Wednesday, March 26, 2008

Posted by Unknown On 3:22 AM No comments
a Kenneth Mwazembe
Mbozi

Wananchi wa miji ya Vwawa, Tunduma na Itaka wilayani Mbozi mkoani Mbeya wamewalalamikia watendaji serikalini likiwemo Jeshi la Polisi kwa unyanyasaji dhidi ya raia na madaraka ya watendaji wa vijiji yasiyo na mipaka.

Malalamiko hayo yalitolewa jana kwa taasisi ya Vantage Communications inayojishughulisha kukusanya takwimu juu ya matatizo ya wananchi likiwemo la urasilimishaji mali na biashara.

Awali kabla ya kuanza kupokea malalamiko hayo Mtakwimu Peter Mayeye wa Turaco Systems Consultant (T) Ltd inayofanya kazi kwa niaba ya Vantage Communications aliwatoa wasi wasi wananchi na kwamba wakitoa maoni yao hawatatajwa majina na hivyo kuwaondoa wasiwasi waliokuwa nao kabla.

Wakielezea unyanyasaji wa Jeshi la Polisi wamesema polisi wana tabia ya kuwafungulia kesi za kubambikiza wakati wowote usipokubaliana na matakwa yao, watuhumiwa kupigwa bila sababu na wengine wamesababishiwa vilema baada ya kupigwa na kuvunjwa mikono na miguu.

Wananchi wengine wamedai kuwa kusikia kuwa kutakuwa na polisi jamii lakini hawajaziona hatua za makusudi za kuwaelimisha wananchi kwa kuwa Jeshi hilo limejifanya adui wa wananchi.

Wameomba pia kuwepo chombo kinachoangalia utendaji kazi wa Jeshi la Polisi kwani mwananchi akiwa na malalamiko dhidi ya Jeshi hilo hana pa kuyapeleka kwani ukimshitaki kwa Kamanda wa Mkoa hawezi kuwachukulia hatua yoyote kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kulindana na kulinda heshima ya Jeshi hilo.

Watendaji wa vijiji na kata pia wamelalamikiwa kwa kujichukulia hatua wasizostahili na hasa wanapodai michango ya ujenzi wa sekondari ambapo imeelezwa kuwa huwakamata wananchi na kuwafungia katika mahabusu zao huku wakilazimishwa kulipa michango na gharama za kuwakamata.

Kero nyingine iliyolalamikiwa ni zoezi zima la uandikishaji hati miliki za kimila ambapo imeelezwa na wananchi kuwa urasimu ni mkubwa na utaratibu wa gharama za picha kwa kila eneo ni mzigo usiobebeka.

Taasisi ya Vantage Communications yenye makao yake makuu Uganda ina tawi hapa Tanzania ambalo limeajiriwa na MKURABITA ili kukusanya maoni ya wananchi katika mchakato mzima wa kujua kero za wananchi hasa katika zoezi la urasilimishaji mali.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text