Tuesday, April 26, 2011

JESHI la Polisi wilayani Mbozi mkoani Mbeya limeingia katika kashfa kiutendaji baada ya kuibuka kundi la watu linalofanya vitendo vya kihalifu ikiwepo mauaji ya watu na kuwafanya wananchi wa kata za Itaka, Bara, Nambinzo na Halungu wilayani hapa kuishi kwa hofu.

Kundi hilo ambalo limeanzishwa miezi mitatu iliyopita linalojulikana kwa jina Shulu ikiwa na maana ya kichuguu (lugha ya Kinyiha) na kuwa ni sungusungu wa polisi jamii na kwamba linafanya kazi hizo kwa lengo la kukomesha vitendo vya kihalifu.

Watu waliotajwa kuuawa na kundi hilo ni Saison Mtajiha wa kijiji cha Hangomba ambaye alikamatwa na silaha na Potea Vileji wa kijiji cha Hamwelo na mwingine ambaye jina lake halikuweza kupatikana mkazi wa kijiji cha Utambalila aliyedaiwa kuiba kuku.

Waliopigwa na kujeruhiwa ni Daudi Mwashitete ambaye amevunjwa miguu yote miwili na mkono na amelazwa katika hospitali ya Vwawa, wengine ni Lidia Shinanga, Misheki Msumeno na Weki Jamson wakazi wa kijiji cha Hangomba na Adimin Mdalavuma wa kijiji cha Bara.

Mmoja wa watu aliyepigwa na kuvunjwa miguu yote miwili na mkono mmoja Daudi Mwashitete akiwa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbozi mjini Vwawa alisema kuwa yeye alikamatwa kwa tuhuma za wizi wa mashine ya kukoboa kahawa aliyokuwa amewekeza rehani kwa Yela Mwalupogo.

“Walinifuata shambani na kunikamata na kunipeleka kilabuni ambako nilihojiwa juu ya mashine ya kukoboa kahawa ambayo waliikuta kwa Mwalupogo wakidhani ni mali ya wizi, niliwathibitishia kuwa hiyo ni mashine yangu halali niliyowekeza rehani ili kulipa deni la pembejeo za kahawa la sh 80,000 nilizokopa kwa Julius Mgala lakini hawakunielewa na ndipo walipoanza kunipiga kwa marungu na kunivunja miguu yangu yote na mkono huu wa kulia” alisema kwa uchungu.

Mwashitete aliwataja waliokuwa wakimpiga kuwa ni Japhet Halinga, Peter Howa, Harrison Mwashilindi, Tusoweye Mnkondya na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Nambwama.

Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida sungusungu hao walifika katika hospitali na kumtorosha majeruhi Daudi Mwashitete na kumpeleka kwa mganga wa kienyeji katika kijiji cha Nambinzo ili atibiwe huko na kuondoa ushahidi wa hospitali lakini baada ya majeruhi kupata fahamu alituma ujumbe kwa ndugu zake ambao walimrudisha hospitalini hapo.

Kiongozi wa kikundi hicho Japhet Halinga (au Ngwede) alipohojiwa kwa simu namba 0754 050 667 alikiri kuwakamata watuhumiwa waliotajwa kupigwa akidai kuwa anafanya kazi hizo kwa maagizo ya polisi na kwamba matukio yote hutolewa taarifa zake katika kituo cha polisi Itaka.

“Sisi tukiwakamata huwalazimisha watuoneshe mali walizoiba na wakisumbua ndipo vijana wetu huwashughulikia kama ulivyoona” aliongeza Halinga.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wametajwa kuwa wamekamiwa kuadhibiwa na kikundi hicho na wameshatoa taarifa hizo katika kituo cha polisi Itaka ambapo hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa.

Wananchi hao waliozungumza na mwandishi wa habari hizi ni Langford Philimon, Yangson Shinanga, Williad Mwashilindi, Anjelo Simfukwe, Chilumba Philimon, Oyes Mgala na Juma Mgaya. Wamedai kuwa wamekuwa wakipewa vitisho vya mara kwa mara kwamba siku yao bado inakuja.

Watu hao wameeleza kuwa wanapopeleka malalamiko yao katika kituo cha polisi huambiwa wakatoe taarifa hiyo kwa mwenyekiti wa sungusungu (SHULU) ndiye atakayeshughulikia matatizo yao.

Baadhi ya wananchi walisema hatua ya kukamata wahalifu hatupingi tatizo ni pale wanapowapiga na kuwafanya vilema hapo wanaongeza tatizo kwa taifa. Wameongeza raia hao kuwa kundi hilo likikukamata ukiwa na shilingi 200,000 linakudai ukiwapa wanakuachia ila kama kuna mali ulizokamatwa nazo wanazichukua.

Mkazi mwingine aliyeomba kuhifadhiwa jina lake anasema watu wote walioorodheshwa kukamatwa wanatakiwa angalau kuwa na shilingi 100,000 kama kima cha chini ili ukikamatwa wasikupige kufuatia tishio hilo baadhi ya wananchi wanakimbia wakiziacha familia zao.

Joseph Mwanakulya mkazi wa kijiji cha Itaka akitoa maoni yake juu ya kundi hilo alisema mali za wizi zinakamatwa watu waliopotelewa vitu vyao wanavipata shida ni hivyo vilema wanavyowatia watu pengine wangerekebisha kipigo tungewaona wanafaa.

Nako katika kijiji cha Halambo kata ya Halungu sungusungu hao wamewapiga na kuwajeruhi vibaya Wilinasi Sikanyika na mtoto wake Stephano Wilinas ambao wanapata matibabu katika hospitali ya Vwawa, mtoto akiwa na tuhuma ya kuiba ng’ombe miaka mitatu iliyopita ilihali baba yake alipigwa kwa tuhuma za kutaka kumsaidia mtoto wake ambaye alipeleka malalamiko katika kituo cha polisi mjini Vwawa.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Hangomba Watson Maduguli alipoulizwa juu ya kundi hilo alikiri kuwepo na kwamba kazi wanazofanya hajui utaratibu wake lakini anadhani wilaya inajua. Alipohojiwa juu ya uongozi wa kundi hilo alionekana kujibu kwa mashaka na akaomba apewe muda wa kufuatilia na kwamba anachojua ni kukamatwa kwa watu na kuadhibiwa.

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Utambalila Francis Nzowa alipohojiwa juu ya kuwepo kwa mauaji kijijini kwake alisema kuwa mtu aliyeuawa aliiba kuku lakini taarifa za kifo chake zilipelekwa polisi.

Afisa mtendaji wa kijiji cha Hamwelo Osia Mgala alipohojiwa juu ya mauaji ya Potea Vileji alijibu kuwa huyo aliiba mablanketi ndipo akaadhibiwa na wananchi.

Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya Nicolaus Mbilinyi alithibitisha kuwapokea majeruhi wawili Admin Mdalavuma ambaye ametibiwa na kuruhusiwa na Daudi Mwashitete ambaye alisema anapelekwa katika hospitali ya rufaa jijini Mbeya kufuatia mivunjiko ya miguu na mkono ambapo hawataweza kumtibu katika hospitali yake.

Mkuu wa wilaya ya Mbozi Gabriel Kimoro alipohojiwa juu ya kuwepo kwa kundi hilo alidai kuwa hana habari na kwamba ndiyo kwanza anapata habari kupitia mahojiano hayo.

Mkuu wa polisi mkoani hapa Advocate Nyombi alipohojiwa juu ya kuwepo kwa kundi hilo na vitendo hivyo vya kinyanyasaji vinavyofanywa alikanusha kuwa na taarifa yoyote juu ya kundi hilo na kwamba atafanya uchunguzi.

Hata hivyo polisi hawajachukua hatua yoyote kwa wahusika walio wajeruhi watu hao pamoja na taarifa kupelekwa katika vituo vya polisi vya Itaka na Vwawa hali inayofanya wananchi waishiwe imani na jeshi hilo.

0 comments:

Post a Comment

Thank you for reading the article

Site search

    More Text