Saturday, February 28, 2009

Na Kenneth Mwazembe
Tunduma

Kundi la vijana wenye hasira kali zilizochochewa na mkuu wa kituo cha polisi mjini Tunduma A.S. Wendo wamevamia nyumba ya diwani wa kata ya Tunduma na ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Aden Mwakyonde na kuvunja vioo 83 vya madirisha 14 na kuwajeruhi mgambo wanne.

Chanzo cha ghasia hizo ni kukamatwa kwa baiskeli za vijana hao zilizokuwa zikitumika kuvusha mahindi na mchele mpakani mwa Tanzania na Zambia kwa madai kuwa ni operesheni usafi wa mji.

Vijana hao wamesema kuwa polisi walianza ukamataji wa baiskeli hizo usiku wa Februari 26 na kuendelea 27 ambapo vijana hao wamedai kuwa wamedaiwa fedha (RUSHWA) ili kukomboa baiskeli hizo.

Katika kukabiliana na kitendo hicho ambacho wamekiita unyanyasaji unaofanywa na jeshi hilo vijana hao waliandamana kuelekea kituo cha polisi ili kuishinikiza polisi kuwarejeshea baiskeli zao ambapo mkuu wa kituo aliwaambia waende kuchukua baiskeli hizo kwa diwani wao.

Kauli hiyo ndiyo iliyowafanya wao kurusha mawe kituoni hapo na baadaye kwenda nyumbani kwa diwani wao na kuharibu madirisha yote na kuipiga mawe nyumba hiyo.

Akizungumza na gazeti hili Aden Mwakyonde alieleza kuwa alipigiwa simu na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi shirikishi ya mjini hapa kuwa kuna maandamano makubwa ya vijana wenye hasira wakienda nyumbani kwake hali iliyomfanya awapigie askari polisi.

“Nimepiga simu kwa OCS ili atume askari kuzuia madhara ambayo yangeweza kutokea lakini hakufanya hivyo, alidai hana gari, mke wangu amempelekea magari mawili akadai hawawezi kutumia salon wanataka gari la wazi hata alipopelekewa gari la wazi akasema ni chakavu kasha akaondoka kwenda mjini Vwawa” alilalama Mwakyonde.

“Nimewaomba polisi wawape vijana hao baiskeli zao ili kuepusha shari ambayo ingeweza kutokea lakini polisi hawakufanya hivyo na hivyo kunisababishia hasara hii ”aliongeza Mwakyonde akielekeza lawama zote kwa jeshi la polisi.

Mwenyekiti huyo aliyekua akihudhuria kikao cha kamati ya uchumi na mipango alilazimika kuacha kikao na kukimbilia nyumbani kwake akiwabeba mkuu wa polisi wilayani hapa Stephen Mtengeth na timu yake lakini alipofika na kuona nyumba imeharibiwa aliwajia juu na kuwafukuza OCD na timu yake ya watu wane.

Hatua hiyo na ambayo imewaudhi polisi hao imelalamikiwa vikali kutolewa na kiongozi kama yeye wakidai angetumia busara.

Mkuu wa kituo cha polisi cha Tunduma aliyejitaja kwa jina moja la A. S. Wendo alipohojiwa juu ya yeye kuwa chanzo cha ghasia hizo alikanusha na kudai kuwa yeye amewatuliza wakakataa na hivyo kumfanya aende wilayani kuomba msaada wa askari wengine.

“Niliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kukinusuru kituo baada ya vijana hao kutaka kukivamia” anaongeza Wendo.

Mamlaka ya mji mdogo wa Tunduma inafanya operesheni ya kusafisha mji kwa kuondoa uchafu katika mifereji na vibanda vya wafanyabiashara ndogondogo ambayo ilianza juzi ikahamia na kukamata baiskeli hali iliyozusha machafuko yaliyosababisha wanamgambo wa halmashauri wane kujeruhiwa na mmoja kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbozi mjini Vwawa.

Mgambo waliojeruhiwa ni John Mwakalinga ambaye amelazwa katika hospitali ya Vwawa na Andrew Sing’ambi aliyetibiwa na kuondoka na wengine wawili ambao hawakuweza kupatikana majina yao .

Muuguzi katika wodi la majeruhi Ester Nyondo ameeleza kuwa hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri.

Hili ni tukio la tatu tangu mwaka 2006 ambapo ghasia za mpakani zilizuka kufuatia kifo cha Lukas Msuya kuuawa katika mahabusu za Zambia lile la mgomo wa mawakala wa usafirishaji (Clearing & Forwarding) ambapo katika ghasia hizo kulitokea uharibifu wa mali na majeruhi.

Mkuu wa wilaya ya Mbozi Halima Kihemba alipohojiwa juu ya matukio hayo alikiri kupewa taarifa muda mchache uliopita na kwamba kwa wakati huo alikuwa safarini Tukuyu kwenye kikao.

2 comments:

  1. hii ni style mpya ya kuwasilisha ujumbe. Alipigwa Raisi, akapigwa Raisi mstaafu, uvamizi wa vituo vya polisi nk. Na bilashaka inatokana na wananchi kuona kuwa kila wakisema kwa maneno hawasikilizwi. Lakini je, ni staili muafaka? Je, tutafika?

    nimepita kusabahi tu

    ReplyDelete
  2. Kama alivyosema Rama, yani ni jino kwa jino tu, sikio la kufa safari hii lazima lisikie dawa tu.

    ReplyDelete

Thank you for reading the article

Site search

    More Text