Monday, August 11, 2008

Wananchi wagomea ukarabati zahanati

Posted by Unknown On 7:16 AM No comments
Na Kenneth Mwazembe, Mbozi

WANANCHI wa Kijiji cha Mpemba, wilayani Mbozi, Mbeya, wamekataa mpango wa serikali wa kukarabati zahanati ya kijiji hicho na badala yake wanataka jengo hilo lijengwe upya.

Hali hiyo ilibainika juzi wakati mkandarasi alipopelekwa kijijini hapo, ili kuweka sahihi mkataba huo wa ukarabati ambapo wananchi kwa pamoja walikataa na kuomba fedha iliyotolewa milioni 14 zitumike kujenga jengo jipya.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, John Sinyinza, alisema jengo hilo lilijengwa kwa udongo na limeliwa na mchwa na hivyo kufanya ukarabati kuwa mgumu kwa kuwa limeoza na kwamba hakuna maana kukarabati.

Alisema kijiji hicho chenye wakazi 10,000 kinahitaji kuwa na huduma ya afya ya uhakika na kwamba wao kama wananchi wameshaanza kukusanya mawe kwa ujenzi wa kituo cha afya na si zahanati.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Julius Kamwela, alisema wananchi kupitia mkutano mkuu wa kijiji wamekataa ukarabati huo na kwamba wamepeleka miniti za mkutano kwa mkurugenzi wakipinga ujenzi na kudai ujenzi mpya.

Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God, Justus Sinkonde, alidai kutokana na kijiji hicho kuwa kiungo kati ya Zambia na Malawi idadi ya wakazi inaongezeka kwa kasi na hivyo kuona haja ya serikali kujenga kituo cha afya badala ya zahanati.

Wananchi kwa nyakati mbalimbali waliiambia Tanzania Daima kuwa sh milioni 14 zilizotengwa zikiongezwa na nguvu za wananchi zitaweza kukamilisha ujenzi wa zahanati mpya na kwamba kama serikali itawaunga mkono basi watajenga kituo cha afya.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya, Egifrid Mwingilihela, alithibitisha kuwapo mgomo huo na kwamba atafanya mazungumzo na uongozi wa kijiji, ili kupata ufumbuzi.

Hata hivyo, aliulaumu uongozi wa kijiji ambao ulikaa kimya wakati wa kufanya tathmini na walisaini makubaliano ya ukarabati na si kujenga upya.

Aliongeza kuwa iwapo hawatakuwa tayari kukubali ukarabati idara yake itahamisha mradi huo, kwani unatakiwa kwisha haraka.

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text