Thursday, February 14, 2008

UBOVU WA BARABARA YA MBEYA-TUNDUMA

Posted by Unknown On 11:25 AM No comments
Na Kenneth Mwazembe
Mbeya

Barabara ya Mbeya -Tunduma iliyokarabatiwa miaka minne iliyopita na kampuni ya ukandarasi ya kichina ya China Road & Bridge Corporation
ikisimamiwa na NorConsult As iliyogharimu zaidi ya shilingi bilioni 11 imeanza kuharibika na kwamba hatua za haraka zisipochukuliwa za kudhibiti
uharibifu huo katika maeneo mengi ambayo ni korofi yatalazimika kukarabatiwa upya kwa gharama kubwa.

Ukarabati wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 70 ni miongoni mwa miradi iliyojengwa katika kipindi cha awamu ya tatu chini ya Rais mstaafu
Benjamin Mkapa ambao ulianza mwaka 2002 na kukamilika 2005 kiwango cha lami ikianzia kijiji cha Nanyala hadi Tunduma ambako ni mpakani mwa
Tanzania na Zambia.

Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari umebaini kuwa barabara hiyo imeharibiwa na watu ambao wamekuwa wakilazimisha kupita kwa kukatiza
kwenye barabara hiyo na kusababisha maeneo mengi ya barabara kuharibika kingo na mabega (shoulders) na kuchimbika kiasi cha kumeguka.

Maeneo ya barabara ya lami yaliyoonekana kumeguka ni Mlowo, Ivwanga, Nselewa, Hanseketwa, Chimbuya, Mpemba, Chapwa na Tunduma ambapo
juhudi za serikali kupitia Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoa wa Mbeya zinahitajika kufanywa haraka iwezekanavyo ili kuilinda barabara isiharibike zaidi.

Hata hivyo imebainika kuwa maeneo mengine uharibifu umefanywa makusudi na wananchi ili kupata urahisi wa kuingia barabara kuu kwa kuwa maeneo husika
hayana mchepuo wa barabara (Access road).

Meneja wa Kampuni ya Ujenzi wa barabara ya China Road & Bridge Corporation Guo Bingfeng alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusu uharibifu wa barabara
hiyo alisema kuwa kampuni yake ilishakabidhi kwa serikali barabara hiyo miaka mitatu iliyopita hivyo hawezi kusema lolote juu ya uharibifu wa barabara hiyo
ambayo ni tegemeo kubwa kwa kusafirishia mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda katika nchi za Zambia, Zimbabwe, Botswana, Kongo na Afrika ya Kusini.


Baadhi ya madereva wa magari makubwa ya mizigo yanayosafirisha mizigo kwenda nchi jirani ambao wameomba majina yao yahifadhiwe wameeleza kuwa
uwezekano wa kutokea ajali hasa kuwagonga watembea kwa miguu na waendesha baiskeli ni mkubwa kwa kuwa eneo la kupita magari nao wanalazimika kupita
humo baada ya kingo na mabega ya barabara kuharibika.

Wananchi wa kawaida wameeleza masikitiko yao kuona Mamlaka yenye majukumu ya kuangalia usalama wa barabara (Tanroads) wamekaa kimya ilihali barabara
iliyoigharimu serikali mabilioni ya shilingi ikiharibika.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya John Mwakipesile ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Bodi ya barabara ya mkoa alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusiana na uharibifu
huo wa barabara alimtafuta meneja wa Tanroad Lucian Kilewo ili aweze kutoa ufafanuzi zaidi ambapo alifika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa ambako waandishi walikuwa
wakimsubiri.

Kilewo alikiri kuwepo kwa uharibifu huo na kwamba ofisi yake inaandaa bajeti ya ukarabati na kwa kuanzia wameanza kujaza kokoto (base materials) maeneo yenye
mashimo na kwamba ataanza kujenga kingo zilizoharibika kwa mawe ili kuilinda barabara.

aliongeza kuwa kilomita sita kutoka Songwe viwandani hadi Nanyala eneo korofi katika barabara hiyo ukarabati wa muda umeanza lakini wanatarajia kufumua kipande hicho
ili kijengwe upya.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text