Tuesday, May 20, 2008

Na Kenneth Mwazembe
Mbozi MAJAMBAZI

Watu wawili wanaodhaniwa kuwa majambazi wameuawa kwa kuchomwa moto na wananchi katika kijiji cha Chimbuya wilayani Mbozi mkoani Mbeya.

Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Alfred Siwale amewataja waliouawa kuwa ni Ruben Mbukwa (52) mkazi wa kijiji cha Ukwile na mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Shibanda mkazi wa Tunduma.

Siwale ameeleza kuwa mnamo Mei 18 mwaka huu majambazi wapato 7 walivamia duka la Aswile Kibona na kuiba bidhaa zote na kisha kutokomea ambapo usiku wa pili walirudi tena na kuvunja nyumba alimokuwa amelala na kumjeruhi kwa risasi na mapanga ambapo haijajulikana kama walipata kiasi chochote cha fedha.

Wezi hao kabla hawajaanza unyama huo walifunga milango ya majirani kwa nje na kisha kupiga hewani risasi nne kuwatisha waliotaka kutoa msaada na baadaye kutoroka ambapo wananchi waliamua kufanya msako uliowakamata watu 7.

Mmoja wa waliouawa Ruben Mbukwa alikutwa na risasi moja ya shotgun iliyoamsha hasira za wananchi na kumpa kipigo na baadaye moto.

Polisi waliofika kijijini hapo wamefaulu kuwakamata Mafikiri Sinkala (34), mkazi wa kijiji cha Mpemba, Mwinyi Nyilu (25), Alex Msukwa (25), Majuto Mwamgunda (17), Victor Mwembe (23) wote wakazi wa Ukwile.

Majeruhi Aswile Kibona amekimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mjini Mbeya kutokana na majeraha ya risasi aliyopata.

Jeshi la Polisi wilayani hapa limethibitisha kutokea tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea ambapo bado hawajaipata silaha aina ya shotgun iliyotumika katika uhalifu huo.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text