Wednesday, June 25, 2008

UKATILI DHIDI YA WATOTO

Posted by Unknown On 1:13 AM No comments

Na Kenneth Mwazembe

Mbozi.

PAMOJA na jitihada zinazofanywa na serikali kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu, hali ni tofauti kwa Giveness Edward (19) mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Hangomba wilayani Mbozi mkoani Mbeya ambaye amekatishwa masomo na baba yake na kutakiwa aolewe.

Mkasa wa kusikitisha unaomhusu mtoto huyo ulianza mapema mwaka huu ambapo baba yake alitofautiana na binti yake huyo kutokana na imani ya Kikristo ya madhehebu ya Kimoravian ambapo baba mtu alimkataza kuabudu kwa madai kuwa imani hiyo imemfanya asimsikilize baba yake ambaye alimtaka kuolewa.

Giveness akizungumza na mwandishi wa habari hizi amesema kuwa baba yake Edward Kamgodi akishirikiana na kaka zake wawili Shida Edward na Mashaka Mwampashe walimpiga kwa mpini na kumsababishia maumivu ya miguu ambapo mtoto alilazimika kupata PF 3 ya polisi na kutibiwa katika zahanati ya Itaka.

Kipigo hicho kilimfanya Afisa Mtendaji wa kata ya Itaka Lukosomolo Ndimbwa kumshikilia kwa muda mzazi huyo asiye huruma na ambaye anathamini ng’ombe kuliko elimu hadi mtoto alipopona.

Hata hivyo Giveness anasema kuwa hatua ya serikali kushikilia baba yake kwa kosa hilo baba yake aliapa kumuua kisha naye kujiua, ndipo alipolazimika kukimbilia nyumbani kwa mwenyekiti wa kijiji Askofu Mbazu ambaye alimpokea na kumhifadhi na kuruhusu mtoto huyo kuendelea na masomo akitokea nyumbani kwa mwenyekiti huyo.

Hali ilibadilika usiku wa 27 Mei mwaka huu ambapo mwenyekiti alikula njama na mzazi wa Giveness ambapo usiku majira ya saa 9 baba huyo akiongozana na watoto wake wawili alifika na kubisha hodi ambapo mwenyekiti alifungua mlango na kusaidia kumfunga mtoto huyo mikono kwa kamba na kisha kuondoka naye hadi kijiji cha Wasa kwa mganga wa kienyeji aitwae Chilaka umbali wa kilometa 40 ili kumnywesha dawa za kuondoa imani ya kikristo na kumpandikiza uchawi.

Kwa nasibu Mungu alimnusuru binti huyo ambapo anaeleza kuwa mara baada ya kufika kwa mganga huyo walikaribishwa kula chakula ambapo yeye alizuiwa kula hadi atakaponyweshwa dawa hizo, hali iliyomfanya binti huyo kuomba aoneshwe msalani na kutumia mwanya huo kutoroka na kukimbia hadi kijiji cha pili ambako alipata msaada wa kuoneshwa njia ya kwenda mjini Vwawa ambako pia Wasamaria walimsaidia usafiri hadi Mbeya mjini.

Akisimulia zaidi binti huyo anabainisha sababu kubwa ya kuhitirafiana na baba yake kuwa ni pale alipokataa kupewa uchawi. “Nilipewa hirizi niliyokuwa navaa nikienda shuleni, hirizi hiyo ilikuwa na madhara kwa wanafunzi wenzangu, kwani siku nikivaa wanafunzi wengine walikuwa wanajisikia vibaya hali iliyowafanya wasielewe masomo hayo” alisimulia.

“ Nilivaa hirizi hiyo bila kuwa na amani moyoni na hasa pale nilipoona wanafunzi wenzangu wanahangaika ndipo nilipolazimika kumwendea mwalimu Kyomo ambaye alinishauri kuichoma moto hirizi hiyo ambayo hata baada ya kujaribu kuichoma haikuungua ndipo nilipoitupa chooni na hapo nikawa nimewasha moto na baba” anaongezea Giveness.

Mambo mengine anayosimulia binti huyo ni pale baba yake alipoongozana naye kwa mganga mmoja jirani yao ambapo alishuhudia ndege mkubwa jamii ya mwewe akitua mtini juu ya kilima na baadaye kuonekana binadamu mwenye mkoba aliyefika hapo huku akiwa na wasiwasi wa kuonwa alipokuwa akijigeuza kutoka umbile la ndege na kuwa binadamu na kisha kutoa hizo dawa zilizofanyiza hirizi hiyo.

Mtoto huyo ambaye hadi sasa anahifadhiwa na wasamaria amefikishwa katika kituo cha polisi mjini Vwawa ambao wamechukua hatua za kuwakamata watuhumiwa wote wanne ili kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili za unyanyasaji na kumzuia masomo.

Kaimu Afisa Elimu wilayani hapa Juma Kitabuge alieleza masikitiko yake kwa mkasa uliompata binti huyo na kueleza kuwa hali hiyo inaweza kumwathiri kimasomo, akaahidi kumsaidia kuhakikisha anaendelea kusoma katika shule jirani ambapo ataendelea kulelewa na wafadhili hadi atakapofanya mtihani miezi michache ijayo.

Jeshi la Polisi wilayani hapa limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba linaendelea na uchunguzi wa kisa hicho.

Mwisho

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text