Friday, February 6, 2009

Na Kenneth Mwazembe
Mbozi.

Wananchi 95 wakazi wa kijiji cha Nambala Wilayani Mbozi mkoani Mbeya juzi waliandamana hadi kituo kikuu cha Polisi kulishinikiza Jeshi la Polisi Wilayani hapa kuwaachia huru wana kijiji wenzao wanne waliowekwa mahabusu na jeshi hilo.

Jeshi hilo liliwakamata watuhumiwa hao kwa kosa la kupekua nyumba ya Penson Nkoswe na kubomoa nyumba za wanakijiji wenzao kinyume cha sheria.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Jumanne Mziho aliwataja watu waliokamatwa na ambao wamekuja kudai waachiwe kuwa ni Moses Nzunda (36), Julius Mwashilindi (51), Wadi Mwashilindi (42) na Tomaso Nzunda (30) ambao wanatarajiwa kupandishwa kizimbani kujibu tuhuma hizo.

Mziho aliongoza maandamano hayo hadi kumwona Kamanda wa Polisi wilayani hapa ambaye alitumia busara kumaliza mgogoro huo baada ya kuwasikiliza na kufanya mazungumzo baina yake na viongozi wa kijiji na kata yaliyofanya polisi kusalimu amri na kuwaachia kwa dhamana.

“Sisi tumekuja kudai haki na kutaka kufahamishwa kama Jeshi letu limeacha mpango wa Ulinzi Shirikishi na badala yake kuzitumia taarifa za watu wenye chuki dhidi ya mpango huo, na kuwatia nguvuni wananchi wasio kuwa na hatia” alisema mwenyekiti.

Alisema tatizo lililopo kijijini kwake ni la mwanakijiji Penson Nkoswe ambaye amekuwa akipinga juhudi zinazo fanywa na kijiji hicho za kuimarisha ulinzi na usalama dhidi ya wahalifu sugu ambao wamekuwa wakijificha na kulindwa na Nkoswe.

Naye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi wa kijiji hicho Tadeo Nzunda alibainisha kwa kuwa taja wahalifu wanaolindwa na Nkoswe kuwa ni Luka Mgode (31), Jelas Sampamba (29) na Mpandachilima Mwasaka (22) ambao hujihusisha na mtandao wa wizi wa mifugo, baiskeli, redio na Tv.

Nzunda alisema Januari 27, mwaka huu watuhumiwa waliiba ng’ombe mmoja wa Wilson Shombe (56), na wengine wawili mali ya Ibrahim Chelelo na Beledon Nzyela ambapo wanakijiji walipofanya msako walimkamata Luka Mgode nyumbani kwa Nkoswe akiwa na ng’ombe mmoja na wenzake walifaulu kutoroka.

“Kitendo hicho kilipandisha jazba kwa wanakijiji ambao kwa idhini ya mkuu wa kituo cha Polisi kilichojirani mjini Mlowo, alitoa idhini kufamya upekuzi na kuwasaka wahalifu katika nyumba ya Nkoswe wakati baadhi yao wakiwa na hasira kali walivamia nyumba za washukiwa na kuziharibu nyumba zao” alisema.

Hata hivyo watuhumiwa waliokuwa rumande waliachiwa kwa masharti ambayo hayakuweza kufahamika maramoja jambo ambalo liliwafanya wenzao waliokuwa nje kidogo ya eneo la Polisi kuanza kuimba nyimbo za kuashiria ushindi dhidi ya kitendo hicho.

Nkoswe alipotakiwa kujibu tuhuma zilizoelekezwa dhidi yake alikanusha na kudai kuwa hahusiki na lolote ingawaje alikubali kuwa na mahusiano ya karibu na Sampamba ambaye alimtetea kuwa ni mtu mwema.

Mwanakijiji Menard Msongole ameeleza kuwa nyumba moja mali ya Leward Nzunda imechomwa moto na watu wasiofahamika tukio linaloleta wasiwasi kuwa linahusishwa na uhasama uliojitokeza kati ya wanakijiji wema na wanaotuhumiwa wa uhalifu kijijini hapo.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya Zerothe Stephen alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo kwa njia ya simu kutoka Mbozi alisema bado hajapokea taarifa kutoka eneo la tukio hilo.

Uchunguzi zaidi umebaini kuwepo kwa kukamiana hali itakayohatarisha amani kutokana na walifu kulipiza kisasi kwa kuchoma nyumba huku wanakijiji wema wakidai kuwa watachukua hatua mikononi mwao mara watakapowatia mikononi mwao kwani wamechoshwa na vitendo hivyo.

Jeshi la polisi mkoani hapa litahitaji kuchukua hatua za tahadhari kabla hali haijawa mbaya kwani wananchi wana wasiwasi na jeshi hilo kutokuwa serious.
mwisho

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text