Friday, August 1, 2008

DARAJA LA LUASHO - MTO MOMBA

Posted by Unknown On 6:06 AM No comments
Daraja hilo lipo Mto Momba wilayani Mbozi, mto wenye mamba wengi, mamba hao ni tishio kwa usalama wa binadamu. yamekuwa yakiripotiwa matukio kadha wa kadha kuhusiana na mamba hao. Juzi mtoto Lucia Osward (9/12) aliliwa na mamba na mama Bahati Kawepa (28) akiokolewa akiachwa na majeraha makubwa ambayo nusura apoteze nyeti zake.

Kama si ujasiri wa mume wake mama huyo aliyefika na kutoa msaada kwa kuingiza mkono kinywani mwa mamba na kumshika ulimi huku akisaidiwa na mwanamke mwingine aliyevuta mkia na kujitahidi kumkokota nje ya maji mamba huyo leo ingekuwa habari nyingine.

MTOTO AKATISHWA MASOMO ILI AOLEWE, BABA YAKE AKAMATWA NA KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Na Kenneth Mwazembe
Mbozi
Licha ya jitihada za serikali kutimiza malengo ya pili ya Milenia ya kutoa elimu ya msingi kwa watoto wote kuna baadhi ya wazazi waliojitokeza kuwa kikwazo cha malengo hayo kwa tamaa ya kujipatia mali kwa kuwaoza wasichana.
Giveness Edward (19) mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Hangomba wilayani Mbozi mkoani Mbeya amekatishwa masomo na baba yake na kutakiwa aolewe.
Mkasa wa kusikitisha unaomhusu mtoto huyo ulianza mapema mwaka huu ambapo baba yake alitofautiana na binti yake huyo baada ya mzazi huyo kumkataza kuabudu kwa madai kuwa imani ya Kikristo aliyonayo binti huyo imemfanya asimsikilize baba yake ambaye alimtaka kuolewa.
Giveness akizungumza na mwandishi wa habari hizi amesema kuwa baba yake Edward Kamgodi Mwapule alimkatisha masomo pale alipomkamata na kumfunga kamba kisha kumpeleka kwa mganga wa kienyeji ili kumnywesha dawa ambazo zingemfanya mtoto kumtii baba yake kwa kila alitakalo.
Kabla ya tukio hilo baba yake alimpiga mtoto huyo kwa mpini wa shoka na kumsababishia maumivu ya miguu ambapo mtoto alilazimika kupata PF 3 ya polisi na kutibiwa katika zahanati ya Itaka.
Kipigo hicho kilimfanya Afisa Mtendaji wa kata ya Itaka Lukosomolo Ndimbwa kumshikilia kwa muda mzazi huyo asiye huruma na ambaye anathamini ng’ombe kuliko elimu hadi mtoto alipopona.
Hata hivyo Giveness anasema kuwa hatua ya serikali kumshikilia baba yake kwa kosa hilo baba yake aliapa kumuua kisha naye kujiua, ndipo alipolazimika kukimbilia nyumbani kwa mwenyekiti wa kijiji Askofu Mbazu ambaye alimpokea na kumhifadhi na kuruhusu mtoto huyo kuendelea na masomo akitokea nyumbani kwa mwenyekiti huyo.
Hali ilibadilika usiku wa 27 Mei mwaka huu mwenyekiti alipokula njama na mzazi wa Giveness, ambapo usiku majira ya saa 9 baba huyo akiongozana na watoto wake wawili Shida Edward na Mashaka Mwampashe walifika nyumbani kwa mwenyekiti na kubisha hodi, mwenyekiti alifungua mlango na kusaidia kumfunga mtoto huyo mikono kwa kamba na kisha kuondoka naye hadi kijiji cha Wasa kwa mganga wa kienyeji aitwae Chilaka umbali wa kilometa 40 ili kumnywesha dawa za kuondoa imani ya kikristo na kumpandikiza uchawi.
Kwa nasibu Mungu alimnusuru binti huyo ambaye anaeleza kuwa mara baada ya kufika kwa mganga huyo walikaribishwa kula chakula, yeye alizuiwa kula hadi atakaponyweshwa dawa hizo, hali iliyomfanya binti huyo kuomba aoneshwe msalani na kutumia mwanya huo kutoroka na kukimbia hadi kijiji cha pili ambako alipata msaada wa kuoneshwa njia ya kwenda mjini Vwawa ambako pia Wasamaria walimsaidia usafiri hadi Mbeya mjini.
Mtoto huyo ambaye hadi sasa anahifadhiwa na wasamaria amefikishwa katika kituo cha polisi mjini Vwawa ambao wamechukua hatua za kuwatafuta watuhumiwa wote wanne ili kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili za unyanyasaji na kumzuia masomo.
Kaimu Afisa Elimu wilayani hapa Juma Kitabuge alieleza masikitiko yake kwa mkasa uliompata binti huyo na kueleza kuwa hali hiyo inaweza kumwathiri kimasomo, akaahidi kumsaidia kuhakikisha anaendelea kusoma katika shule jirani ambapo ataendelea kulelewa na wafadhili hadi atakapofanya mtihani miezi michache ijayo.
Jeshi la Polisi wilayani hapa limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari limeshamkamata baba yake binti huyo na kwamba atafikishwa mahakamani wakati wowote.
Mwisho


MENEJA WA PENTAGON SECURITY AFUNGIWA NDANI YA OFISI

Walinzi wa kike wa kampuni ya Pentagon Security Guards inayofanya kazi ya ulinzi wilayani Mbozi mkoani Mbeya jana waliwafungia mameneja wao ofisini baada ya wakubwa hao kukataa kuwalipa mishahara yao .

Hatua hiyo ilichukuliwa na walinzi wawili Maria Sinyinza na Lucy Nashiuya ambao waliwafungia ndani ya ofisi Meneja wa Tawi la Mbeya Charles Makwaza na Meneja wa Kituo cha Mbozi Lt. Mstaafu Mwaijibe wakishinikiza kulipwa mishahara yao baada ya mkataba wa ulinzi baina ya kampuni hiyo na kampuni ya China Road & Bridge kumalizika.

Awali kabla ya tukio hilo Makwaza alilipwa mishahara hiyo na kampuni ya Kichina ambapo walinzi hao walimdai awalipe mishahara hiyo kabla hajaondoka kurudi mjini Mbeya, meneja huyo alikataa ombi hilo na kuwaeleza kuwa hamlipi mtu kwa kuwa mkataba umekwisha na kwamba wao kama walinzi wameajiriwa moja kwa moja na kampuni ya kichina hivyo haoni sababu ya kulipa fedha hizo.

Hata hivyo meneja huyo alilazimika kuvunja dirisha la ofisi hiyo na kutoroka bila kuwalipa fedha hizo.

Maria Sinyinza alieleza kuwa wao wanadai haki yao waliyofanya kazi kabla hawajaajiriwa na CRBC na kwamba wamechukua hatua hiyo kwa kuwa meneja huyo amekuwa anawanyanyasa kwa kuwakata mishahara yao kwa visingizio visivyoeleweka na kwamba yeye anadai jumla ya shilingi 70,000 ikiwa ni mshahara wa miezi mitatu.

Meneja wa tawi alipotakiwa kueleza tukio hilo alithibitisha kuwa yeye na bosi wake walifungiwa ndani ya ofisi ambapo bosi wake alilazimika kutumia mbinu za medani kwa kuvunja dirisha na kutoroka kupitia dirisha hilo.

Alipohojiwa kwa simu juu ya tuhuma za kudhulumu wafanyakazi hao mishahara, Meneja wa Tawi Charles Makwaza alikiri kufungiwa na kwamba kwake hayo ni matukio ya kawaida na kwamba fedha wanazodai siyo nyingi haziwezi kuwaathiri.

Uchunguzi umebaini kuwepo ka malalamiko ya walinzi juu ya kukatwa fedha kwa visingizio mbalimbali ikiwemo kupotea kwa baadhi ya mali katika malindo yao na kwamba vitendo vya wizi vinavyofanywa na baadhi ya walinzi wasio waaminifu vinatokana na malipo duni wanayolipwa na waajiri wao.

Aidha malalamiko ya wafanyakazi hao yamebainisha kuwa wamekuwa wanalipwa shilingi 10,000 kwa mwezi baada ya kukatwa sh 30,000 hali inayowafanya walinzi waishi maisha magumu.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text