Friday, June 13, 2008

WANANCHI KUNUFAIKA NA HAKIMILIKI

Posted by Unknown On 2:07 AM No comments
Na Kenneth Mwazembe
Mbozi.

WANANCHI wilayani Mbozi wameanza kunufaika na hakimiliki za kimila baada ya mabenki na asasi nyingine za fedha kuzitambua na kuzikubali kwa dhamana ya mikopo, imeelezwa.

Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Levison Chilewa katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Amesema hadi Juni 11 mwaka huu jumla ya Hatimiliki za kimila 2314 zimesajiliwa na jumla ya wananchi 48 wamepata mikopo kutoka vyombo mbalimbali vya fedha ikiwemo Mfuko wa Pembejeo waombaji 9, NMB 23, CRDB 7 na SIDO 9.

Akifafanua zaidi amesema kasi ya utoaji Hati hizo imeongezeka baada ya kuanza kutumia tekinolojia ya mfumo wa Kompyuta wa Kijiografia (GIS) na hivyo kufanya utekelezaji wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999.

Zoezi hilo limekwenda sanjali na ujenzi wa masjala 9 za vijiji katika vijiji vya Halungu, Ipunga, Igamba, Mponela, Sakamwela, Bara, Ivwanga, Mbozi, Hatelele na Nambinzo.

Aidha ameeleza kuwa kumekuwepo na uelewa mkubwa miongoni mwa wananchi juu ya thamani ya ardhi wanayomiliki, migogoro ya ardhi imepungua na wananchi wamekuwa na ari ya kuwekeza kwenye ardhi yao.

Halmashauri ya Mbozi ambayo ni wilaya ya mfano katika zoezi la utoaji hakimiliki nchini imepata mafanikio yaliofanya wilaya nyingine zije kujifunza ambazo ni Simanjiro, babati, Kilosa, Kigoma, Mbinga, Makete, Kyela, Rungwe, Arusha, Mtwara, Njombe na wanafunzi toka UCLAS.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text