Kilimo kama uti wa mgongo wa
taifa hili umekuwa ni wimbo mtamu vinywani mwetu tangu Azimio la Iringa la
Siasa ni kilimo likisheheni kauli mbiu kadha wa kadha ambazo zimedumu kwa
takribani miongo minne.
Serikali katika awamu zake tatu
zilizotangulia ilijitahidi kuhamasisha kilimo kwa kuwaandaa wataalam na kutumia
wanasiasa katika majukwaa yao kuhimiza kilimo ambacho mpaka hivi sasa hakijawa
na mafanikio ya kuridhisha na hii ni kwa sababu ya kuwa na maneno mengi kuliko
vitendo yaani hatukuwa serious.
Azimio hilo lilipokelewa kwa
furaha na wananchi/wakulima wengi nchini na hasa wa hapa Mbozi ambao
walilipokea na kwenda nalo sanjali na operation vijiji ambapo mashamba ya
ujamaa yalianzishwa, vijiji vikasajiliwa chini ya sheria ya vijiji, mabwana
shamba wakasambazwa vijijini, mipango maalum ya kuboresha mazao ya biashara
ikaanzishwa na mafanikio yalianza kunukia kabla ya kuharibiwa na mipangilio ya
serikali au uongozi bora.
Nasema mwelekeo uliyumba kwa
kukosa uongozi bora kwani vyama vya ushirika vilivyoanzishwa hata kabla ya
uhuru vilivurugwa na badala yake zikaanzishwa mamlaka za mazao kama Mamlaka ya
pamba, ya Pareto na ile ya kahawa na tumbako nazo zilishindwa, zikavunjwa
zikaanzishwa Bodi za mazao hayohayo kwa upande wa mazao ya chakula likawepo
shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), mazao mengine ikawepo GAPEX yote hayo
imebaki kuwa historia.
Rais wa awamu ya kwanza hayati
J.K.Nyerere enzi za uhai wake alisema ili nchi iwe na maendeleo tunahitaji vitu
vinne, yaani ardhi, watu, uongozi bora na siasa safi
(Ujamaa uk
27). Sasa hapo sijui tulikosa nini kati ya uongozi bora na siasa safi kwani ardhi ilikuwepo
ya kutosha, na watu walikuwepo wa kutosha.
Wahimizaji hawa aidha wenyewe
hawakijui kilimo au wanafanya kazi kwa kuwa wameajiriwa kufanya hivyo ili mradi
waonekane wamesema na kwamba serikali inawalipa mishahara kwa kazi hiyo.
Pamoja na ukweli kwamba ardhi
inawaajiri asilimia 80 ya watanzania, bado ajira hii haina tija, mkulima
hajaweza kufaidi matunda ya kilimo ili kujiletea maendeleo.
Awamu ya nne ya Mheshimiwa JK
imeanza vizuri kwa kuainisha matatizo mbalimbali yanayoikumba sekta ya kilimo
na mifugo na migongano ambayo imekuwa ikitokea sehemu mbalimbali baina ya
wakulima na wafugaji.
Kuna matatizo yanayotokea yaliyo
nje ya uwezo wetu kama ukame, mafuriko n.k ,
kwa hayo tunamwachia Mungu, lakini kuna matatizo yanayosababishwa aidha na
mipangilio mibaya ya serikali au watu wachache wenye nyadhifa zao na wenye
dhima ya kuinua kilimo nchini.
Hapa ndipo penye matatizo yote
ambayo kwa mimi mkulima nitaishia kulaumu serikali kwani kila baya linapotokea
tunasingizia serikali hata kama yupo mtu
anayestahili kuwajibika kwa uzembe na pengine ni hujuma tu.
Umefika wakati wa Watanzania
kuufichua udhalimu na uhujumu wa baadhi ya watumishi serikalini walioamua
kurudisha maendeleo nyuma kwa makusudi na kukebehi dhana nzima ya serikali ya
awamu ya nne ya kumpatia maendeleo na maisha bora kila Mtanzania.
Katika kuhakikisha kuwa kilimo
ambacho ni uti wa mgongo kinazaa matunda wakulima wamejiandaa kuzalisha zaidi
na hasa baada ya bei ya mahindi, mpunga na maharage kupanda katika msimu
uliopita ambapo mahindi kwa hapa Mbozi yaliuzwa kwa shilingi 60,000 kwa gunia
la kilo 100, mpunga 75,000 kwa gunia la kilo 60 na maharage 90,000 kwa gunia la
kilo 100 .
Wakulima walitegemea ahadi ya
serikali ya kuwauzia pembejeo na hasa mbolea kwa bei ya ruzuku ambayo kwa hapa
Mbozi imezua kizazaa na malalamiko mengi kwa zoezi zima la ugawaji mbolea
lilivyoendeshwa na hasa pale walipoletewa mbolea za kukuzia badala ya zile za
kupandia ili hali majira ya mbolea hizo ni miezi ya Januari na Februari .
Tukimtafuta mchawi tunaambiwa
wizara ya kilimo ndiyo iliyopanga kuleta mbolea za kukuzia wakati wa kupandia,
sisi kama wakulima tunaamua kupanda bila
mbolea tukijua kwa makusudi kabisa kuwa kupanda bila mbolea ni kuvunja kanuni
za kilimo bora na hivyo kwenda kinyume na Azimio la Iringa la Siasa ni kilimo.
Mfano mzuri ni msimu wa 2007/8
ugawaji wa pembejeo ulikuwa wa vituko na kuonesha kuwa hujuma zilijulikana na
wahusika wenye dhamana ya kilimo. Makampuni yenye uzoefu wa kuuza na kusambaza
mbolea kwa miaka mingi yalipewa mgawo mdogo sana wa kuuza hizo mbolea mfano
mzuri ni kampuni ya mbolea Tanzania (TFC) wakapendelewa makampuni ya binafsi,
mfano TFC iliruhusiwa kuuza tani 650, Export Traders tani 2497, Premium tani
205, STACCO tani 1077, Chapameli tani 1500, Nyiombo tani 154 na kufanya jumla
ya tani 6084 kwa wilaya badala ya mahitaji ya jumla ya tani 28,000.
Msimu 2012/13 mbolea za kupandia
zililetwa wilayani hapa mwezi Februari badala ya Oktoba je hao wakubwa
wanadhamira gani na kilimo? Aibu tupu!
Kama dhamira ni kuinua kilimo kwa
faida ya taifa zima kuna haja sasa Mheshimiwa Rais kuangalia muundo wa baadhi
ya vyombo husika vilivyotarajiwa kufanikisha zoezi zima la kusambaza pembejeo
na hasa wizara ya kilimo.
Wizara ya kilimo kupitia Mfuko wa
Pembejeo inatoa mikopo kwa ajili ya kuinua na kuboresha kilimo, kwa mujibu wa
kipeperushi cha Mfuko huo, Mfuko unatoa mikopo ya pembejeo za kilimo na mifugo,
mikopo ya ununuzi wa matrekta mapya, mikopo ya kukarabati matrekta na mikopo ya
kuanzisha vituo vya kukodisha matrekta (Farm Service Centres)
Inawezekana kabisa kuwa Mfuko wa
Pembejeo haujawezeshwa kiasi cha kutosha kulingana na mahitaji yalivyo hivi
sasa kwani awamu hii ya nne imedhamiria kuinua kilimo na hivyo kila kona
inahitajika kwenda kwa kasi mpya na nguvu mpya bila hiyo mikopo wakulima wetu
wataishia jembe la Adamu na Hawa.
Kazi kubwa inayofanywa na Mfuko
wa Pembejeo wa Taifa (AGITF) inahitaji kuungwa mkono na kuwekwa jukwaani ili
taasisi nyingine ziige. Mfuko huo chini ya Mkurugenzi wake Mariam Nkumbi licha
ya kuwa na watumishi wachache, wanajitahidi kuzunguka katika mikoa yote na
kujua mahitaji ya wakulima, kutoa mikopo na ufuatiliaji wa marejesho.
Serikali inapaswa kuongeza fedha
kwenye mfuko huu sanjali na maandalizi ya kuanzisha benki ya kilimo. Mfuko huu
umesimama badala ya benki kwa muda mrefu na umekuwa ukitoa mikopo kwa
kuzikubali hatimiliki za kimila ambazo zinaenda sambamba na mipango ya serikali
ya Mkukuta na Mkurabita.
Mfuko huu ungeweza kuwasimamia
mawakala katika suala zima la uagizaji na usambazaji wa pembejeo kwa
ushirikiano na mashirika mengine kama AGRA n.k.
Mapinduzi ya kilimo ni lazima,
yalenge kuongeza maeneo ya uzalishaji kutoka hapa tulipo , mkulima wa jembe la
mkono awezeshwe afikie zana za kukokotwa na wanyama, na yule anayetumia wanyama
kazi apewe trekta kulingana na uwezo wake.
Pembejeo zifike vijijini aliko
mkulima kwa utaratibu mzuri na kwa wakati stahili na si kama
hivi sasa mkulima anahitaji mbolea za kupandia anapelekewa za kukuzia na
atakapohitaji za kukuzia atapelekewa za kupandia hicho ni kichekesho.
Kwa bei hizi hata ungelikuwa ni
wewe kwa vyovyote ungelikata tamaa na kuamua kuzalisha chakula cha kuganga njaa
tu na si cha kibiashara na kujiongezea kipato.
Mwanzoni mwa Disemba hii 2013
nilimsikia ndugu David Mwaibula akielezea mipango ya kilimo na uwekezaji katika
kipindi cha Baragumu kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Channel Ten
kuwa ni lazima kiende kwa wakati. Alifafanua kilimo enzi za mkoloni kuwa
alihimiza mazao hayo na kuweka soko la uhakika kwani walaji walikuwa wengi na
mahitaji ya dunia yalikuwa makubwa. Alitoa mfano wa zao la mkonge ambalo
lilitoa katani zilizo tumika kutengeneza kamba. Meli zote zilitumia kamba za
nanga za mkonge kabla ya teknolojia hii mpya ya kamba za manila.
Tumeadhimisha miaka 52 ya uhuru
wa Tanganyika tunahitaji kuyapitia yote mabaya na mema tuliyoyapitia na
kujisahihisha kwa kuondoa vikwazo au vizingiti vyote vinavyofanya uti wa mgongo
wa Taifa hili kuyumba.
Ahadi za serikali yetu
zinasubiriwa kwa hamu kubwa, wakulima wako tayari kuiunga mkono serikali yao katika mchakato mzima
wa kuwapa maisha bora kwa kila Mtanzania, jicho la serikali lipite kila idara
na Rais asiwaonee haya wote wenye ajenda ya siri na uchumi wa watanzania.
Ni imani yangu kuwa ziara za
Mheshimiwa Rais zitaleta mapinduzi katika kilimo kwani amejifunza mengi na hasa
nchi za Asia ambao walikuwa maskini kuliko
hata sisi lakini walifanya mapinduzi ya kilimo wakaendelea kwa kujitosheleza
kwa chakula na ziada kuuza nje.
Kuna haja sasa kuwakubali
waisrael, wajapan na wengineo waje nchini kufundisha kilimo vijijini aidha kwa
kuajiriwa na serikali au kama misaada ya ufundi. Mfano ni mradi wa Sasakawa
Global 2000 ulioendeshwa muda mfupi ulifundisha mbinu za kilimo zilizowezesha
wakulima kuongeza kipato cha ekari ya mahindi kutoka gunia 15 hadi gunia 20
hadi 25.
0 comments:
Post a Comment
Thank you for reading the article