Na Kenneth Mwazembe
Mbozi.
WANANCHI wa vijiji vya kata ya Myunga wilayani Mbozi mkoani Mbeya wanaishi kwa wasiwasi wakihofia kulipuka kwa mapigano kati yao na jamii ya wafugaji ya Wasukuma waliohamia katika vijiji hivyo, imefahamika.
Hofu hiyo imekuja baada ya kutokea ghasia na mapigano madogo ambapo wakulima wamevamia vibanda na makazi ya wafugaji hao na kuvibomoa na kuchoma moto wakishinikiza wafugaji hao kuondoka katika vijiji vyao.
Kwa upande mwingine, mfugaji mmoja Mwendesha Kitakuja (28) wiki iliyopita alimpiga na kumjeruhi Paulo Simkonda (36) kwa fimbo kichwani katika mapigano yaliyohusisha mashoka na mikuki ambapo viongozi walishinikiza mjeruhiwa kulipwa fedha za matibabu shilingi 160,000 na mjeruhi na kisha viongozi kulipwa shilingi 40,000 za ofisi.
Wakulima hao wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari aliyefika katika vijiji hivyo, wameeleza kutokuwa na imani na viongozi wao kutokana na kuwatuhumu kupokea fedha (rushwa) kutoka kwa wafugaji hao ambako kumewawezesha kupokelewa kijanja katika vijiji vyao.
Aidha wametaja vijiji vilivyokumbwa na zahama hiyo ya wafugaji kuwa ni Ipatikana, Chilangu, Nzoka, Mpui na Myunga ambapo kiini cha mgogoro huo ni usaliti wa viongozi uliobainika ambapo wameelezewa kujinufaisha binafsi kwa kuwepo kwa wafugaji hao.
Wameongeza kuwa wafugaji wanatoa pesa nyingi kuwapa viongozi wa vijiji na kata na kuwapuuza wakulima wanapopeleka malalamiko yao kuhusu uharibifu unaofanywa na mifugo.
Vily Daimon Sichalwe, balozi wa shina na 3 amelalamikia mwenendo mzima wa kuwapokea wafugaji hao na kwamba wao hawana sauti kwa viongozi wao na hakuna ushirikishwaji wala taarifa inayotolewa.
Naye Sadock Simkonda, mkulima wa kijiji cha Myunga aliyepambana na wasukuma kwa kutumia upinde na mishale na kuwafukuza kwenye eneo lake ameeleza kuwa wao wanawalaumu viongozi ambao wameshindwa kuweka utaratibu maalum wa kutenga maeneo ya kilimo na ufugaji na hivyo kuongeza uhasama baina ya pande mbili hizo.
Hali hiyo imewalazimu wakulima wengi kuhamia mashambani kwa msimu huu wa kilimo ili kulinda mashamba yao kutokana na mifugo hiyo.
Sinsco Simpanzye (45) mkulima ambaye shamba lake lilivamiwa na kuisha mwaka jana amelazimika kuhamia shambani msimu huu wa mazao kulinda hadi atakapovuna.
Katika jamii ya wafugaji, Mwendesha Kitakuja ameeleza kuwa yeye amehamia hapo kijijini kwa kukaribishwa na viongozi ambao walimdai kutoa jumla ya shilingi 630,000 kama fedha za kiingilio na mchango wa ujenzi wa shule ya sekondari ambapo yeye ana miliki ngombe 600 na kondoo 40 na kwamba alipohamia hapo kijijini alishauriwa kuoa binti wa wenyeji ili kudumisha mahusiano na kwamba ameoa tayari na kununua shamba la ekeri nane kwa shilingi 210,000 kwa Maiko Simpanzye.
Aidha alieleza kuwa yeye anawaleta ng’ombe wake kwa awamu na kila awamu hudaiwa kulipa fedha za kiingilio, na kwamba yeye anasaidia wanakijiji kwa kuwauzia maziwa.
Naye Masasila Daudi (22) mfugaji mwingine katika kijiji hicho anadai kuwa wao kama wafugaji wamelazimika kuhama kutoka kijiji cha Uzia kata ya Muze tarafa ya Mtowisa wilayani Sumbawanga na kuhamia hapo wakimfuata ndugu yao Mwendesha kwa kuwa yeye anafahamiana na viongozi na kwamba uhamiaji wao siyo mgumu kwani wanatumia jina moja la yule aliyekubalika kijijini hapo.
Viongozi waliotuhumiwa kupokea fedha hizo akiwemo diwani wa kata hiyo Credo Simwinga walipohojiwa kwa simu baada ya kutopatikana kijijini hapo wamekanusha kulipwa fedha hizo na kudai kuwa malipo hayo ni halali kwa kuwa kulikuwa na maelewano maalum.
Kaimu Mtendaji wa kijiji cha Myunga Yohana Simwanza amedai kuwa hali ya kuchukua fedha za wafugaji ni halali kwa kuwa wanachangia maendeleo na kwamba serikali za vijiji hazina mafungu ya kukarimu wageni kutoka wilayani na hivyo kuwalazimu kutumia akili ya kuwaomba jamii ya wafugaji kukidhi haja.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwepo mtandao wa upokeaji fedha hizo kuanzia ngazi ya kijiji, kata, tarafa hadi wilayani ambapo jeshi la polisi wilayani hapa wamedaiwa kupokea fedha hizo na wakala aliyetajwa kwa jina moja la Ibrahimu ambaye hupita kwa wafugaji na kuwachangisha ili kujiwekea uhalali wa wao kuendelea kuwepo katika vijiji hivyo.
Baadhi ya viongozi wa kijiji cha Chilangu wamedaiwa kupewa ng’ombe na wafugaji hao na kwamba walipokosana wafugaji hao walidai kurudishiwa ng’ombe hizo na hivyo kuwafanya viongozi hao kuchochea chuki kwa wakulima.
Afisa Mtendaji Kata ya Myunga Mdinde Mdinde alipotakiwa kutoa maelezo juu ya migogoro iliyoikumba kata yake alisema kuwa chanzo ni viongozi wenyewe wa vijiji ambao wametanguliza maslahi yao bila kujali athari zake kwani wafugaji nao wanastahili kuishi katika maeneo hayo kinachotakiwa ni mipango mizuri ya kugawa matumizi ya ardhi.
Aliongeza kuwa tukio la juzi ambalo naye alikamatwa na polisi kwa tuhuma za kumvamia mfugaji lilifanywa na Halmashauri ya kijiji cha Mpui ambapo viongozi wenyewe ndiyo walioongoza operesheni hiyo ya kubomoa vibanda na kuvichoma moto kwa lengo la kuwafukuza wafugaji.
Hata hivyo tathmini ya awali iliyofanywa na mwandishi aliyepita kuona hali halisi katika mashamba yanayodaiwa kufanyiwa uharibifu imebaini kuwepo uharibifu wa kawaida kwa mashamba hayo hali inayoonesha kuwepo kwa sababu nyingine zaidi ya hiyo inayodumisha chuki za chini kwa chini baina ya jamii hizo.
Mkuu wa wilaya ya Mbozi Halima Kihemba akizungumzia migogoro hiyo amesema amewapa maelekezo viongozi wote wa maeneo husika kukaa vikao vya pamoja na kufuata taratibu za kisheria ili wafugaji hao waishi bila kubughudhiwa na kuandaa ramani zitakazo idhinishwa na mamlaka husika.

0 comments:
Post a Comment
Thank you for reading the article