Saturday, September 6, 2008

HUU NI UCHAWI, USHIRIKINA AU ?

Posted by Unknown On 10:18 AM No comments
Na Kenneth Mwazembe
Mbozi

Mtoto mmoja Isah Hassan Mkoka (14) mwanafunzi wa wa darasa la nne katika shule ya msingi ya Mkwajuni jijini Dar es salaam, juzi alipeperushwa kwa nguvu ya upepo umbali wa kilometa 1100 kutoka jijini na kutupwa katika kijiji cha Mpemba Wilayani Mbozi kwa muda wa masaa sita,
Maajabu hayo yalishuhudiwa na mamia ya wanachi wa kijiji hicho kilichopo umbali wa kilometa kumi kutoka mji mdogo wa Tunduma wilayani Mbozi ambao walidai kuwa mtoto huyo aliokotwa kijijini hapo Septemba 2 saa mbili usiku akiwa hajitambui na akahifadhiwa nyumbani kwa Rafael Kamendu mkazi kijijini hapo.
Kwa mujibu wa maelezo yake aliyoyatoa wakati akihojiwa na mwandishi wa habari hizi Isah alisema kuwa , tukio hilo lilimtokea Jumatatu Septemba mosi saa sita mchana mara baada ya kutoka shuleni akiwa chumbani katika nyumba yao iliyopo eneo la Kisiju Jijini Dar es salaam.
Alisema punde alipokuwa katika harakati za kubadili sare, alisikia sauti ya ngurumo ikiambatana na upepo mkali ambao ulimtoa nje na kuanza kumpeperusha angani kwa mtindo wa kudundadunda kama mpira ,huku akilia na kupiga kelele za kuomba msaada lakini hakufanikiwa .
“Nilimuona mwanamke mmoja nisiye mtambua akiwa katikati ya upepo huo akiwa amevaa kipande cha nguo nyeusi aina ya kaniki na shanga nyingi shingoni hakuwa tayari kutoa msaada na hata nilipo jaribu kumnyoshea kidole mkono wangu ulipinda” alisema.
Alisema baada ya juhudi hizo kushindwa polepole aliishiwa nguvu na kupoteza fahamu hadi alipo zinduka baada ya wananchi wasamaria wema walipo muokota jirani na mto Mpemba na kumtunza kwa jirani hadi siku iliyofuata alipopelekwa kituo cha polisi cha Tunduma.
Hata hivyo Isah amekutwa amevaa sare za shule ambazo hazina nembo, anapata maumivu makali ya tumbo wakati anapokula chakula, anajieleza kwa shida kidogo na anasema hajui wapi yupo lakini anadai kuwa wazazi wake wapo Kisiju hawafahamu kilicho mtokea.
Mwenyekiti wa kijiji hicho John Sinyinza alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na akatoa mwito kwa wananchi kuwafichua watu wanaotumia nguvu za kishirikina kuwachezea watoto ambao hawajui jambo lolote na kuwafanya wazazi wao na Taifa kwa ujumla kupata usumbufu usiokuwa wa lazima.
Mwisho

Na Kenneth Mwazembe
Mbozi

MWANAUME mmoja Giwelo Tuyonge (37) mkazi wa kitongoji cha Migombani mjini Tunduma wilayani Mbozi jana alikatwa na kuondolewa sehemu zake za siri kwa kinachoaminiwa kuwa ni imani za kishirikina.

Akiwa amelazwa katika hospitali ya mjini Vwawa Tuyonge anasema kuwa ilikuwa majira ya saa 10.00 usiku wa Septemba 5, akiwa amelala mtu mmoja raia wa Zambia alivunja mlango na kuingia ndani na kumshambulia kwa rungu la kichwa na alipomzidi nguvu alimkata nyeti zake na kisha kuondoka nazo.

Tuyonge ambaye ameishi kwa zaidi ya miaka kumi eneo hilo hujishughulisha na biashara ya kuuza mkaa anaobeba kwa baiskeli, na hakuwahi kuoa mke.

Tukio hilo ambalo limevuta hisia za wakazi wa mjini hapa limewapa hofu kwani ni la aina yake na ambalo limeongeza mashaka juu ya usalama wao, mauaji yamekuwa yakitokea mara kwa mara yahusuyo uporaji wa fedha na mali lakini siyo kunyofolewa viungo.

Mganga mmoja katika hospitali hiyo (jina lipo) ameeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa mtu aliyefanya kitendo hicho akawa ni mzoefu wa muda mrefu au anayo taaluma ya kiganga kwani ameondoa nyeti hizo kitaalam akiwa ameacha mishipa hatari bila kuigusa.

Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya Egifrid Mwingilihera amethibitisha kumpokea majeruhi huyo akiwa hana nyeti na kwamba atapelekwa katika hospitali ya Rufaa mjini Mbeya kwa matibabu zaidi.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Zerote Steven hakuweza kupatikana baada ya kuelezwa na Katibu Muhtasi wake kuwa yuko kwenye kikao.

Mwisho

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text