Friday, February 6, 2009

MTOTO ERICA APATA MSAADA

Posted by Unknown On 8:35 AM No comments
Watanzania wawili wanawake wanaoishi Marekani wametoa msaada wa dola 200 za Marekani kugharamia matibabu ya mtoto Erica Laurent (1) aliyekataliwa na baba yake baada ya kuzaliwa bila njia ya haja kubwa.

Wanawake hao Elizabeth Sawe wa Dallas na Joyce Joseph wa California waliamua kumsaidia mtoto huyo baada ya kusoma habari za Erica na kuona picha yake katika blogu ya http://www.maishanivita.blogspot.com/ ambayo ilimuonesha mtoto huyo akiishi matumbo yakiwa nje.

Mtoto huyo aliyezaliwa Novemba 2007 na Huruma Mwaijande akiwa na tatizo la kutokuwa na njia ya haja kubwa alikuwa akitibiwa katika hospitali ya rufaa mjini Mbeya ambapo walimfanyia upasuaji wa awali uliosababisha eneo la kitovu alipopasuliwa kufumuka mara baada ya ushonaji hali iliyowalazimu waganga hao kumshauri mama wa mtoto kuendelea kumlea hadi atakapofikia umri wa mwaka mmoja ndipo upasuaji ufanyike.

Kutokana na hali ya umaskini wa kutisha unaoikabili familia hiyo mume aliamua kumtekelekeza mkewe na kumwacha akihangaika ambapo alilazimika kuomba msaada wa wasamaria.

Wasamaria hao katika ujumbe wao wamesema kuwa haja yao ni mtoto Erica kupewa matibabu yanayostahili na kukua kama watoto wengine.

Wametoa wito pia kwa Watanzania wengine kuwasaidia wenye shida kama mtoto huyo “Tunaomba watu wawe na huruma na moyo wa kusaidiana kwani ukimsaidia mtoto kama Erica ambaye ni malaika unakuwa umejiwekea hazina mbinguni, Erica ni malaika ambaye hajui kitu duniani” ilisema sehemu ya ujumbe huo.

Hivi sasa mtoto huyo yuko katika hospitali ya Peramiho ambapo anatarajiwa kufanyiwa upasuaji Februari 9 mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text