima walio wengi walitarajia sera imara zingewekwa ili kuwa na fursa kwa vyombo vya fedha kuchangia moja kwa moja katika kilimo.

serikali ibuni mikakati ya kuwakopesha wakulima hawa wadogo wajishughulishe na ujasiriamali utakaohusisha usindikaji wa mazao yao na kuyauza vizuri.

Kati ya mambo yaliyochekesha mwaka huu ni pale serikali inapojitangaza na kujigamba kuwa itaiuzia shehena ya mahindi Kenya takriban tani 50000, Tujiulize kuwa fursa iliyokuwepo inapotea kwa kuuza ghafi bila kusindika na kuyaongezea thamani huo ni upwagu.


Hilo ndiyo banda la maonesho la jiji la Mbeya linasema Kilimo ni Biashara.

Hilo ni kati ya mabanda machache yaliyoandaliwa

Hiyo ni bustani ya jiko imewekwa hapo kama shamba darasa kwa mtu asiye na eneo unaweza kufanya hivyo

Monday, April 14, 2014

Alishikiliwa kwa masaa matatu, hakunywa maji japo alizamishwa kwa masaa hayo, maajabu hayo!





  “Mungu asiporuhusu kufa huwezi kufa hadi aruhusu yeye” ndivyo anavyoanza kusimulia kisa cha kusisimua na cha ajabu Erika Kajuanga (70) mwanamke aliyenusurika kuliwa na mamba baada ya kushikiliwa kwa masaa matatu chini ya maji.

Erika Kajuanga ni mkazi wa kijiji cha Bujonde wilayani Kyela mkoa wa Mbeya ambaye alifikwa na mkasa wa kukamatwa na mamba mnamo Novemba 27 mwaka 2012 majira ya saa moja asubuhi alipokuwa anafua nguo kando ya mto Kiwira.

“Nikiwa nafua nguo ghafla nilishikwa na mamba ambaye alinizamisha kwenye maji akikimbia toka pale aliponikamatia na kunipeleka ndani zaidi umbali ambao wenzagu tuliokuwa tunafua nao hawakuweza kubaini”anasimulia. 

Akiwa huko chini mamba alimwingiza kwenye pango chini ya maji akiwa tayari amemvunja mikono yote miwili na kumjeruhi goti na kumuacha kwa muda baadaye mamba huyo alirejea na kumtoa pale alipomuacha na kumwinua juu na kisha kumzamisha tena.

Mama huyo alikuwa akiomba Mungu amnusuru na hatari hiyo. Fahamu zilimjia akaingiza mdomoni mwa mamba nguo aliyokuwa ameshikilia mkononi licha ya mikono hiyo kuvunjwa aliweza kuishindilia vizuri kinywani mwa mamba huyo ndipo alipomwachia na kukimbia.

Akiwa chini ya pango kwenye maji mama huyo anashindwa kujua ilikuwaje hakudhuliwa na maji kwani hadi anatoka hakunywa hata kidogo na kwamba aliwezaje kupumua kwenye maji bado kwake ni kitendawili.
Baada ya kuachiwa hakuwa na uwezo wa kuogelea hivyo alijilaza chali akitumia miguu aliweza kufika eneo lenye jiwe kubwa akiwa hapo aliwaona watu waliokuwa wanajitahidi kumtafuta akapiga ukulele wa kuomba msaada ndipo walipofika wanaume wenye mikuki na kumwokoa.

Anasema ilifika hatua alikata tamaa ya kuokoka kwani alijua mamba yule angeweza kumrudia wakati wowote kabla hajapata msaada.

Alikimbizwa katika hospitali ya Kyela na kupatiwa msaada kisha kukimbizwa katika hospitali ya rufaa Mbeya ambapo hakuweza kupata matibabu yoyote kwasababu ya kutokuwa na fedha. Aliambiwa atoe shilingi laki tatu. Hata hivyo Kajuanga anadai kuwa yalitokea mabishano kati ya wahudumu wa hospitali hiyo waliodai kuwa bibi amepona kifo cha mamba na sasa mnamwacha afie hospitali kwa kukosa matibabu.

Kama ilivyo ada ya mja hunena mahali pande mbili zikivutana Mungu huinua upande mmoja kumtetea mja wake, walijitokeza ndugu na kumsaidia kumpeleka katika hospitali ya Peramiho iliyoko Songea mkoani Ruvuma baada ya kuwepo katika hospitali ya rufaa Mbeya kwa siku tatu bila matibabu. 

 Erika Kajuanga anawashukuru watu wa Mungu ambao walijitolea na kumsaidia kwenda katika hospitali ya Peramiho ambako anaendelea na matibabu hadi leo na kwamba hali yake inaendelea vizuri baada ya mikono iliyovunjwa kuungwa vizuri.

Tukio hili liliwashangaza wanakijiji wa Bujonde wakijiuliza bibi huyo aliwezaje kuwa mikononi mwa mamba kwa masaa matatu na baadaye kuachiwa; kweli Mungu mkubwa.

 Unaweza kuona makovu makubwa mikononi mwake hapa ni baada ya kutoka katika hospitali ya Peramiho

  

Site search

    More Text