Wednesday, February 18, 2009

Mchungaji Cosmas Mwasenga (48) aliyekamatwa na viungo vya binadamu anayedaiwa kuwa albino siyo mchungaji kitaaluma, imefahamika.

Kukamatwa kwa mchungaji huyo na ambaye alidaiwa kuwa ni kanisa la Pentekoste kumewastusha wakuu wa madhehebu hayo ambao walidai kuwa hawana mchungaji wa jina hilo.

Askofu wa kanisa la Muungano wa Makanisa ya Kipentekoste wilayani Mbozi Erasto Makalla akizungumza na gazeti hili amesema kuwa, mtu huyo kabla hajabadili tabia alikuwa ni muumini wa kawaida wa madhehebu hayo ya Pentecoste Holiness Mission (PHM), na kuwa alikuwa akiwahubiria watu waokoke wamjue Yesu.

“Tumefuatilia kujua mchungaji aliyehusika na tukio hilo na tumeambiwa sio mchungaji kama ilivyoelezwa, ila kutokana na uwezo wake wa kuwashuhudia watu ili wapate wokovu, walimpa jina la Mchungaji, lakini yeye siyo mchungaji bali kazi yake ni mhunzi” alisema Askofu Makalla.

Makala aliongeza kuwa Umoja wa makanisa hayo unaendelea kufuatilia ili kujua habari zaidi za mtu huyo (anayedaiwa kuwa mchungaji), baada ya hapo watatoa taarifa rasmi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nambala Jumanne Mziho aliyewaongoza askari kupekua nyumba ya Luseshelo Mwashilindi alisema kuwa Februari 13 saa 11 za jioni Polisi walifika kilabuni na kumtaka awaongoze nyumbani kwa Mwashilindi.

Polisi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Inspekta Ndimbo akiongozana na E.276 D/Sgt Datstan na F. 679 D/Sgt Daniel wakiwa na watuhumiwa Cosmas Mwasenga na Luseshelo Mwashilindi walifanya upekuzi na kukuta Mifupa miwili inayosadikika kuwa ya binadamu, na chupa 18 za dawa aina ya Benzyl Penicillin na maji ya kuyeyushia dawa hiyo chupa 14, na koti jeusi la Mchungaji, vitu ambavyo vilikutwa bafuni kwa Luseshelo.

Mziho aliendelea kueleza kuwa baada ya polisi kuona mifupa hiyo waliwahoji watuhumiwa kueleza juu ya mifupa hiyo ambapo Mwashilindi alisema ni mifupa ya mzungu hali Mwasenga akisema ni ya Albino.

Imeelezwa kuwa siku mbili kabla ya tukio watuhumiwa hao walikwenda Mbeya katika maeneo ya Mwanjelwa wakitafuta mteja wa kununua mifupa ya kunguru mweupe, jambo ambalo lilifanya wasamaria wema kutoa taarifa Polisi ambao waliweka mtego ambao ulipelekea kukamatwa kwa watu hao.

Afisa Tarafa wa Tarafa ya Iyula Nathian Mpandachombo alipoulizwa kama kuna tukio lolote la kifo cha albino katika eneo lake alithibitisha kuwa hakuna mtu yeyote wa aina hiyo aliyepotea kwani idadi ya walemavu wa ngozi waliopo katika tarafa yake wote wapo.

Tuki linalofanana na hilo liliwahi kutokea katika kijiji cha Mpanda kata ya Nyimbili ambapo mwananchi mmoja ilidaiwa alifukua kaburi alilokuwa amezikwa albino ambaye alikuwa nduguye wa familia moja kisha kukimbilia wilayani Chunya ambako kuna machimbo ya dhahabu, lakini baadaye Polisi walidai kuwa kaburi hilo lilikuwa limefukilwa nusu tu na kwamba walithibitisha kuwepo kwa mifupa hiyo.
MWISHO.

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text