Tuesday, August 12, 2008

WANANCHI HATARINI KWA KULA SUMU

Posted by Unknown On 5:08 AM 1 comment
Na Kenneth Mwazembe
Mbozi

AFYA za wakazi wa wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya na Dar es Salaam zipo hatarini kufuatia kula vyakula vinavyohifadhiwa kwa sumu kali, imefahamika.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini maduka ya madawa katika miji ya Vwawa, Tunduma na Mlowo kuuza madawa ya kuhifadhia nafaka aina ya Actellic 50%ec yasiyothibitishwa na Taasisi ya Utafiti ya Arusha (TPRI) yakiwa pia yamehifadhiwa kwenye chupa zinazoonesha kutengenezwa na kampuni ya Sygenta Agro Services AG.

Mazao hayo yanayohifadhiwa kwa sumu kali husafirishwa hadi jijini Dar es Salaam ambako ndiyo kuna soko kuu la mahindi na maharage yanayozalishwa wilayani hapa japo wakati mwingine husafirishwa nje ya nchi yaani Zambia na Kongo.

Utambuzi wa chupa uliofanyika katika maduka mbalimbali katika miji hiyo ulibaini kutofautiana kwa alama chache za maandishi ukilinganisha na zile halisi pia rangi na harufu yake.

Madawa mengine yanayouzwa yakiwa ni bandia ni pamoja na Cuprocaffaro (Copper Oxychloride) Tancopa 50% WP na Round up, Gesaprim 500FW.

Uhifadhi nafaka wa hatari umetokana pia na baadhi ya wafanyabiashara wanaonunua mazao ya nafaka hasa mahindi na maharage ambao wanatumia madawa hatari ya kuua wadudu kama mchwa na vidomozi kupuliza mazao hayo kwa kuhifadhi ghalani.

Sumu zilizobainika kutumiwa kama mbadala wa Actellic ni Dusburn 50EC, Sumithion EC, na Thiodan 50EC ambazo hutumika kuua wadudu kama vidomozi (leaf miner), vidugamba (scales), buu wa shina (stem borer), mchwa na wadudu wengine.

“Kaka huwezi kununua Actellic shilingi 30,000/= kwa lita badala ya 12,000 kwa lita ya Dursban itakayotunza mahindi gunia 100 utakuwa unafanya biashara kichaa” alisema mfanyabiashara mmoja ambaye aliomba jina lake lisitajwe.

Baadhi ya wenye maduka walipohojiwa juu ya tuhuma za kuuza madawa bandia walikiri kuwepo kwa madawa hayo na kwamba husambazwa na vijana wasio waaminifu ambao huyaleta toka Malawi na Msumbiji na mengine yanatengenezwa kwenye viwanda bubu ambavyo vinaaminika kuwepo Uyole kwenye jiji la Mbeya.

“Ni watu wachache wacha Mungu ndiyo wanaweza kukubali kuingia hasara baada ya kuona wameuziwa madawa badnia wanaoweza kuyatupa na kukubali hasara, wengi wanaamua kuuza hadi yaishe ili kurudisha fedha zao” aliongeza mmoja wao.

Afisa Maendeleo ya Kilimo wilayani hapa Nason Kigobanya alipohojiwa juu ya kuwepo madawa madukani yasiyostahili na matumizi ya sumu kali kuhifadhia nafaka alithibitisha kuwepo kwa wafanya biashara wasiowaaminifu na kwamba kwa taarifa hizi atafuatilia na kuchukua hatua.

“Uelewa mdogo juu ya madawa ndiyo sababu kubwa inayowafanya wananchi kununua madawa hayo au pengine bei ndogo inawafanya wanunue dawa zisizofaa” aliongeza.

Afisa wa Afya wilayani hapa Eddo Kyara alipohojiwa juu ya watu wanaoathirika kwa matumizi ya madawa hayo aliahidi kufatilia kwa karibu na kwamba atachunguza ili kubaini wafanyabiashara wanaouza madawa bandia kwa hatua zaidi.

Naye Afisa Biashara wilayani hapa Salehe Ibrahim alipohojiwa juu ya wafanyabiashara kuuza madawa yasiyothibitishwa na TPRI alisema Bodi ya Madawa na Chakula (TDFA) ndiyo wahusika wakubwa na kwamba atawasiliana nao ili waweze kushughulikia mapema iwezekanavyo.

Msambazaji mkuu wa sumu iliyobainika kuwa bandia kampuni ya Mukpardar alipohojiwa kwa simu mtu aliyejitambulisha kwa jina moja la Ketan (Muasia) alijibu kuwa kuna watu Kariakoo wanaotengeneza dawa hizo na kuweka nembo yao ya Mukpardar na kwamba wao hawahusiki kutengeneza hizo dawa zinazodaiwa bandia.

Maelezo zaidi aliyatoa Abduli Razak mfanyakazi dukani hapo ambapo alifafanua kuwa wao wanashindwa kuthibiti utengenezaji huo bandia kwa kuwa kazi hizo zinafanywa na wahuni wa Kariakoo na kwamba wanaiga kila kitu hata wao wanashindwa kubaini bandia na halisi ni ipi.

Hata hivyo kuna kila sababu Wizara ya Afya kutuma wataalam wake ili kufanya uchunguzi kwa miili ya wakazi wa wilayani hapa ili kubaini ni kwa kiwango gain wameathirika na madawa hayo

MWISHO

MAALBINO WAPEWA TSH 1.9 MILIONI

Na: Kenneth Mwazembe – Mbozi

Wahisani mbalimbali wametoa jumla ya sh. Mil.1.9, ikiwa ni msaada kwa chama cha maalbino mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kuendesha semina na mikutano elekezi kwa lengo la kuielimisha jamii kutambua albino kuwa ni sehemu ya jamii yenye ulemavu wa ngozi.

Kiasi hicho cha fedha kilitajwa juzi na Mwenyekiti wa chama hicho Mathayo Mwantemani alipokuwa anahubiri katika ibada iliyoandaliwa maalumu kwa ajili ya kukabidhi msaada huo iliyofanyika katika Kanisa la Moravian Mbozi Mission wilayani Mbozi.

Alieleza kuridhishwa kwake na jinsi jamii ya watanzania walivyoitikia wito wa kuwasaidia ili kuwaokoa albino kwa kuwachangia kiasi hicho cha fedha ambacho kitasaidia kutoa elimu kwa jamii juu ya imani potofu ya kuwaua kwa madai kuwa viungo vyao vinaweza kusaidia kupata utajili.

Mwantemani aliwataja waliochangia kiasi hicho cha fedha kuwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya ambaye ametoa sh. 931,000/=, Benki Kuu sh. Milioni moja na waumini wa kanisa la Moraviani ambao walitoa sh. 33,000/= ikiwa ni mchango wa papo kwa papo katika ibada hiyo.

Mwenyekiti huyo ameitaka jamii kuelewa kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Maalbino) hawakutokana na kasoro za wazazi wao au wazazi kula vyakula ambavyo havitakiwi wakati wa ujauzito bali ni majaaliwa ya Mwenyezi Mungu kwani hakuna anayependa kuzaa vilema na kwamba mtu mwenye mawazo hayo asije akashangaa Mungu anampa albino kwenye ndoa yake.

Alifafanua kuwa mtu mwenye ulemavu wa ngozi (albino) anazaliwa na ngozi nyeupe kutokana na upungufu wa chembe hai aina ya melanin, mtu akiwa na melanin ya kutosha anazaliwa akiwa na ngozi nyeupe ambapo kazi kubwa ya chembe hizo ni kuzuia mionzi ya jua kuharibu ngozi ya binadamu.

Katibu wa Chama hicho mkoa wa Mbeya Sydney Mwamlima alieleza kuwa albino ni sawa na mtu mwingine wa kawaida na ana uwezo sawa na wengine, lakini anakabiliwa na tatizo namna ya kujilinda na mionzi ya jua ambayo ina sumu inayochoma ngozi na kuwa nyekundu inayosababisha vidonda ambavyo hugeuka kuwa kansa ya ngozi.

Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwepo kwa mila potofu ambazo zinawafanya wakunga wa jadi kuwaua watoto wanaozaliwa na ulemavu wa viungo wakiwemo maalbino kabla hawajatolewa nje (wenyeji huita Mushiyumba) ambapo mtoto hutolewa rasmi.

MWISHO.

1 comment:

  1. Hello from Canada - many years ago, 1980 I think, a Tanzanian named Nason Kigobanya worked on my husband's farm in Saskatchewan for the summer. My husband's name is Cyril Laforge and Nason worked also with Martin Laforge. I am coming to Tanzania in a couple of weeks and I would like to meet him if possible. I see that you mention him in your blog but I don't read Swahili and don't understand it. Anyway, if you have any way of contacting him ask him to e-mail me at cgerwing@gmail.com or claforge@hotmail.com.

    ReplyDelete

Thank you for reading the article

Site search

    More Text