Thursday, February 28, 2008

ULANGUZI NYAMA YA NGOMBE

Posted by Unknown On 12:46 AM No comments
Na Kenneth Mwazembe
Mbozi

Walaji wa nyama ya ng’ombe katika miji ya Vwawa, Mlowo na Tunduma wilayani Mbozi wamewalalamikia wauza nyama kwa kuwauzia bei kubwa na kupima chini ya vipimo vilivyo idhinishwa na serikali.

Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti wateja hao wamedai kuwa wanapokwenda buchani kununua nyama hupimiwa robo tatu ya kilo kama kilo moja.

Jackson Mwamlima alieleza kuwa bei ya nyama imepanda kutoka sh 2000 hadi 2400 kwa kilo wakati huohuo hupimwa ¾ ya kilo na kumfanya mlaji kuibiwa sh 750 kwa kila kilo inayonunuliwa.

Aidha walaji hao wamedai kuwa ujanja mwingine unaotumiwa na wauza nyama ni kuongeza uzito wa ziada kwenye bakuli la mizani kwa kuweka chuma au sumaku au jiwe la kupimia ili kwamba nyama inapowekwa ndani ya bakuli hilo mizani husoma uzito wa nyama na uzito wa kitu kilichoongezwa.

Kwa upande wa wauza nyama hao walipohojiwa na gazeti hili kwa nyakati tofauti, walikanusha kuwapo kwa hujuma hizo na kwamba inatokea baadhi ya wateja wanakuwa na fedha pungufu ya bei iliyopangwa, hivyo wanakadiriwa kiasi kinacholingana na fedha yao waliyolipa pasipo kufuata kipimo cha mzani.

Queen Chaula mmoja wa wamiliki wa mabucha katika mji wa Vwawa alipohojiwa alisema kuwa yeye akiwepo katika biashara yake haruhusu mchezo huo kufanyika, lakini hata hivyo hawezi kuwakatalia vijana wake ambao huwaachia kuuza anapokuwa na dharula ya kutoka kidogo, kwani alishapokea malalamiko kadhaa yanayohusiana na suala hilo.

Naye Kamjanja Nzunda alipohojiwa kuhusu malalamiko hayo alijibu kuwa yeye akiwa mfanyabiashara wa nyama ameyasikia malalamiko mengi kutoka kwa wateja wao lakini yeye ameilinda biahsara yake kwa kuhakikisha anatoa huduma ya haki na kwamba ameshawafukuza vijana wake watatu waliobainika kuwaibia wateja.

Bei ya kununua ng’ombe mwenye uzito unaokadiriwa kuwa kilo 150 ni kati ya sh. 250,000 na 300,000/=, wakati bei ya kilo moja ya nyama ni kati ya sh. 2200 na 2400, ambayo hata hivyo kipimo chake ni cha ujanja ujanja.

Aidha wenye mabucha hao wamepata fursa ya kufanya watakavyo kutokana na hali ya upatikanaji wa vitoweo mbadala kama samaki, wilayani hapa ambao umekuwa mgumu kutokana na barabara iendeyo ziwa Rukwa (Mlowo – Kamsamba) kuwa mbovu isiyopitika hasa wakati wa masika, pia upungufu wa samaki katika ziwa hilo, kwani hata wale wanaojaribu kusafirisha samaki hao kwa punda na baiskeli huleta samaki wadogo na ambao huuzwa kwa bei ghali.

Soko la samaki katika nchi za Zambia na Kongo nalo limeongeza uhaba wa samaki baada ya wafanyabiashara wa nchi hizo kutoa malipo mapema kwa mawakala na wakati mwingine huenda wenyewe ziwani ambapo huwasafirisha samaki hao bila kulipa ushuru wakitumia njia za panya.

Faiton Silon, mkazi wa mji wa Tunduma ameeleza kuwa wafanyabishara wa Kongo na Zambia wanayo nafasi ya kununua samaki wote kwa kuwa wanao uwezo wa kukodi magari ya kuwafikisha ziwani mara hali ya hewa inaporuhusu tofauti na wenyeji ambao wanategemea usafiri wa jumuia kutokana na mitaji yao kuwa midogo.

Uchunguzi uliofanywa kufuatia tatizo hilo umebaini kuwa hata vitoweo kama kuku na mbuzi vimeadimika kutokana na ufugaji duni ambao mazao yake hayatoshelezi walaji, ambapo kitoweo pekee chenye bei nafuu na kinachopatikana kirahisi ni kitimoto, ingawa kutokana na imani mbalimbali za dini baadhi yao ni haramu kukitumia, kwani hata bei yake ni nafuu zaidi ambayo ni kati ya sh. 1500 na 2000 kwa kilo moja.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi Zaraf Yango alipotakiwa kuzungumzia suala hili alikiri kupokea malalamiko hayo kupitia kwa Ofisa wake wa Idara ya Biashara kwamba kuna malalamiko yaliyotolewa na wananchi juu ya suala la upunjaji linalofanywa na wafanyabiashara hao.

Meneja na wakala wa vipimo Mkoani Mbeya Willy Mbise alipohojiwa kwa simu kuhusu kero hilo alikiri kupelekewa malalamiko hayo na Afisa Biashara Saleh Ibrahim na kwamba ofisi yake imejipanga kufanya ukaguzi wiki ijayo .

Aliongeza kuwa mara ya mwisho kukagua mizani za wilaya ya Mbozi ilikuwa ni Agosti 27 mwaka jana, na kwamba idara yake haina ofisi wilayani hapa.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text