Wednesday, November 12, 2014





Wadaiwa shilingi 50,000 kwa ajili ya maabara za shule ndipo maombi yafikiriwe


Serikali inahusika na kuwacheleweshea wakulima pembejeo, kutokana na kushindwa kukamilisha mikataba na wadau wa kilimo kwa wakati.

Hayo yalielezwa jana na afisa kilimo wa mkoa wa Mbeya Enock Nyasebwa alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Alitoa kauli hiyo kufuatia malalamiko ya wakulima wa wilaya za Mbozi na Momba ambao kupitia vikundi vyao waliomba serikali mapema mwaka huu kuwakopesha pembejeo za kilimo cha mahindi.

Maombi hayo ya mikopo ya pembejeo yametokana na serikali kubadili mfumo wa kutoa pembejeo kwa njia ya ruzuku ambao ulishindikana na kubuni mpango mpya ambao wakulima kupitia vikundi vyao wanaomba mkopo kupitia idara ya kilimo na benki na serikali kutoa mkopo huu ukiwa umechangiwa na wakulima kwa asilimia 20 na riba ya mkopo kulipwa na serikali.

Hata hivyo serikali imeonekana kusuasua katika kutekeleza mpango huo hali iliyowasababishia wakulima kupata pembejeo kwa wakati muafaka.

Akizungumza na gazeti hili mwenyekiti wa chama cha wakulima wa Momba Sadiki Simaya alisema kuwa serikali iliahidi kutoa pembejeo kabla ya msimu wa kilimo kuanza lakini mpaka sasa mvua zimeanza na hakuna lolote katika utekelezaji wa mpago huo.

Simaye aliongeza kuwa kutokana na hali hii wana wasiwasi kuwa huenda wakashindwa kupanda mahindi kwa wakati na hivyo kupata hasara na kuongezeka kwa gharama kwani mashamba yaliyolimwa yameanza kuota nyasi na hivyo kuwalazimu kulima tena waliwa wanasubiri pembejeo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Halungu Charles Simkoko ameeleza kusikitishwa na mipango ya serikali ya kuwatoza vikundi vya wakulima mchango wa shilingi 50,000 kwa ajili ya ujenzi wa maabara kama sharti la kupata mikopo hiyo ya pembejeo.

Mkulima mwingine kutoka Tunduma Economic Group Dr Samson Kibona alilalamikia utaratibu huo kuwa unaweza kuwaathiri wasipate mazao ya kutosha msimu huu iwapo watachelewa kupanda mazao yao kwa wakati kwani mvua za kwanza ni za kupandia.

Akifafanua zaidi Kibona alisema kuwa mpaka sasa wameshindwa kuuza mahindi ya mwaka huu kwa kukosa soko hali inayowafanya washindwe kufanya chochote zaidi ya kungojea mikopo hiyo.

Hata hivyo afisa kilimo huyo wa mkoa alitetea ucheleweshaji huo kuwa serikali inafanya mazungumzo na wadau wa kilimo yakiwemo mabenki na makampuni ya ununuzi wa mazao na kuhakikisha kuwa wakulima wanaingia mikataba kwa kutoa asilimia 20 ambapo serikali itatoa asilimia 20 na mabenki kutoa asilimia 60 ya mkopo huo “tunaamini kuwa wakulima watapata pembejeo mapema mara baada ya kukamilisha mikataba hiyo” alisisitiza.

Naye afisa kilimo wilaya ya Mbozi alipohojiwa juu ya kuweka masharti ya kuchangia 50,000 kwa vikundi vinavyoomba mkopo alisema sisi tunawaomba tu hatuwalazimishi kauli inayopingwa na viongozi wa vikundi.

Mwisho

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text