Saturday, November 22, 2008

AJALI YA LORI YAUA 10 WAMAUME 5 WAKE 5

Posted by Unknown On 12:12 AM No comments
Na Kenneth Mwazembe
Mbozi.

Watu kumi wamefariki dunia na wengine kumi kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea jana usiku katika kijiji cha Nambinzo wilayani Mbozi mkoani Mbeya.

Gari hilo aina ya Mitsubishi Fuso (maarufu kama Machame Trans) ambalo namba zake hazikuweza kupatikana mara moja lilikuwa likiendeshwa na dreva aliyejulikana jina moja la Ray lilitoka Kamsamba likielekea mjini Mlowo likiwa limepakia magunia 70 ya mahindi na magunia kadha ya samaki.

Mganga wa zamu katika hospitali ya wilaya Ferdinand Lusawa amewataja majeruhi kuwa ni Wiliam Mwakaboko (37), Nuhu Saanane (35), Aliko Lukilisho (40), Josephat Peter (30), Elia Alam (59) na Fredrick Mwalyagile (35).

Wengine ni Tuma Maiko (22), Lazaro Amani (27), Dorika Ishimael (44) na mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Allen.

Amewataja marehemu wawili waliotambuliwa kwa jina moja moja ambao ni Enock na Tembo wengine nane bado hawajatambuliwa ambapo kati ya marehemu wanaume ni 5 na wanawake 5.

Mmoja wa majeruhi hao Wiliam Mwakaboko akielezea ajali hiyo anasema kuwa ilikuwa majira ya saa 4 usiku walipofika eneo la Nambinzo gari hilo lilikwama kutokana na tope kufuatia mvua iliyokuwa imenyesha eneo hilo.

“Baada ya kulikwamua gari tulianza safari, dereva alidai kuwa atafidia muda ili tuwahi kufika mjini Mlowo hivyo gari lilikuwa kwenye mwendo kasi ambapo mbele aliona kufusi kilichomwagwa barabarani na alipojaribu kukwepa akiwa katika mwendo huo gari lilimshinda na kupinduka” alisema.

“Kilicholeta madhara kwa wenzetu ni magunia yaliyowafunika na kuwakandamiza abiria na waliofika kutoa msaada walikuwa wanawake ambao walishindwa kuondoa magunia na kufanya hali kuwa kama mnavyoona na hata sisi watano tumevunjika miguu” aliendelea kueleza.

Jeshi la polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo unafanyika.

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text