Friday, March 14, 2008

HOFU YAZIDI SHULE YA SEKONDARI

Posted by Unknown On 1:19 AM No comments
Na: Kenneth Mwazembe – Mbozi.

Wananchi wa Kata ya Msia wilayani Mbozi mkoani Mbeya wamesikitishwa na hali ya hofu inayowakabiri walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Msia kufuatia mlolongo wa matukio ya kihalifu likiwepo la kupigwa risasi na kufa mwanafunzi mmoja mwezi uliopita, Tanzania Daima limegundua.

Hali ya usalama katika shule ya sekondari Msia iliyopo wilayani Mbozi mkoani Mbeya inaendelea kuwa ya wasiwasi kufuatia vitendo vya uhalifu na vitisho vinavyofanywa huku uongozi ukiwa haujui la kufanya.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi aliyefika shuleni hapo wananchi mbalimbali pamoja na walimu waliopo katika shule hiyo, walisema wamekuwa wakiishi maisha ya hofu kufuatia matukio ya uhalifu yanayofanywa na wanafunzi pasipo hatua zozote kuchukuliwa na uongozi wa shule.

Mmoja wa walimu ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini alisema wamekuwa wakiishi kwa hofu hali ambayo inapelekea baadhi ya walimu wenzake kutaka kuhama shule ili kwenda mahali pengine ambapo usalama wao utakuwa ni wa uhakika.

Alidai kuwa wamejaribu kujadili hatma ya maisha yao shuleni hapo na kupitisha mapendekezo kadhaa ikiwemo kumuona Mkuu wa Mkoa wa Mbeya John Mwakipesile ili aweze kuwasaidia kutatua matatizo yanayoizunguka shule hiyo baada ya uongozi wa shule na wilaya kushindwa kufanya hivyo.

Wameelekeza lawama kwa Bodi ya Shule hiyo ambapo imeonekana kushindwa kutekeleza majukumu yake na kwamba baadhi ya wajumbe wa Bodi hiyo hawana sifa za kufanya kazi hiyo na wametoa mapendekezo ya kuvunjwa Bodi ya shule hiyo ili iundwe Bodi nyingine ambayo itajenga mahusiano mazuri baina ya shule na wanajamii wanaoizunguka shule hiyo.
Mwalimu huyo akielezea matukio hayo alisema kuwa mwishoni mwa mwaka jana wanafunzi walifanya fujo iliyosababisha uharibifu wa mali kwa kufyeka kahawa na kuharibu saruji na mbolea vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh. 25 milioni, tukio lingine ni lile la hivi karibuni ambapo mwanafunzi mmoja aliuawa na Polisi wakati akiwa pamoja na watu wengine wasiojulikana walipofika shuleni hapo kwa nia ya kutaka kuvunja na kuiba, lakini kwa bahati nzuri taarifa za ujio wao zilivuja hivyo kupelekea polisi kuweka doria usiku huo.

Pamoja na hayo, walimu hao wameendelea kudai kuwa hivi sasa wamepata taarifa kwamba kuna kikundi kina mpango wa kutaka kuichoma moto shule hiyo taarifa ambazo pia polisi wamezipata, hivyo kwa kuwa matukio yote mabaya yaliyotokea shuleni hapo taarifa za kuwapo kwake ziliwahi kuvuja mapema, wanaamini kuwa hata tukio hilo linaweza kuwa kweli na kwa vile tayari wanawataja baadhi ya walimu kuwa nao watawashambulia kwa kuwa ni kikwazo cha kufanya mambo yao.

Mwananchi mmoja anayeishi jirani na shule hiyo Daudi Simkoko aliliambia gazeti hili kuwa matatizo yanayotokea katika shule hiyo yanatokana na uongozi mbovu ambao haushirikiani na watumishi pamoja na wananchi wengine katika kuimarisha nidhamu ya wanafunzi, kwani matukio haya yanatokana na utovu wa nidhamu kwa wanafunzi.

Alisema hivi sasa baadhi ya walimu wameondoka kwa madai ya kwenda kusoma na kusababisha upungufu mkubwa wa walimu, hali ambayo imesababisha wazazi kuamua kuitisha mkutano utakaofanyika wiki ijayo ili kujadili namna ya kuwapata walimu wa muda ambao watawalipa wenyewe.

Afisa Mtendaji wa kata ya Msia Partson Nsyengula alipoulizwa kama kata yake ina mkakati gani wa kurejesha mahusiano baina ya wanafunzi, walimu na wanakijiji alisema kuwa Kamati ya ulinzi na usalama ya kata imepitisha mapendekezo ya kuongeza ulinzi kwa kuajiri walinzi wengine wanne, pia wamependekeza kununua bunduki badala ya kulinda kwa kutumia marungu.

Nsyengula alikiri kuwa Bodi ya shule hiyo haijawahi kufanya vikao vyake hivyo kuongeza kuwa pengine matatizo yaliyopo yanatokana na kulimbikizwa kwa matatizo mengi madogo madogo.

Mwenyekiti wa Bodi ya shule Francis Mwakabenga alipohojiwa na gazeti hili kuhusu migogoro ya shule hiyo alidai yapo mambo mengi yaliyochangia na kwamba atatoa ufafanuzi wake kimaandishi kutokana na simu yake kuishiwa chaji hata hivyo aliomba muda wa kujipanga ili ajibu maswali ya gazeti hili.

Mkuu wa shule Absolom Mwakyoma alipoombwa kuzungumza na mwandishi wa habari hizi baada ya kumkosa shuleni na kukutana naye njiani aliahidi kuja siku inayofuata kwani siku hiyo alikuwa na haraka.

“hivi sasa niko Busy naelekea Mbeya, hata baadaye nikirudi sitafika hapa nitakwenda kijijini, lakini nitaangalia ili nikutafute” alieleza Mkuu huyo kwa kusisitiza lakini hadi tunakwenda mitamboni hajatokea.

Mratibu wa Elimu ya sekondari wilayani hapa Mathias Lyoto alikiri kuwa migogoro inayoonekana inatokana na matatizo ya kiuongozi na kwamba mapendekezo ya wakaguzi wa shule wa kanda yamepelekwa ngazi za juu kwa kubarikiwa na hatua zaidi likiwepo la kuvunjwa Bodi ya Shule.

Aliongeza kuwa mengi ya matatizo hayo yamekuwepo kwa muda mrefu na kwamba Bodi ilikuwa haifuati ratiba ya kufanya vikao mara nne kwa mwaka kitu kilichofanya matatizo kuwa makubwa.

Uchunguzi zaidi wa gazeti hili umebaini kuwepo kwa makundi matatu katika migogoro hiyo, ambapo kundi moja ni la wanafunzi wanaoungwa mkono na baadhi ya walimu wasioridhika na shule inavyoendeshwa ambapo wamedai inaendeshwa kidikteta na mkuu wa huyo wa shule.

Kundi jingine ni la wanafunzi walio upande wa walimu wanaokubaliana na Mkuu huyo wa shule na hili ndilo lililovujisha habari za kuwepo kwa njama za kutaka kuvunja na kuiba shuleni hapo ambapo walitoa taarifa na polisi wakawahi kujipanga na kumuua mwanafunzi aliyekuja kuvunja kama ilivyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari.

Kundi la tatu ni la baadhi ya wananchi ambao hawaridhiki na mwenendo mzima wa maendeleo ya shule hiyo wakiwatuhumu viongozi kutafuna michango ya shule na kugomea kuchangia shule nyingine inayojengwa katika kata hiyo ambayo ilimfanya Mkuu wa wilaya Halima Kihemba kumsimamisha uenyekiti wa kijiji Mwashitete miezi miwili iliyopita.

Hata hivyo uchunguzi zaidi umebaini suala la migogoro katika shule hiyo yanabeba pia sura ya kisiasa kufuatia hatua zilizochukuliwa na Mkuu huyo wa wilaya ambapo anadaiwa kutoshirikisha uongozi wa chama tawi la Msia ambalo linaendelea kumtambua Mwashitete kama mwenyekiti halali kwani hakuna taratibu kichama zilizochukuliwa dhidi yake.

MWISHO.

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text