Tuesday, August 12, 2008

WANANCHI HATARINI KWA KULA SUMU

Posted by Unknown On 5:08 AM 1 comment
Na Kenneth Mwazembe
Mbozi

AFYA za wakazi wa wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya na Dar es Salaam zipo hatarini kufuatia kula vyakula vinavyohifadhiwa kwa sumu kali, imefahamika.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini maduka ya madawa katika miji ya Vwawa, Tunduma na Mlowo kuuza madawa ya kuhifadhia nafaka aina ya Actellic 50%ec yasiyothibitishwa na Taasisi ya Utafiti ya Arusha (TPRI) yakiwa pia yamehifadhiwa kwenye chupa zinazoonesha kutengenezwa na kampuni ya Sygenta Agro Services AG.

Mazao hayo yanayohifadhiwa kwa sumu kali husafirishwa hadi jijini Dar es Salaam ambako ndiyo kuna soko kuu la mahindi na maharage yanayozalishwa wilayani hapa japo wakati mwingine husafirishwa nje ya nchi yaani Zambia na Kongo.

Utambuzi wa chupa uliofanyika katika maduka mbalimbali katika miji hiyo ulibaini kutofautiana kwa alama chache za maandishi ukilinganisha na zile halisi pia rangi na harufu yake.

Madawa mengine yanayouzwa yakiwa ni bandia ni pamoja na Cuprocaffaro (Copper Oxychloride) Tancopa 50% WP na Round up, Gesaprim 500FW.

Uhifadhi nafaka wa hatari umetokana pia na baadhi ya wafanyabiashara wanaonunua mazao ya nafaka hasa mahindi na maharage ambao wanatumia madawa hatari ya kuua wadudu kama mchwa na vidomozi kupuliza mazao hayo kwa kuhifadhi ghalani.

Sumu zilizobainika kutumiwa kama mbadala wa Actellic ni Dusburn 50EC, Sumithion EC, na Thiodan 50EC ambazo hutumika kuua wadudu kama vidomozi (leaf miner), vidugamba (scales), buu wa shina (stem borer), mchwa na wadudu wengine.

“Kaka huwezi kununua Actellic shilingi 30,000/= kwa lita badala ya 12,000 kwa lita ya Dursban itakayotunza mahindi gunia 100 utakuwa unafanya biashara kichaa” alisema mfanyabiashara mmoja ambaye aliomba jina lake lisitajwe.

Baadhi ya wenye maduka walipohojiwa juu ya tuhuma za kuuza madawa bandia walikiri kuwepo kwa madawa hayo na kwamba husambazwa na vijana wasio waaminifu ambao huyaleta toka Malawi na Msumbiji na mengine yanatengenezwa kwenye viwanda bubu ambavyo vinaaminika kuwepo Uyole kwenye jiji la Mbeya.

“Ni watu wachache wacha Mungu ndiyo wanaweza kukubali kuingia hasara baada ya kuona wameuziwa madawa badnia wanaoweza kuyatupa na kukubali hasara, wengi wanaamua kuuza hadi yaishe ili kurudisha fedha zao” aliongeza mmoja wao.

Afisa Maendeleo ya Kilimo wilayani hapa Nason Kigobanya alipohojiwa juu ya kuwepo madawa madukani yasiyostahili na matumizi ya sumu kali kuhifadhia nafaka alithibitisha kuwepo kwa wafanya biashara wasiowaaminifu na kwamba kwa taarifa hizi atafuatilia na kuchukua hatua.

“Uelewa mdogo juu ya madawa ndiyo sababu kubwa inayowafanya wananchi kununua madawa hayo au pengine bei ndogo inawafanya wanunue dawa zisizofaa” aliongeza.

Afisa wa Afya wilayani hapa Eddo Kyara alipohojiwa juu ya watu wanaoathirika kwa matumizi ya madawa hayo aliahidi kufatilia kwa karibu na kwamba atachunguza ili kubaini wafanyabiashara wanaouza madawa bandia kwa hatua zaidi.

Naye Afisa Biashara wilayani hapa Salehe Ibrahim alipohojiwa juu ya wafanyabiashara kuuza madawa yasiyothibitishwa na TPRI alisema Bodi ya Madawa na Chakula (TDFA) ndiyo wahusika wakubwa na kwamba atawasiliana nao ili waweze kushughulikia mapema iwezekanavyo.

Msambazaji mkuu wa sumu iliyobainika kuwa bandia kampuni ya Mukpardar alipohojiwa kwa simu mtu aliyejitambulisha kwa jina moja la Ketan (Muasia) alijibu kuwa kuna watu Kariakoo wanaotengeneza dawa hizo na kuweka nembo yao ya Mukpardar na kwamba wao hawahusiki kutengeneza hizo dawa zinazodaiwa bandia.

Maelezo zaidi aliyatoa Abduli Razak mfanyakazi dukani hapo ambapo alifafanua kuwa wao wanashindwa kuthibiti utengenezaji huo bandia kwa kuwa kazi hizo zinafanywa na wahuni wa Kariakoo na kwamba wanaiga kila kitu hata wao wanashindwa kubaini bandia na halisi ni ipi.

Hata hivyo kuna kila sababu Wizara ya Afya kutuma wataalam wake ili kufanya uchunguzi kwa miili ya wakazi wa wilayani hapa ili kubaini ni kwa kiwango gain wameathirika na madawa hayo

MWISHO

MAALBINO WAPEWA TSH 1.9 MILIONI

Na: Kenneth Mwazembe – Mbozi

Wahisani mbalimbali wametoa jumla ya sh. Mil.1.9, ikiwa ni msaada kwa chama cha maalbino mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kuendesha semina na mikutano elekezi kwa lengo la kuielimisha jamii kutambua albino kuwa ni sehemu ya jamii yenye ulemavu wa ngozi.

Kiasi hicho cha fedha kilitajwa juzi na Mwenyekiti wa chama hicho Mathayo Mwantemani alipokuwa anahubiri katika ibada iliyoandaliwa maalumu kwa ajili ya kukabidhi msaada huo iliyofanyika katika Kanisa la Moravian Mbozi Mission wilayani Mbozi.

Alieleza kuridhishwa kwake na jinsi jamii ya watanzania walivyoitikia wito wa kuwasaidia ili kuwaokoa albino kwa kuwachangia kiasi hicho cha fedha ambacho kitasaidia kutoa elimu kwa jamii juu ya imani potofu ya kuwaua kwa madai kuwa viungo vyao vinaweza kusaidia kupata utajili.

Mwantemani aliwataja waliochangia kiasi hicho cha fedha kuwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya ambaye ametoa sh. 931,000/=, Benki Kuu sh. Milioni moja na waumini wa kanisa la Moraviani ambao walitoa sh. 33,000/= ikiwa ni mchango wa papo kwa papo katika ibada hiyo.

Mwenyekiti huyo ameitaka jamii kuelewa kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Maalbino) hawakutokana na kasoro za wazazi wao au wazazi kula vyakula ambavyo havitakiwi wakati wa ujauzito bali ni majaaliwa ya Mwenyezi Mungu kwani hakuna anayependa kuzaa vilema na kwamba mtu mwenye mawazo hayo asije akashangaa Mungu anampa albino kwenye ndoa yake.

Alifafanua kuwa mtu mwenye ulemavu wa ngozi (albino) anazaliwa na ngozi nyeupe kutokana na upungufu wa chembe hai aina ya melanin, mtu akiwa na melanin ya kutosha anazaliwa akiwa na ngozi nyeupe ambapo kazi kubwa ya chembe hizo ni kuzuia mionzi ya jua kuharibu ngozi ya binadamu.

Katibu wa Chama hicho mkoa wa Mbeya Sydney Mwamlima alieleza kuwa albino ni sawa na mtu mwingine wa kawaida na ana uwezo sawa na wengine, lakini anakabiliwa na tatizo namna ya kujilinda na mionzi ya jua ambayo ina sumu inayochoma ngozi na kuwa nyekundu inayosababisha vidonda ambavyo hugeuka kuwa kansa ya ngozi.

Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwepo kwa mila potofu ambazo zinawafanya wakunga wa jadi kuwaua watoto wanaozaliwa na ulemavu wa viungo wakiwemo maalbino kabla hawajatolewa nje (wenyeji huita Mushiyumba) ambapo mtoto hutolewa rasmi.

MWISHO.

Monday, August 11, 2008

Wananchi wagomea ukarabati zahanati

Posted by Unknown On 7:16 AM No comments
Na Kenneth Mwazembe, Mbozi

WANANCHI wa Kijiji cha Mpemba, wilayani Mbozi, Mbeya, wamekataa mpango wa serikali wa kukarabati zahanati ya kijiji hicho na badala yake wanataka jengo hilo lijengwe upya.

Hali hiyo ilibainika juzi wakati mkandarasi alipopelekwa kijijini hapo, ili kuweka sahihi mkataba huo wa ukarabati ambapo wananchi kwa pamoja walikataa na kuomba fedha iliyotolewa milioni 14 zitumike kujenga jengo jipya.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, John Sinyinza, alisema jengo hilo lilijengwa kwa udongo na limeliwa na mchwa na hivyo kufanya ukarabati kuwa mgumu kwa kuwa limeoza na kwamba hakuna maana kukarabati.

Alisema kijiji hicho chenye wakazi 10,000 kinahitaji kuwa na huduma ya afya ya uhakika na kwamba wao kama wananchi wameshaanza kukusanya mawe kwa ujenzi wa kituo cha afya na si zahanati.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Julius Kamwela, alisema wananchi kupitia mkutano mkuu wa kijiji wamekataa ukarabati huo na kwamba wamepeleka miniti za mkutano kwa mkurugenzi wakipinga ujenzi na kudai ujenzi mpya.

Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God, Justus Sinkonde, alidai kutokana na kijiji hicho kuwa kiungo kati ya Zambia na Malawi idadi ya wakazi inaongezeka kwa kasi na hivyo kuona haja ya serikali kujenga kituo cha afya badala ya zahanati.

Wananchi kwa nyakati mbalimbali waliiambia Tanzania Daima kuwa sh milioni 14 zilizotengwa zikiongezwa na nguvu za wananchi zitaweza kukamilisha ujenzi wa zahanati mpya na kwamba kama serikali itawaunga mkono basi watajenga kituo cha afya.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya, Egifrid Mwingilihela, alithibitisha kuwapo mgomo huo na kwamba atafanya mazungumzo na uongozi wa kijiji, ili kupata ufumbuzi.

Hata hivyo, aliulaumu uongozi wa kijiji ambao ulikaa kimya wakati wa kufanya tathmini na walisaini makubaliano ya ukarabati na si kujenga upya.

Aliongeza kuwa iwapo hawatakuwa tayari kukubali ukarabati idara yake itahamisha mradi huo, kwani unatakiwa kwisha haraka.

Friday, August 1, 2008

DARAJA LA LUASHO - MTO MOMBA

Posted by Unknown On 6:06 AM No comments
Daraja hilo lipo Mto Momba wilayani Mbozi, mto wenye mamba wengi, mamba hao ni tishio kwa usalama wa binadamu. yamekuwa yakiripotiwa matukio kadha wa kadha kuhusiana na mamba hao. Juzi mtoto Lucia Osward (9/12) aliliwa na mamba na mama Bahati Kawepa (28) akiokolewa akiachwa na majeraha makubwa ambayo nusura apoteze nyeti zake.

Kama si ujasiri wa mume wake mama huyo aliyefika na kutoa msaada kwa kuingiza mkono kinywani mwa mamba na kumshika ulimi huku akisaidiwa na mwanamke mwingine aliyevuta mkia na kujitahidi kumkokota nje ya maji mamba huyo leo ingekuwa habari nyingine.

MTOTO AKATISHWA MASOMO ILI AOLEWE, BABA YAKE AKAMATWA NA KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Na Kenneth Mwazembe
Mbozi
Licha ya jitihada za serikali kutimiza malengo ya pili ya Milenia ya kutoa elimu ya msingi kwa watoto wote kuna baadhi ya wazazi waliojitokeza kuwa kikwazo cha malengo hayo kwa tamaa ya kujipatia mali kwa kuwaoza wasichana.
Giveness Edward (19) mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Hangomba wilayani Mbozi mkoani Mbeya amekatishwa masomo na baba yake na kutakiwa aolewe.
Mkasa wa kusikitisha unaomhusu mtoto huyo ulianza mapema mwaka huu ambapo baba yake alitofautiana na binti yake huyo baada ya mzazi huyo kumkataza kuabudu kwa madai kuwa imani ya Kikristo aliyonayo binti huyo imemfanya asimsikilize baba yake ambaye alimtaka kuolewa.
Giveness akizungumza na mwandishi wa habari hizi amesema kuwa baba yake Edward Kamgodi Mwapule alimkatisha masomo pale alipomkamata na kumfunga kamba kisha kumpeleka kwa mganga wa kienyeji ili kumnywesha dawa ambazo zingemfanya mtoto kumtii baba yake kwa kila alitakalo.
Kabla ya tukio hilo baba yake alimpiga mtoto huyo kwa mpini wa shoka na kumsababishia maumivu ya miguu ambapo mtoto alilazimika kupata PF 3 ya polisi na kutibiwa katika zahanati ya Itaka.
Kipigo hicho kilimfanya Afisa Mtendaji wa kata ya Itaka Lukosomolo Ndimbwa kumshikilia kwa muda mzazi huyo asiye huruma na ambaye anathamini ng’ombe kuliko elimu hadi mtoto alipopona.
Hata hivyo Giveness anasema kuwa hatua ya serikali kumshikilia baba yake kwa kosa hilo baba yake aliapa kumuua kisha naye kujiua, ndipo alipolazimika kukimbilia nyumbani kwa mwenyekiti wa kijiji Askofu Mbazu ambaye alimpokea na kumhifadhi na kuruhusu mtoto huyo kuendelea na masomo akitokea nyumbani kwa mwenyekiti huyo.
Hali ilibadilika usiku wa 27 Mei mwaka huu mwenyekiti alipokula njama na mzazi wa Giveness, ambapo usiku majira ya saa 9 baba huyo akiongozana na watoto wake wawili Shida Edward na Mashaka Mwampashe walifika nyumbani kwa mwenyekiti na kubisha hodi, mwenyekiti alifungua mlango na kusaidia kumfunga mtoto huyo mikono kwa kamba na kisha kuondoka naye hadi kijiji cha Wasa kwa mganga wa kienyeji aitwae Chilaka umbali wa kilometa 40 ili kumnywesha dawa za kuondoa imani ya kikristo na kumpandikiza uchawi.
Kwa nasibu Mungu alimnusuru binti huyo ambaye anaeleza kuwa mara baada ya kufika kwa mganga huyo walikaribishwa kula chakula, yeye alizuiwa kula hadi atakaponyweshwa dawa hizo, hali iliyomfanya binti huyo kuomba aoneshwe msalani na kutumia mwanya huo kutoroka na kukimbia hadi kijiji cha pili ambako alipata msaada wa kuoneshwa njia ya kwenda mjini Vwawa ambako pia Wasamaria walimsaidia usafiri hadi Mbeya mjini.
Mtoto huyo ambaye hadi sasa anahifadhiwa na wasamaria amefikishwa katika kituo cha polisi mjini Vwawa ambao wamechukua hatua za kuwatafuta watuhumiwa wote wanne ili kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili za unyanyasaji na kumzuia masomo.
Kaimu Afisa Elimu wilayani hapa Juma Kitabuge alieleza masikitiko yake kwa mkasa uliompata binti huyo na kueleza kuwa hali hiyo inaweza kumwathiri kimasomo, akaahidi kumsaidia kuhakikisha anaendelea kusoma katika shule jirani ambapo ataendelea kulelewa na wafadhili hadi atakapofanya mtihani miezi michache ijayo.
Jeshi la Polisi wilayani hapa limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari limeshamkamata baba yake binti huyo na kwamba atafikishwa mahakamani wakati wowote.
Mwisho


MENEJA WA PENTAGON SECURITY AFUNGIWA NDANI YA OFISI

Walinzi wa kike wa kampuni ya Pentagon Security Guards inayofanya kazi ya ulinzi wilayani Mbozi mkoani Mbeya jana waliwafungia mameneja wao ofisini baada ya wakubwa hao kukataa kuwalipa mishahara yao .

Hatua hiyo ilichukuliwa na walinzi wawili Maria Sinyinza na Lucy Nashiuya ambao waliwafungia ndani ya ofisi Meneja wa Tawi la Mbeya Charles Makwaza na Meneja wa Kituo cha Mbozi Lt. Mstaafu Mwaijibe wakishinikiza kulipwa mishahara yao baada ya mkataba wa ulinzi baina ya kampuni hiyo na kampuni ya China Road & Bridge kumalizika.

Awali kabla ya tukio hilo Makwaza alilipwa mishahara hiyo na kampuni ya Kichina ambapo walinzi hao walimdai awalipe mishahara hiyo kabla hajaondoka kurudi mjini Mbeya, meneja huyo alikataa ombi hilo na kuwaeleza kuwa hamlipi mtu kwa kuwa mkataba umekwisha na kwamba wao kama walinzi wameajiriwa moja kwa moja na kampuni ya kichina hivyo haoni sababu ya kulipa fedha hizo.

Hata hivyo meneja huyo alilazimika kuvunja dirisha la ofisi hiyo na kutoroka bila kuwalipa fedha hizo.

Maria Sinyinza alieleza kuwa wao wanadai haki yao waliyofanya kazi kabla hawajaajiriwa na CRBC na kwamba wamechukua hatua hiyo kwa kuwa meneja huyo amekuwa anawanyanyasa kwa kuwakata mishahara yao kwa visingizio visivyoeleweka na kwamba yeye anadai jumla ya shilingi 70,000 ikiwa ni mshahara wa miezi mitatu.

Meneja wa tawi alipotakiwa kueleza tukio hilo alithibitisha kuwa yeye na bosi wake walifungiwa ndani ya ofisi ambapo bosi wake alilazimika kutumia mbinu za medani kwa kuvunja dirisha na kutoroka kupitia dirisha hilo.

Alipohojiwa kwa simu juu ya tuhuma za kudhulumu wafanyakazi hao mishahara, Meneja wa Tawi Charles Makwaza alikiri kufungiwa na kwamba kwake hayo ni matukio ya kawaida na kwamba fedha wanazodai siyo nyingi haziwezi kuwaathiri.

Uchunguzi umebaini kuwepo ka malalamiko ya walinzi juu ya kukatwa fedha kwa visingizio mbalimbali ikiwemo kupotea kwa baadhi ya mali katika malindo yao na kwamba vitendo vya wizi vinavyofanywa na baadhi ya walinzi wasio waaminifu vinatokana na malipo duni wanayolipwa na waajiri wao.

Aidha malalamiko ya wafanyakazi hao yamebainisha kuwa wamekuwa wanalipwa shilingi 10,000 kwa mwezi baada ya kukatwa sh 30,000 hali inayowafanya walinzi waishi maisha magumu.

MWISHO
Na Kenneth Mwazembe
Mbozi

MTOTO Lucia Osward mwenye miezi 9 juzi aliliwa na mamba huku mama yake Bahati Kawepo (28) mkazi wa Irambo Ivuna wilayani Mbozi mkoani Mbeya akinusurika kifo baada ya kukamatwa na mamba alipokuwa akivuka mto Momba.

Akielezea mkasa huo uliomfanya apoteze mtoto wake Lucia Osward (9/12) akiwa amelazwa katika wodi la wanawake na watoto katika hospitali ya mjini Vwawa, alisema kuwa juzi jioni saa 2 usiku akitokea kijiji cha Ivuna kusaga mashineni akiwa anavuka mto ndipo mamba alipotokea na kumng’ata sehemu za siri ambazo nusura aziondoe kabisa.

“Nilipiga kelele za kuomba msaada ndipo mume wangu alipofika na kumshika mamba ulimi na mwanamke mwingine aliyefika kutoa msaada alimshika mkia mamba wakawa wanamvutia nchi kavu ndipo aliponiachia na kuninyang’anya motto aliyakuwa mgongoni na kukimbia naye” anamalizia mama huyo.

Mama huyo alipelekwa katika kituo cha afya cha Kamsamba kwa mkokoteni uliokokotwa na ng’ombe na kupewa matibabu ya awali na kukimbizwa katika hospitali ya wilaya ambako anaendelea na matibabu.

Mganga Mkuu Egfrid Mwingirihela ameeleza kuwa majeruhi huyo alijeruhiwa vibaya sehemu za siri na kutenguka bega la kushoto na majeraha ya vidonda kichwani na miguuni na kwamba hali yake inaendelea vizuri.

Habari kutoka Kamsamba zimeeleza kuwa msako mkali unaendelea dhidi ya mamba huyo aliyemla mtoto ukishirikisha wanakijiji waishio jirani na eneo hilo .

Ziwa Rukwa linaaminika kuwa na mamba wengi kuliko samaki na hivyo kuwafanya wananchi wanaoishi jirani na ziwa hilo kuishi kwa mashaka, pengine umefika wakati wa serikali kuvuna mamba hao ili kuwapunguza au kuwafuga kitaalam na kunusuru maisha ya wenyeji.

KATIKA hospitali hiyo hiyo, jana jioni mwanamke mmoja Morina Sichone (22) mkazi wa kijiji cha Nambala wilayani hapa alijifungua kitu cha ajabu baada ya kuwa mjamzito wa miezi 8.

Akieleza mkasa huo uliovuta hisia za watu na kuhusisha kitendo hicho na ushirikina, Sichone alisema kuwa yeye alijihisi mjamzito tangu mwezi wa Novemba 2007 na kwamba alihudhuria kliniki katika hospitali ya wilaya ambako walimfungulia kadi na kuthibitisha kuwa ilikuwa mamba.

Ni miezi miwili iliyopita hakusikia kucheza kwa mtoto hadi jana alipojisikia uchungu na kufika katika wodi la wazazi ambapo alijifungua kiumbe hicho kilichokuwa kama yai ambacho alilazimika kukipeleka kwa wakwe zake ili wasijedai kuwa ameuza mtoto.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Egifrid Mwingirihela amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba bado wahawajaweza kutambua ni kitu gani kilisababisha hayo.
MWISHO



Katika tukio jingine MCHUNGAJI

Mchungaji Silas Mwamwezi wa kanisa la Moravian wilayani Mbozi wiki iliyopita alizuiwa kufungisha ndoa katika kijiji cha Mpela baada ya kubainika kuwa bibi harusi alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha III katika shule ya Ipunga wilayani Mbozi.

Zoezi la ufungaji ndoa baina ya Hamisi Zawadi Mnkondya na Maria Makanga (20) lilizuiwa na Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Ihanda Blaya Msongole aliyefika na mgambo hapo kanisani na kumkamata bwana harusi na kumpeleka kituo cha polisi mjini Vwawa.

Afisa huyo alieleza kuwa alipewa taarifa na Mkuu wa shule hiyo kuhusu kuozwa kwa binti huyo ambapo alilazimika kwenda na kuzuia Ibada hiyo isifanyike ambapo tayari shamla shamla zilikuwa zimeshaanza na walikuwa hatua za awali za kuvishana pete.

Aidha Msongole alisema kuwa jitihada za kumtafuta Rosta Mnkondya ambaye ni mama yake bibi harusi anatafutwa kwa tuhuma za kumuoza kwa ng’ombe mbili ilihali akijua kuwa binti yake ni mwanafunzi.

Mkuu wa shule Daniel Kasomo alipohojiwa juu ya tukio hilo alisema kuwa Maria ni mwanafunzi mtoro tangu Aprili mwaka huu alipoacha kuhudhuria masomo na kwamba alipopata taarifa za ndoa hiyo alitoa taarifa kwa uongozi.

Naye Mchungaji Silas Mwamwezi alipohojiwa juu ya yeye kufungisha ndoa na mwanafunzi alisema anasikitika kwa tukio hilo , yeye ni mchungaji wa usharika wa Vwawa makao makuu ya wilaya katika jimbo hilo na kwamba aliitwa kufungisha ndoa hiyo bila kujua kuwa kuna mwanafunzi kati ya maaharusi hao kwani kanisa lake haliruhusu wanafunzi kuolewa.

Polisi wilayani hapa wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba bwana harusi anashikiliwa na polisi ambapo atafikishwa mahakamani mara uchunguzi ukishakamilisha.

MWISHO

Site search

    More Text