Thursday, December 26, 2013

Kilimo kinahitaji mikakati zaidi

Posted by Unknown On 11:08 AM No comments


Kilimo kama uti wa mgongo wa taifa hili umekuwa ni wimbo mtamu vinywani mwetu tangu Azimio la Iringa la Siasa ni kilimo likisheheni kauli mbiu kadha wa kadha ambazo zimedumu kwa takribani miongo minne.

Serikali katika awamu zake tatu zilizotangulia ilijitahidi kuhamasisha kilimo kwa kuwaandaa wataalam na kutumia wanasiasa katika majukwaa yao kuhimiza kilimo ambacho mpaka hivi sasa hakijawa na mafanikio ya kuridhisha na hii ni kwa sababu ya kuwa na maneno mengi kuliko vitendo yaani hatukuwa serious.

Azimio hilo lilipokelewa kwa furaha na wananchi/wakulima wengi nchini na hasa wa hapa Mbozi ambao walilipokea na kwenda nalo sanjali na operation vijiji ambapo mashamba ya ujamaa yalianzishwa, vijiji vikasajiliwa chini ya sheria ya vijiji, mabwana shamba wakasambazwa vijijini, mipango maalum ya kuboresha mazao ya biashara ikaanzishwa na mafanikio yalianza kunukia kabla ya kuharibiwa na mipangilio ya serikali au uongozi bora.

Nasema mwelekeo uliyumba kwa kukosa uongozi bora kwani vyama vya ushirika vilivyoanzishwa hata kabla ya uhuru vilivurugwa na badala yake zikaanzishwa mamlaka za mazao kama Mamlaka ya pamba, ya Pareto na ile ya kahawa na tumbako nazo zilishindwa, zikavunjwa zikaanzishwa Bodi za mazao hayohayo kwa upande wa mazao ya chakula likawepo shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), mazao mengine ikawepo GAPEX yote hayo imebaki kuwa historia.

Rais wa awamu ya kwanza hayati J.K.Nyerere enzi za uhai wake alisema ili nchi iwe na maendeleo tunahitaji vitu vinne, yaani ardhi, watu, uongozi bora na siasa safi (Ujamaa uk 27). Sasa hapo sijui tulikosa nini kati ya uongozi bora na siasa safi kwani ardhi ilikuwepo ya kutosha, na watu walikuwepo wa kutosha.

Wahimizaji hawa aidha wenyewe hawakijui kilimo au wanafanya kazi kwa kuwa wameajiriwa kufanya hivyo ili mradi waonekane wamesema na kwamba serikali inawalipa mishahara kwa kazi hiyo.

Pamoja na ukweli kwamba ardhi inawaajiri asilimia 80 ya watanzania, bado ajira hii haina tija, mkulima hajaweza kufaidi matunda ya kilimo ili kujiletea maendeleo.

Awamu ya nne ya Mheshimiwa JK imeanza vizuri kwa kuainisha matatizo mbalimbali yanayoikumba sekta ya kilimo na mifugo na migongano ambayo imekuwa ikitokea sehemu mbalimbali baina ya wakulima na wafugaji.

Kuna matatizo yanayotokea yaliyo nje ya uwezo wetu kama ukame, mafuriko n.k , kwa hayo tunamwachia Mungu, lakini kuna matatizo yanayosababishwa aidha na mipangilio mibaya ya serikali au watu wachache wenye nyadhifa zao na wenye dhima ya kuinua kilimo nchini.

Hapa ndipo penye matatizo yote ambayo kwa mimi mkulima nitaishia kulaumu serikali kwani kila baya linapotokea tunasingizia serikali hata kama yupo mtu anayestahili kuwajibika kwa uzembe na pengine ni hujuma tu.

Umefika wakati wa Watanzania kuufichua udhalimu na uhujumu wa baadhi ya watumishi serikalini walioamua kurudisha maendeleo nyuma kwa makusudi na kukebehi dhana nzima ya serikali ya awamu ya nne ya kumpatia maendeleo na maisha bora kila Mtanzania.

Katika kuhakikisha kuwa kilimo ambacho ni uti wa mgongo kinazaa matunda wakulima wamejiandaa kuzalisha zaidi na hasa baada ya bei ya mahindi, mpunga na maharage kupanda katika msimu uliopita ambapo mahindi kwa hapa Mbozi yaliuzwa kwa shilingi 60,000 kwa gunia la kilo 100, mpunga 75,000 kwa gunia la kilo 60 na maharage 90,000 kwa gunia la kilo 100 .

Wakulima walitegemea ahadi ya serikali ya kuwauzia pembejeo na hasa mbolea kwa bei ya ruzuku ambayo kwa hapa Mbozi imezua kizazaa na malalamiko mengi kwa zoezi zima la ugawaji mbolea lilivyoendeshwa na hasa pale walipoletewa mbolea za kukuzia badala ya zile za kupandia ili hali majira ya mbolea hizo ni miezi ya Januari na Februari .

Tukimtafuta mchawi tunaambiwa wizara ya kilimo ndiyo iliyopanga kuleta mbolea za kukuzia wakati wa kupandia, sisi kama wakulima tunaamua kupanda bila mbolea tukijua kwa makusudi kabisa kuwa kupanda bila mbolea ni kuvunja kanuni za kilimo bora na hivyo kwenda kinyume na Azimio la Iringa la Siasa ni kilimo.

Mfano mzuri ni msimu wa 2007/8 ugawaji wa pembejeo ulikuwa wa vituko na kuonesha kuwa hujuma zilijulikana na wahusika wenye dhamana ya kilimo. Makampuni yenye uzoefu wa kuuza na kusambaza mbolea kwa miaka mingi yalipewa mgawo mdogo sana wa kuuza hizo mbolea mfano mzuri ni kampuni ya mbolea Tanzania (TFC) wakapendelewa makampuni ya binafsi, mfano TFC iliruhusiwa kuuza tani 650, Export Traders tani 2497, Premium tani 205, STACCO tani 1077, Chapameli tani 1500, Nyiombo tani 154 na kufanya jumla ya tani 6084 kwa wilaya badala ya mahitaji ya jumla ya tani 28,000.  

Msimu 2012/13 mbolea za kupandia zililetwa wilayani hapa mwezi Februari badala ya Oktoba je hao wakubwa wanadhamira gani na kilimo? Aibu tupu!

Kama dhamira ni kuinua kilimo kwa faida ya taifa zima kuna haja sasa Mheshimiwa Rais kuangalia muundo wa baadhi ya vyombo husika vilivyotarajiwa kufanikisha zoezi zima la kusambaza pembejeo na hasa wizara ya kilimo.  

Wizara ya kilimo kupitia Mfuko wa Pembejeo inatoa mikopo kwa ajili ya kuinua na kuboresha kilimo, kwa mujibu wa kipeperushi cha Mfuko huo, Mfuko unatoa mikopo ya pembejeo za kilimo na mifugo, mikopo ya ununuzi wa matrekta mapya, mikopo ya kukarabati matrekta na mikopo ya kuanzisha vituo vya kukodisha matrekta (Farm Service Centres)

Inawezekana kabisa kuwa Mfuko wa Pembejeo haujawezeshwa kiasi cha kutosha kulingana na mahitaji yalivyo hivi sasa kwani awamu hii ya nne imedhamiria kuinua kilimo na hivyo kila kona inahitajika kwenda kwa kasi mpya na nguvu mpya bila hiyo mikopo wakulima wetu wataishia jembe la Adamu na Hawa.

Kazi kubwa inayofanywa na Mfuko wa Pembejeo wa Taifa (AGITF) inahitaji kuungwa mkono na kuwekwa jukwaani ili taasisi nyingine ziige. Mfuko huo chini ya Mkurugenzi wake Mariam Nkumbi licha ya kuwa na watumishi wachache, wanajitahidi kuzunguka katika mikoa yote na kujua mahitaji ya wakulima, kutoa mikopo na ufuatiliaji wa marejesho.

Serikali inapaswa kuongeza fedha kwenye mfuko huu sanjali na maandalizi ya kuanzisha benki ya kilimo. Mfuko huu umesimama badala ya benki kwa muda mrefu na umekuwa ukitoa mikopo kwa kuzikubali hatimiliki za kimila ambazo zinaenda sambamba na mipango ya serikali ya Mkukuta na Mkurabita.

Mfuko huu ungeweza kuwasimamia mawakala katika suala zima la uagizaji na usambazaji wa pembejeo kwa ushirikiano na mashirika mengine kama AGRA n.k.

Mapinduzi ya kilimo ni lazima, yalenge kuongeza maeneo ya uzalishaji kutoka hapa tulipo , mkulima wa jembe la mkono awezeshwe afikie zana za kukokotwa na wanyama, na yule anayetumia wanyama kazi apewe trekta kulingana na uwezo wake.

Pembejeo zifike vijijini aliko mkulima kwa utaratibu mzuri na kwa wakati stahili na si kama hivi sasa mkulima anahitaji mbolea za kupandia anapelekewa za kukuzia na atakapohitaji za kukuzia atapelekewa za kupandia hicho ni kichekesho.

Kwa bei hizi hata ungelikuwa ni wewe kwa vyovyote ungelikata tamaa na kuamua kuzalisha chakula cha kuganga njaa tu na si cha kibiashara na kujiongezea kipato.

Mwanzoni mwa Disemba hii 2013 nilimsikia ndugu David Mwaibula akielezea mipango ya kilimo na uwekezaji katika kipindi cha Baragumu kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Channel Ten kuwa ni lazima kiende kwa wakati. Alifafanua kilimo enzi za mkoloni kuwa alihimiza mazao hayo na kuweka soko la uhakika kwani walaji walikuwa wengi na mahitaji ya dunia yalikuwa makubwa. Alitoa mfano wa zao la mkonge ambalo lilitoa katani zilizo tumika kutengeneza kamba. Meli zote zilitumia kamba za nanga za mkonge kabla ya teknolojia hii mpya ya kamba za manila.

Tumeadhimisha miaka 52 ya uhuru wa Tanganyika tunahitaji kuyapitia yote mabaya na mema tuliyoyapitia na kujisahihisha kwa kuondoa vikwazo au vizingiti vyote vinavyofanya uti wa mgongo wa Taifa hili kuyumba.

Ahadi za serikali yetu zinasubiriwa kwa hamu kubwa, wakulima wako tayari kuiunga mkono serikali yao katika mchakato mzima wa kuwapa maisha bora kwa kila Mtanzania, jicho la serikali lipite kila idara na Rais asiwaonee haya wote wenye ajenda ya siri na uchumi wa watanzania.

Ni imani yangu kuwa ziara za Mheshimiwa Rais zitaleta mapinduzi katika kilimo kwani amejifunza mengi na hasa nchi za Asia ambao walikuwa maskini kuliko hata sisi lakini walifanya mapinduzi ya kilimo wakaendelea kwa kujitosheleza kwa chakula na ziada kuuza nje.

Kuna haja sasa kuwakubali waisrael, wajapan na wengineo waje nchini kufundisha kilimo vijijini aidha kwa kuajiriwa na serikali au kama misaada ya ufundi. Mfano ni mradi wa Sasakawa Global 2000 ulioendeshwa muda mfupi ulifundisha mbinu za kilimo zilizowezesha wakulima kuongeza kipato cha ekari ya mahindi kutoka gunia 15 hadi gunia 20 hadi 25.

 Walichofanya ni kuangalia upandaji wa mbegu na matumizi ya mbolea waliposhauri kisasa mabadiliko yalionekana.
0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text