Monday, March 8, 2010

Jinsi Camartec ilivyo jizatiti kuokoa misitu kwa kusambaza teknolojia ya matumizi ya gesi itokanayo na wanyama
• CARMARTEC yatua Mbozi

• Yaja na aina mpya ya mtambo wa gesi uitwao CAMARTEC MODIFIED DESIGN

• Vijana kunufaika na ujenzi

• Wateja kujengewa kwa 2/3 ya bei



Wananchi wilayani Mbozi mkoani Mbeya wameshauriwa kuanza ufugaji wa kisasa ambao kwa kutumia teknolojia ya gesi ya wanyama utapunguza ukataji miti na kuiokoa nchi kwa janga la ukame.



Wito huo umetolewa na kaimu Mkurugenzi Mtendaji wilaya ya Mbozi Afwilile Lamsi alipofungua mafunzo ya siku 10 yanayotolewa na kituo cha zana za kilimo na teknolojia vijijini (CAMARTEC) kwa mafundi waashi ya namna ya kujenga mitambo ya gesi.



Lamsi aliongeza kuwa wilaya ya Mbozi kwa hivi sasa ina watu zaidi ya 600,000 ambao wanahitaji kubadilisha ufugaji kutoka ule wa kuchunga mbugani na kulishia ndani hali itakayofanya upatikanaji wa nishati ya gesi kuwa rahisi na hivyo kuokoa mazingira.



Awali Afisa Mkuu wa Mafunzo wa CAMARTEC Harold Ngowi akimkaribisha mkurugenzi kufungua mafunzo alisema kuwa kituo chake kinatoa mafunzo hayo na kuendesha mradi wa gesi kwa hisani ya shirika la maendeleo la Uholanzi (SNV) likiwa mshiriki mkuu.



Ngowi aliongeza kuwa lengo ni kujenga mitambo mitambo 12,000 katika miaka 5 ya mradi ambao ulianza Novemba 2008 na ambao hadi sasa umejenga mitambo 165 na kufundisha mafundi 180 katika mikoa ya Tanga, Arusha, Iringa, Kilimanjaro, Manyara na Pwani.



Aidha Ngowi alifafanua kuwa CAMARTEC wamebuni aina mpya ya mtambo ambao ni bora zaidi ya ule wa awali uliojulikana kama CAMARTEC FIXED DOME kwa kuanza aina mpya iitwayo Modified CAMARTEC Design ambao umeelezwa kuwa ujenzi wake ni rahisi zaidi.





Kutokana na mtambo huo mpya nchi kadhaa zikiwemo Uganda, Ethiopia, Kenya na Ruanda wanakuja Tanzania kujifunza kwa kuwa ni nchi yenye uzoefu na mitambo ya biogas.



Hata hivyo mkakati huo ulianzishwa na serikali ya Uholanzi iliyoitisha mkutano mkubwa wa wadau wa technolojia ya biogas wa nchi za Afrika jijini Nairobi nchini Kenya mwaka 2007 ambao ulihudhuriwa na nchi nyingi.



Ni kutokana na mkutano huo wizara ya nishati na madini ikaitikia na kukabidhi mradi huo kwa CAMARTEC ili kuusimamia na kuuendesha kwa kusambaza teknolojia hiyo vijijini.



Mradi wa Biogas Tanzania umelenga kaya vijijini ili kuwanusuru wanawake na adha ya utafutaji kuni pamoja na kuhifadhi mazingira kwa kuinusuru miti inayokatwa kwa ajili ya nishati ya kuni na mkaa.


Wateja watakaokuwa tayari kujengewa mitambo hiyo watalipiwa gharama za ujenzi huku wakichangia kiasi kidogo cha pesa kwa ajili ya vifaa kama saruji, mabomba, taa na majiko ya gesi.


Mafunzo hayo yanatolewa huku idadi kubwa ya mafundi wanafunzi wakiwa ni wanawake ambao ni 14 na wanaume 11 ishara ya kutambua umuhimu wa teknolojia hiyo kwa wanawake. Ujenzi huo utawafanya akina mama kufanya kazi nyingine zaidi kuliko kwenda misituni kutafuta kuni

1 comment:

  1. Ni wazi teknolojia hii ni nzuri na itakua na manufaa sana kwa jamii. Ila sijui mtu akihitaji kuipata aende wapi na amuone nani?

    ReplyDelete

Thank you for reading the article

Site search

    More Text