Tuesday, April 26, 2011

Wafanyabiashara mtatumaliza

MAUAJI yanayoambatana na imani za kishirikina yameibuka na kutia hofu wakazi wa kijiji cha Myunga wilayani hapa na kuwafanya washindwe kufanya kazi za uzalishaji mali.

Matukio yaliyozua hofu ni mauaji ya msichana ambaye hajatambuliwa aliyeuawa Aprili 20 na kutupwa katika mto Lwasho ambapo alikutwa na wavuvi ambao walitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji.

Baada ya uchunguzi maiti alibainika kutolewa ulimi, maziwa, meno na sehemu za siri hali iliyoamsha hasira za wananchi na wakawataka polisi kuondoka na mfanyabiashara Kasandilo Mteka ambaye walimtuhumu kuhusika na mauaji hayo.

Hata baada ya polisi kuondoka na mtuhumiwa huyo wananchi hao wenye hasira waliamua kuvunja nyumba ya mtuhumiwa ambapo walipekua na kuvikuta vitu vinavyodhaniwa kutumika katika kazi hizo za mauaji zikiwemo sindano mbili zilizodaiwa kuwa ni za BM.

Ambapo baada ya mahojiano mtuhumiwa alimtaja kamanda wa polisi mkoani Tanga kuwa ndiye mwenye vyombo hivyo.

Wananchi hao walimkamata mtuhumiwa mwingine Leonard Simfukwe na kumpiga hadi kumuua ambaye aliwataja watu wengine kumi wanaojihusisha na mauaji hayo wakiwemo wengine toka mkoani Rukwa na pia alielekeza kuwa kuna miili mingine mitano imefungwa mawe na kutumbukizwa mtoni ikiwa imenyofolewa baadhi ya viungo ambavyo vinauzwa nchini Zambia.

Katika operesheni hiyo alikamatwa mwingine aliyejulikana kwa jina la Tall Siwiti mkazi wa Miangalua mkoani Rukwa ambaye alinusurika kuuawa baada ya polisi kumnusuru na hivi sasa amelazwa katika hospitali ya Laela mkoani Rukwa kufuatia kipigo kikali alichopewa.

Wananchi walioshuhudia tukio hilo walieleza kuwa watuhumiwa hao hawajaonewa bali mwenendo wao na kazi wanazozifanya ndizo zinawashitaki na kwamba si hao tu bali kundi lote linahitajika kukamatwa na polisi na kama watashindwa basi wao watachukua hatua stahili.

Aidha hali si shwari kabisa eneo hilo kufuatia baadhi ya watuhumiwa waliotajwa kutoroka na kuziacha familia zao wakiwemo wafanyabiashara wa eneo hilo ambapo mmoja wao aliyejulikana kwa jina moja la Simundwe alihamishwa chini ya ulinzi wa polisi.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Myunga Edwin Sikapizye alithibitisha kutokea kwa matukio hayo na kwamba wanasubiri hatua za polisi za uchunguzi ikiwemo utafutaji wa miili hiyo mitano iliyozamishwa mtoni baada ya kuuawa.
Mwisho

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text