Saturday, May 10, 2008

SIKU YA WAUGUZI DUNIANI

Posted by Unknown On 4:31 AM No comments
Na Kenneth Mwazembe
Mbozi

Sherehe za maadhimisho ya kumbukumbu ya muasisi wa fani ya Uuguzi duniani Florence Nightngale zitafanyika kesho kimkoa katika wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya.

Akizungumza na gazeti hili jana ofisini kwake Afisa Muuguzi hospitali ya wilaya ya Mbozi Michael Abdi amesema wataadhimisha kumbukumbu hiyo kwa kumuenzi Florence Nightngale kwa kuwasha mishumaa mawodini, kuwatembelea wagonjwa na kutoa zawadi.

Ameeleza kuwa wilaya imejiandaa kupokea wageni 500, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya John Mwakipesile anatarajiwa kuwa mgeni rasmi. Sherehe hizi zinatarajiwa kuhudhuriwa na wakuu wa wilaya zote nane na Wakurugenzi wa Halmashauri zote za mkoa huu pamoja na Waganga wakuu wote wa hospitali.

Abdi meendelea kueleza kuwa wauguzi wanaadhimisha siku hiyo wakiwa bado wanayo matatizo kadhaa katika fani hiyo ikiwamo mishahara midogo isiyolingana na majukumu yao, kilio cha posho ya mazingira hatarishi na uchache wa vyuo vya wauguzi ambapo uchache wa wauguzi unawafanya waliopo kufanya kazi kwa zaidi ya masaa stahili bila kulipwa posho.

Maadhimisho ya sikukuu hiyo ambayo hufanyika kila mwaka Mei 12 ni kumkumbuka muanzilishi wa fani ya uuguzi duniani Florence Nightngale aliyezaliwa mwaka 1820 na kufariki 1910 ambapo alifanya kazi katika mazingira magumu akitumia mishumaa na taa za kandili wakati wa usiku.

Kwa mujibu wa afisa huyo sherehe hizo zitapambwa kwa vikundi vya ngoma toka Nambinzo Mawazo Tulyanje, Mang’oma toka Msanyila, kwaya mbili za wauguzi wenyewe na kikundi cha sanaa cha Nyota toka mjini Mbeya kitakacho onesha sarakasi, maigizo na ngoma.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text