Monday, March 8, 2010

Simbeye azikwa

Posted by Unknown On 11:14 PM No comments
Buriani David Lumbala Simbeye

Katika mazishi yake yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Mbeya baada ya mwili wa marehemu kuagwa jijini Dar na Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda na viongozi wengine waandamizi wachungaji waliachiwa sehemu yao ya ujumbe kama hivi: 

Watanzania wameshauriwa kumchagua kiongozi anayemwogopa Mungu bila kujali dini yake katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania Alinikisa Cheyo katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi wa Viongozi marehemu David Simbeye yaliyofanyika kijijini kwake Mbimba wilayani Mbozi.
Alisema mwaka wa uchaguzi umewadia ni vizuri wakachaguliwa viongozi wanaomwogopa Mungu bila kujali dini au madhehebu yao na ambao wanauwezo wa kuongoza bila ya kuangalia fedha chafu wanazogawa.

“Mwaka huu wa uchaguzi watu wanagawa fedha chafu nawe ukizipokea utakuwa mchafu na utakuwa umeuza uhuru wako kwa fedha ambayo haiwezi kukuletea maendeleo” Cheyo alisisitiza.

Hata hivyo Cheyo alidai kuwa sababu kubwa ya watu kupenda kupokea rushwa hiyo ya uchaguzi ni kutokana na vijana wengi kutokuwa na mipango thabiti ya kazi hivyo kujiweka katika hali ya uhitaji ambapo akiletewa fedha hiyo chafu hatakuwa na ujasiri wa kuikataa.

Marehemu Simbeye ambaye alifariki Februari 28, mwaka huu alizaliwa mwaka 1933 wilayani Ileje na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya Itumba mwaka 1945-50 na baadae kujiunga na Mbozi Middle School mwaka 1951-hadi 1952.

Mwaka 1953 alijiunga na jeshi la polisi alikofanya kazi hadi 1964 alipohamishiwa Ikulu ambako amefanya kazi hadi alipostaafu 1988 akiwa mkuu wa kikosi cha ulinzi na akiwa ni mlinzi binafsi wa Mwalimu Julius Nyerere (bodyguard) baadae Rais Ali Hasan Mwinyi.

Marehemu David Simbeye alisafiri kutoka Mbozi kwenda Dar siku hiyo ya Februari 28 ambapo alifika jijini Dar majira ya saa tisa alasiri na kufikia katika hoteli na baadaye alijisikia vibaya hali iliyomfanya ampigie simu mtoto wake Leonard ambaye alifika muda mfupi baada ya mauti kumpata.
Maelezo zaidi yalitolewa na msemaji wa familia ambaye pia ni mpwa wa marehemu Henry Mgala Bantu aliyeeleza kuwa safari ya marehemu kwenda Dar ilikuwa kwa minajili ya kumwona daktari kwa maradhi ya moyo aliyokuwa akilalamika mara kwa mara.

Akiwa kijijini hapo Simbeye alikuwa anajishughulisha na kilimo cha kahawa huku akitumia usafiri wa baiskeli kumleta mjini Vwawa kama kilometa 2 ½ kupata mahitaji yake.

Mzee Simbeye atakumbukwa kwa ushauri na nasaha zake ambazo hakuacha kuzitoa kwa vijana kila mnapoonana.

"Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake libarikiwe"

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text