Wednesday, June 25, 2008

UKATILI DHIDI YA WATOTO

Posted by Unknown On 1:13 AM No comments

Na Kenneth Mwazembe

Mbozi.

PAMOJA na jitihada zinazofanywa na serikali kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu, hali ni tofauti kwa Giveness Edward (19) mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Hangomba wilayani Mbozi mkoani Mbeya ambaye amekatishwa masomo na baba yake na kutakiwa aolewe.

Mkasa wa kusikitisha unaomhusu mtoto huyo ulianza mapema mwaka huu ambapo baba yake alitofautiana na binti yake huyo kutokana na imani ya Kikristo ya madhehebu ya Kimoravian ambapo baba mtu alimkataza kuabudu kwa madai kuwa imani hiyo imemfanya asimsikilize baba yake ambaye alimtaka kuolewa.

Giveness akizungumza na mwandishi wa habari hizi amesema kuwa baba yake Edward Kamgodi akishirikiana na kaka zake wawili Shida Edward na Mashaka Mwampashe walimpiga kwa mpini na kumsababishia maumivu ya miguu ambapo mtoto alilazimika kupata PF 3 ya polisi na kutibiwa katika zahanati ya Itaka.

Kipigo hicho kilimfanya Afisa Mtendaji wa kata ya Itaka Lukosomolo Ndimbwa kumshikilia kwa muda mzazi huyo asiye huruma na ambaye anathamini ng’ombe kuliko elimu hadi mtoto alipopona.

Hata hivyo Giveness anasema kuwa hatua ya serikali kushikilia baba yake kwa kosa hilo baba yake aliapa kumuua kisha naye kujiua, ndipo alipolazimika kukimbilia nyumbani kwa mwenyekiti wa kijiji Askofu Mbazu ambaye alimpokea na kumhifadhi na kuruhusu mtoto huyo kuendelea na masomo akitokea nyumbani kwa mwenyekiti huyo.

Hali ilibadilika usiku wa 27 Mei mwaka huu ambapo mwenyekiti alikula njama na mzazi wa Giveness ambapo usiku majira ya saa 9 baba huyo akiongozana na watoto wake wawili alifika na kubisha hodi ambapo mwenyekiti alifungua mlango na kusaidia kumfunga mtoto huyo mikono kwa kamba na kisha kuondoka naye hadi kijiji cha Wasa kwa mganga wa kienyeji aitwae Chilaka umbali wa kilometa 40 ili kumnywesha dawa za kuondoa imani ya kikristo na kumpandikiza uchawi.

Kwa nasibu Mungu alimnusuru binti huyo ambapo anaeleza kuwa mara baada ya kufika kwa mganga huyo walikaribishwa kula chakula ambapo yeye alizuiwa kula hadi atakaponyweshwa dawa hizo, hali iliyomfanya binti huyo kuomba aoneshwe msalani na kutumia mwanya huo kutoroka na kukimbia hadi kijiji cha pili ambako alipata msaada wa kuoneshwa njia ya kwenda mjini Vwawa ambako pia Wasamaria walimsaidia usafiri hadi Mbeya mjini.

Akisimulia zaidi binti huyo anabainisha sababu kubwa ya kuhitirafiana na baba yake kuwa ni pale alipokataa kupewa uchawi. “Nilipewa hirizi niliyokuwa navaa nikienda shuleni, hirizi hiyo ilikuwa na madhara kwa wanafunzi wenzangu, kwani siku nikivaa wanafunzi wengine walikuwa wanajisikia vibaya hali iliyowafanya wasielewe masomo hayo” alisimulia.

“ Nilivaa hirizi hiyo bila kuwa na amani moyoni na hasa pale nilipoona wanafunzi wenzangu wanahangaika ndipo nilipolazimika kumwendea mwalimu Kyomo ambaye alinishauri kuichoma moto hirizi hiyo ambayo hata baada ya kujaribu kuichoma haikuungua ndipo nilipoitupa chooni na hapo nikawa nimewasha moto na baba” anaongezea Giveness.

Mambo mengine anayosimulia binti huyo ni pale baba yake alipoongozana naye kwa mganga mmoja jirani yao ambapo alishuhudia ndege mkubwa jamii ya mwewe akitua mtini juu ya kilima na baadaye kuonekana binadamu mwenye mkoba aliyefika hapo huku akiwa na wasiwasi wa kuonwa alipokuwa akijigeuza kutoka umbile la ndege na kuwa binadamu na kisha kutoa hizo dawa zilizofanyiza hirizi hiyo.

Mtoto huyo ambaye hadi sasa anahifadhiwa na wasamaria amefikishwa katika kituo cha polisi mjini Vwawa ambao wamechukua hatua za kuwakamata watuhumiwa wote wanne ili kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili za unyanyasaji na kumzuia masomo.

Kaimu Afisa Elimu wilayani hapa Juma Kitabuge alieleza masikitiko yake kwa mkasa uliompata binti huyo na kueleza kuwa hali hiyo inaweza kumwathiri kimasomo, akaahidi kumsaidia kuhakikisha anaendelea kusoma katika shule jirani ambapo ataendelea kulelewa na wafadhili hadi atakapofanya mtihani miezi michache ijayo.

Jeshi la Polisi wilayani hapa limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba linaendelea na uchunguzi wa kisa hicho.

Mwisho

Friday, June 13, 2008

WANANCHI KUNUFAIKA NA HAKIMILIKI

Posted by Unknown On 2:07 AM No comments
Na Kenneth Mwazembe
Mbozi.

WANANCHI wilayani Mbozi wameanza kunufaika na hakimiliki za kimila baada ya mabenki na asasi nyingine za fedha kuzitambua na kuzikubali kwa dhamana ya mikopo, imeelezwa.

Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Levison Chilewa katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Amesema hadi Juni 11 mwaka huu jumla ya Hatimiliki za kimila 2314 zimesajiliwa na jumla ya wananchi 48 wamepata mikopo kutoka vyombo mbalimbali vya fedha ikiwemo Mfuko wa Pembejeo waombaji 9, NMB 23, CRDB 7 na SIDO 9.

Akifafanua zaidi amesema kasi ya utoaji Hati hizo imeongezeka baada ya kuanza kutumia tekinolojia ya mfumo wa Kompyuta wa Kijiografia (GIS) na hivyo kufanya utekelezaji wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999.

Zoezi hilo limekwenda sanjali na ujenzi wa masjala 9 za vijiji katika vijiji vya Halungu, Ipunga, Igamba, Mponela, Sakamwela, Bara, Ivwanga, Mbozi, Hatelele na Nambinzo.

Aidha ameeleza kuwa kumekuwepo na uelewa mkubwa miongoni mwa wananchi juu ya thamani ya ardhi wanayomiliki, migogoro ya ardhi imepungua na wananchi wamekuwa na ari ya kuwekeza kwenye ardhi yao.

Halmashauri ya Mbozi ambayo ni wilaya ya mfano katika zoezi la utoaji hakimiliki nchini imepata mafanikio yaliofanya wilaya nyingine zije kujifunza ambazo ni Simanjiro, babati, Kilosa, Kigoma, Mbinga, Makete, Kyela, Rungwe, Arusha, Mtwara, Njombe na wanafunzi toka UCLAS.

MWISHO

Thursday, June 5, 2008

Na Kenneth Mwazembe
Mbozi

Chama cha Mapinduzi wilayani Mbozi mkoani Mbeya kimetoa sh 50 elfu na salaam za pole kwa wachezaji wa timu ya mpira ya Chipaka Rangers ya mjini Tunduma kufuatia ajali iliyotokea jana katika eneo la Tunduma iliyojeruhi watu 16.

Katibu wa CCM wilaya ya Mbozi Aluu Segamba aliyefika katika hospitali ya wilaya kuwaona majeruhi, ameeleza kusikitishwa kwake na ajali hiyo ambayo imewafanya baadhi ya wachezaji kuvunjika viungo vyao na kwamba chama kipo pamoja nao katika wakati huu mgumu wa kuuguza majeraha.

Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya Egifrid Mwingirihela amewataja majeruhi 10 ambao wamepelekwa hospitali ya rufaa kutokana na hali zao kuwa mbaya ni Manase Siwelwe, Joseph Simumba, Rogers Siwale, Sultan Simumba, Jacob Sikaonga, Yona Sikanyika, Leonard Sinkala, Ruben Sinkala, John Siwale, na Aron Sikaonga

Wengine ni Alick Siame, Timoth Siame, Paulo Siwelwe, Izukanji Sikaonga, Antony Simwinga na Imasi Silungwe ambao ameeleza kuwa hali zao zinaendelea vizuri na wanapata matibabu katika hospitali yake.

Akisimulia ajali ilivyotokea, majeruhi Alick Siame (48) anasema kuwa dreva aliyekuwa anaendesha gari Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T160 ARG (Jina la dreva halikupatikana) kuwa alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi hali iliyomfanya ashindwe kulidhibiti na kupinduka.

Gari hilo lilibeba wachezaji na washabiki wa mpira waliotoka kucheza mechi mjini Tunduma wakirejea kijiji cha Chipaka ambapo gari liliacha njia na kupinduka.

MWISHO

Site search

    More Text