Monday, April 20, 2009

MZEE CHILO AKIWA JIJINI MBEYA


Mzee Chilo akiwa jijini Mbeya akipika filamu mpya matata na tishio ambayo itakuwa madukani hivi karibuni.

Mzee Chilo alivuma sana katika mchezo maarufu wa Jumba la Dhahabu

VIONGOZI WA MAALBINO MBOZI




Maalbino (viongozi) wamelivalia njuga suala la mwenzao aliyetishiwa wiki mbili na mtuhumiwa ambaye hadi sasa yuko uraiani.


Sydney Mwamlima ambaye ni katibu wa Chama cha Maalbino amedhamiria kulifikisha suala hilo kwa mkuu wa polisi mkoani hapa ili kuona anatakeleza maagizo ya serikali kuwalinda.


JESHI LA POLISI NA ALBINO



Wadau hapo juu ni mkuu wa kituo cha polisi mjini Tunduma Ally Wendo akimtaka albino Judith Silwimba kumpa maelezo ya kina juu ya uwepo wa mtuhumiwa aliyemtishia kumuua hapo kijijini Chipaka.


mazungumzo hayo yalizua ubishi kati ya mume wa mlemavu huyo na polisi akidai kuwa ameshakwenda polisi zaidi ya mara tatu lakini hawajamsikiliza na kwamba mtuhumiwa bado yuko huru mitaani.


hapo polisi kazi kwenu

Saturday, April 18, 2009

HOFU KWA MAALBINO

Wadau ni muda mrefu sikuwepo hewani tuungane tena.

Judith Msongole mlemavu wa ngozi (Albino) wa kijiji cha Chipaka wilayani Mbozi anaishi kwa hofu ya kuuliwa! jamani hapo sasa ni mambo!

Jamani uungwana uko wapi? Maisha ya albino yanapokuwa hatarini na hasa watu wanapojitokeza kuwatisha wazi wazi wakiwa na nia ya kuwadhuru na kupata viungo vyao. Sasa mama huyo anaishi kwa hofu, polisi nao wamechelewa kuchukua hatua za kumkamata mtuhumiwa sasa mabishano ni kati ya polisi na mume wa mlalamikaji.

Mkuu wa kituo anadai mlalamikaji hajaenda kumwona ilihali mume wa mlalamikaji anadai kwenda zaidi ya mara tatu polisi lakini wanajibiwa visivyo.

Viongozi chukueni hatua za kukomesha mauaji hayo.

Jakaya Kikwete chukua hatua zile alizochukua Mwalimu Nyerere kukomesha mauaji yaliyokuwa yanatokea Tukuyu hasa Ikuti kwa imani za kishirikina miaka ya sabini. Mbinu ile itasaidia, wachawi wote maarufu kama Manyafu walipitiwa na operesheni ile ambayo iliwahamishia Mafia na kuwekewa stop wasirudi mkoani Mbeya.

Hatuwezi kukuelekeza, bado unao maafisa walioshiriki operesheni ile tafadhali uwatumie japo kwa kiasi. Tuone waganga hao wakifanyia uganga huko uhamishoni ikiwezekana ni kuwakusanya pote walipo.
Pamoja na agizo la Waziri Mkuu Mh. Pinda kufuta leseni za waganga wa jadi bado waganga wanaendelea kutoa huduma kwa wateja huku wakiweka mabango yao barabarani hadharani.

Shiriki hapo ulipo kutokomeza mauaji ya albino.

Saturday, February 28, 2009

VIJANA WENYE HASIRA WAIPIGA MAWE NYUMBA YA MWENYEKITI WA HALMASHAURI

Na Kenneth Mwazembe
Tunduma

Kundi la vijana wenye hasira kali zilizochochewa na mkuu wa kituo cha polisi mjini Tunduma A.S. Wendo wamevamia nyumba ya diwani wa kata ya Tunduma na ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Aden Mwakyonde na kuvunja vioo 83 vya madirisha 14 na kuwajeruhi mgambo wanne.

Chanzo cha ghasia hizo ni kukamatwa kwa baiskeli za vijana hao zilizokuwa zikitumika kuvusha mahindi na mchele mpakani mwa Tanzania na Zambia kwa madai kuwa ni operesheni usafi wa mji.

Vijana hao wamesema kuwa polisi walianza ukamataji wa baiskeli hizo usiku wa Februari 26 na kuendelea 27 ambapo vijana hao wamedai kuwa wamedaiwa fedha (RUSHWA) ili kukomboa baiskeli hizo.

Katika kukabiliana na kitendo hicho ambacho wamekiita unyanyasaji unaofanywa na jeshi hilo vijana hao waliandamana kuelekea kituo cha polisi ili kuishinikiza polisi kuwarejeshea baiskeli zao ambapo mkuu wa kituo aliwaambia waende kuchukua baiskeli hizo kwa diwani wao.

Kauli hiyo ndiyo iliyowafanya wao kurusha mawe kituoni hapo na baadaye kwenda nyumbani kwa diwani wao na kuharibu madirisha yote na kuipiga mawe nyumba hiyo.

Akizungumza na gazeti hili Aden Mwakyonde alieleza kuwa alipigiwa simu na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi shirikishi ya mjini hapa kuwa kuna maandamano makubwa ya vijana wenye hasira wakienda nyumbani kwake hali iliyomfanya awapigie askari polisi.

“Nimepiga simu kwa OCS ili atume askari kuzuia madhara ambayo yangeweza kutokea lakini hakufanya hivyo, alidai hana gari, mke wangu amempelekea magari mawili akadai hawawezi kutumia salon wanataka gari la wazi hata alipopelekewa gari la wazi akasema ni chakavu kasha akaondoka kwenda mjini Vwawa” alilalama Mwakyonde.

“Nimewaomba polisi wawape vijana hao baiskeli zao ili kuepusha shari ambayo ingeweza kutokea lakini polisi hawakufanya hivyo na hivyo kunisababishia hasara hii ”aliongeza Mwakyonde akielekeza lawama zote kwa jeshi la polisi.

Mwenyekiti huyo aliyekua akihudhuria kikao cha kamati ya uchumi na mipango alilazimika kuacha kikao na kukimbilia nyumbani kwake akiwabeba mkuu wa polisi wilayani hapa Stephen Mtengeth na timu yake lakini alipofika na kuona nyumba imeharibiwa aliwajia juu na kuwafukuza OCD na timu yake ya watu wane.

Hatua hiyo na ambayo imewaudhi polisi hao imelalamikiwa vikali kutolewa na kiongozi kama yeye wakidai angetumia busara.

Mkuu wa kituo cha polisi cha Tunduma aliyejitaja kwa jina moja la A. S. Wendo alipohojiwa juu ya yeye kuwa chanzo cha ghasia hizo alikanusha na kudai kuwa yeye amewatuliza wakakataa na hivyo kumfanya aende wilayani kuomba msaada wa askari wengine.

“Niliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kukinusuru kituo baada ya vijana hao kutaka kukivamia” anaongeza Wendo.

Mamlaka ya mji mdogo wa Tunduma inafanya operesheni ya kusafisha mji kwa kuondoa uchafu katika mifereji na vibanda vya wafanyabiashara ndogondogo ambayo ilianza juzi ikahamia na kukamata baiskeli hali iliyozusha machafuko yaliyosababisha wanamgambo wa halmashauri wane kujeruhiwa na mmoja kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbozi mjini Vwawa.

Mgambo waliojeruhiwa ni John Mwakalinga ambaye amelazwa katika hospitali ya Vwawa na Andrew Sing’ambi aliyetibiwa na kuondoka na wengine wawili ambao hawakuweza kupatikana majina yao .

Muuguzi katika wodi la majeruhi Ester Nyondo ameeleza kuwa hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri.

Hili ni tukio la tatu tangu mwaka 2006 ambapo ghasia za mpakani zilizuka kufuatia kifo cha Lukas Msuya kuuawa katika mahabusu za Zambia lile la mgomo wa mawakala wa usafirishaji (Clearing & Forwarding) ambapo katika ghasia hizo kulitokea uharibifu wa mali na majeruhi.

Mkuu wa wilaya ya Mbozi Halima Kihemba alipohojiwa juu ya matukio hayo alikiri kupewa taarifa muda mchache uliopita na kwamba kwa wakati huo alikuwa safarini Tukuyu kwenye kikao.

Wednesday, February 18, 2009

MCHUNGAJI FEKI AKAMATWA NA MIFUPA YA ALBINO

Mchungaji Cosmas Mwasenga (48) aliyekamatwa na viungo vya binadamu anayedaiwa kuwa albino siyo mchungaji kitaaluma, imefahamika.

Kukamatwa kwa mchungaji huyo na ambaye alidaiwa kuwa ni kanisa la Pentekoste kumewastusha wakuu wa madhehebu hayo ambao walidai kuwa hawana mchungaji wa jina hilo.

Askofu wa kanisa la Muungano wa Makanisa ya Kipentekoste wilayani Mbozi Erasto Makalla akizungumza na gazeti hili amesema kuwa, mtu huyo kabla hajabadili tabia alikuwa ni muumini wa kawaida wa madhehebu hayo ya Pentecoste Holiness Mission (PHM), na kuwa alikuwa akiwahubiria watu waokoke wamjue Yesu.

“Tumefuatilia kujua mchungaji aliyehusika na tukio hilo na tumeambiwa sio mchungaji kama ilivyoelezwa, ila kutokana na uwezo wake wa kuwashuhudia watu ili wapate wokovu, walimpa jina la Mchungaji, lakini yeye siyo mchungaji bali kazi yake ni mhunzi” alisema Askofu Makalla.

Makala aliongeza kuwa Umoja wa makanisa hayo unaendelea kufuatilia ili kujua habari zaidi za mtu huyo (anayedaiwa kuwa mchungaji), baada ya hapo watatoa taarifa rasmi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nambala Jumanne Mziho aliyewaongoza askari kupekua nyumba ya Luseshelo Mwashilindi alisema kuwa Februari 13 saa 11 za jioni Polisi walifika kilabuni na kumtaka awaongoze nyumbani kwa Mwashilindi.

Polisi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Inspekta Ndimbo akiongozana na E.276 D/Sgt Datstan na F. 679 D/Sgt Daniel wakiwa na watuhumiwa Cosmas Mwasenga na Luseshelo Mwashilindi walifanya upekuzi na kukuta Mifupa miwili inayosadikika kuwa ya binadamu, na chupa 18 za dawa aina ya Benzyl Penicillin na maji ya kuyeyushia dawa hiyo chupa 14, na koti jeusi la Mchungaji, vitu ambavyo vilikutwa bafuni kwa Luseshelo.

Mziho aliendelea kueleza kuwa baada ya polisi kuona mifupa hiyo waliwahoji watuhumiwa kueleza juu ya mifupa hiyo ambapo Mwashilindi alisema ni mifupa ya mzungu hali Mwasenga akisema ni ya Albino.

Imeelezwa kuwa siku mbili kabla ya tukio watuhumiwa hao walikwenda Mbeya katika maeneo ya Mwanjelwa wakitafuta mteja wa kununua mifupa ya kunguru mweupe, jambo ambalo lilifanya wasamaria wema kutoa taarifa Polisi ambao waliweka mtego ambao ulipelekea kukamatwa kwa watu hao.

Afisa Tarafa wa Tarafa ya Iyula Nathian Mpandachombo alipoulizwa kama kuna tukio lolote la kifo cha albino katika eneo lake alithibitisha kuwa hakuna mtu yeyote wa aina hiyo aliyepotea kwani idadi ya walemavu wa ngozi waliopo katika tarafa yake wote wapo.

Tuki linalofanana na hilo liliwahi kutokea katika kijiji cha Mpanda kata ya Nyimbili ambapo mwananchi mmoja ilidaiwa alifukua kaburi alilokuwa amezikwa albino ambaye alikuwa nduguye wa familia moja kisha kukimbilia wilayani Chunya ambako kuna machimbo ya dhahabu, lakini baadaye Polisi walidai kuwa kaburi hilo lilikuwa limefukilwa nusu tu na kwamba walithibitisha kuwepo kwa mifupa hiyo.
MWISHO.

WALIOMPIGA IMAMU WAPANDA KIZIMBANI

Na Kenneth Mwazembe
Mbozi

Watu wawili wamefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Mbozi kwa tuhuma za kumpiga Imamu wa msikiti wa Ijumaa mjini Tunduma Husein Issa Baluza (32) akiwa anaswalisha sala ya alasiri.

Watuhumiwa hao ndugu, wametajwa kuwa ni,Thabit Ismail 37 mkazi wa mji mdogo wa Tunduma na Nasoro Ismail (28) mwanafunzi wa chuo kikuu kishiriki cha Muhimbili .

Ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa polisi Cyprian Michiria kuwa manamo tarehe 16 Februari mwaka huu kwa pamoja watuhumiwa hao walimshambulia kwa kumnyoshea vidole na kumjeruhi usoni na kumchania shati lake lenye thamani ya shilingi 10,000.

Washitakiwa wote wawili wamekana shitaka mbele ya hakimu Enock Matembele na kesi imeahirishwa hadi tarehe 18 Machi ambapo itatajwa tena na washitakiwa wako nje kwa dhamana ya shilingi laki tano kila mmoja.

Wakati huo huo jeshi la polisi wilayani hapa limeimarisha ulinzi katika msikiti huo baada ya kugundua kuwa waumini wa msikiti huo wamegawanyika makundi mawili la kwanza likimshabikia imamu Husein Issa anayeungwa mkono na Bakwata na lingine likimuunga mkono mwalimu wa madrasa Ahmed Pongwa.