Friday, February 6, 2009

Mchungaji Simon Kitwike aliyehukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kukataa kuapa mahakamani ameeleza kuwa haikuwa nia yake kukataa kuapa bali aliiomba mahakama atoe ushahidi bila kuapa.

Aliyasema hayo jana nyumbani kwake alipozungumza na Tanzania Daima mara baada ya kutoka gerezani ambako amefungwa kifungo cha nje, alielezea mkasa uliompata Oktoba 25 mwaka jana saa 6 za usiku alipovamiwa na kundi la majambazi lililovunja mlango wa nyumba yake na kuwaamuru kutoa fedha.

Kitwike alitaja mali zilizoibiwa kuwa ni pamoja na fedha taslim shilingi milioni 1,212,000, godoro moja, seti moja ya luninga, radio mbili, rewinder moja, masanduku mawili yaliyokuwa na nguo za mchungaji huyo na simu za mkononi mbili vyote jumla vikiwa na thamani ya shilingi milioni 2.2.

Baada ya majambazi hao kuondoka mchungaji alipiga kelele za kuomba msaada ambapo majirani walifika na kuanza msako ambao ulifanikiwa kuwanasa watuhumiwa watatu akiwemo mwanamke mmoja aliyekutwa na redio ambaye alipohojiwa alimtaja mumewe kuwa ndiye aliyempa redio hiyo, mtuhumiwa ambaye hadi hivi sasa hakamatwa pamoja na polisi kuarifiwa.

Kuhusu tukio la yeye kufungwa mahakamani Februari 4 mwaka huu, Kitwike amesema kuwa hakukataa kuapa kwa kusudi bali aliiomba mahakama imruhusu kutoa ushahidi wake bila kuapa kwa kutumia kifungu katika Biblia Mathayo 5:33-37 ambacho kinasema “Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa usiape uongo ila mtimizie Bwana nyapo zako lakini mimi nawaambia usiape kabisa hata kwa mbingu kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu”

Hakimu Nyasije Kajanja kabla hajatoa hukumu alimwamuru mchungaji huyo kusoma Waraka wa Warumi 13:1-2 kinachoeleza kuwa “Kila mtu na aitii mamlaka iliyokuu kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, na ile iliyopo imeamriwa na Mungu, hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu nao washindanao hujipatia hukumu”

Ndipo Hakimu huyo alimsomea kifungu cha sheria na 198 (1) kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 kinachokataza mtu kudharau Mahakama na kuwa kuendelea kukataa kuapa ni kuvunja sheria na hivyo anatenda kosa la jinai.

Ndipo hakimu alipomhukumu kwenda jela miezi sita kwani sheria inasema asiyeapa ametenda kosa la kudharau mahakama ambalo adhabu yake ni kifungo cha miezi 12 jela, hata hivyo kufuatia utetezi alioutoa mahakamani hapo hakimu aliamua kumfunga kifungo cha miezi sita gerezani.

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text