Tuesday, April 26, 2011

HUJUMA nzito zimefanywa dhidi ya chuo cha uuguzi na ukunga cha Mbozi kilichopo wilayani Mbozi mkoani Mbeya zilizosababisha hasara kubwa na kuzusha wasiwasi miongoni mwa jamii inayokizunguka chuo hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika chuoni hapo jana mkuu wa chuo hicho Hiza alieleza kuwa matukio yaliyotokea mfululizo ni pamoja na kutiwa chumvi kwenye injini ya gari STK 3014 aina ya Land Cruiser Machi 14 mwaka huu na kusababisha gari hilo kuharibika.

Tukio la pili ni kuchomwa moto kwa ofisi ya mkuu wa chuo ambapo mali nyingi na nyaraka muhimu ziliteketea zikiwepo kompyuta kubwa 2, laptop 2, photocopy 1 pamoja na samani zilizokuwemo humo ambapo thamani halisi ya mali iliyoharibika bado haijafanywa na mthaminishaji wa serikali.

Pamoja na mambo hayo pia mkuu huyo ameeleza kuwa anaishi kwa hofu kufuatia vitisho anavyopewa ikiwa ni pamoja na kulazimishwa kumteua msaidizi wa mkuu wa chuo ambao wafanyakazi walio wengi walimtaka.

“Nilivyofika hapa mwaka jana Februari wafanyakazi wa ngazi ya chini walikuwa wakinijia mara kwa mara kunitaka nimteue mmoja wa walimu (jina limehifadhiwa) kuwa msaidizi wangu lakini nilikaa kimya nikiangalia ni nani ningemteua ndipo nilipomteua Josephat Kaja kuwa msaidizi wangu na hapo ndipo nilipopokea barua ya kunipa siku 14 nibatilishe uamuzi vinginevyo wangenifanyizia” alieleza mkuu wa chuo.

Baadhi ya wafanyakazi chuoni hapo ambao waliomba majina yao kuhifadhiwa walisema kuwa chanzo cha mgogoro huo ni mfumo wa uongozi ambapo walidai kuwa tangu aje mkuu wa chuo huyo mgeni pamekuwepo mabadiliko makubwa ya namna ya kudhibiti mali ya chuo na kwamba uhuru uliokuwepo wa kufanya watakavyo ulikwisha.

“ Nenda kwenye bwalo la chakula kumenunuliwa viti vipya zaidi ya mia tatu, kumepakwa rangi na kuwekwa marumaru mambo hayo yamefanywa na mgeni huyu ambaye amemaliza mwaka sasa” aliongea mfanyakazi huyo.

Hata hivyo wananchi wameomba kuitishwa kwa mkutano ambapo wanatarajia kupiga kura za kumtaja anayehujumu chuo hicho mbele ya mkuu wa wilaya ya Mbozi na kwamba watamtaka mkuu wa wilaya kuondoka naye mara baada ya kura hizo.

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text